27.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 20, 2023

Contact us: [email protected]

CCM yapiga marufuku wazazi kuwatumia watoto wa kike kwenye shughuli za kimila

Na Ashura Kazinja, Morogoro

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Daniel Chongolo amepiga marufuku tabia za wazazi na walezi nchini kuwatumia watoto wakike katika shughuli za kimila ikiwemo kuwacheza ngoma na kuwaozesha mapema kwa kuwageuza chombo cha kujipatia mali na mitaji bali wawasomeshe ili waweze kuwasaidia zaidi baadae.

Chongolo amesema hayo wakati akizungumza na wanachama wa CCM shina namba mbili lililopo kwenye Kijiji cha Kiroka wilayani Morogoro ambapo alisema kumsomesha mtoto wa kike ni mtaji mkubwa sana kwa sababu anapofanikiwa hawezi kuwaacha wazazi wake wakihangaika tofauti na mtoto wa kiume ambaye huelemea kwa mke aliyemuoa.

“Katika wilaya hii hatupatii kipaumbele watoto wa kike katika suala la elimu bali hukimbilia kuwacheza ngoma na kuwaozesha kwa lengo la kupata mali, tutambue kuwa mtoto wa kike sio chombo cha kupatia fedha, wala mali, wala utajiri kwa kumuozesha bali ukimsomesha itamsaidia kupata kazi nzuri, na mshahara mzuri utakaomuwezesha kuwalea wazazi wake hata atakapoolewa,” alisema.

“Wazee acheni Mambo ya kupokea mahali na kuwekea ahadi watu juu ya kuwaoza watoto wenu, muendelee kuwalea kimaadili na elimu ili muwafanye kuwa watoto wanaoweza kuajiri wengine na sio wao kuajiriwa kuwa watumishi kwenye nyumba za watu” alisema Chongolo.

Alisema tabia hiyo ya wazazi isipodhibitiwa itaendelea kuwa kigingi kwa watoto wengi wakike wilayani Morogoro kutoonja radha ya elimu .

Hata hivyo aliwataka wazazi kujenga tabia ya kujua mienendo ya vijana wao na kufuatilia kazi wanazofanya hasa wanapopata mafanikio wajue wamepataje ili kuepukana na kupata watoto wenye tabia za udokozi na wizi.

“Ukimuona mwanao mwizi au wanamwambia mwizi maana yake umeacha malezi, msiwashangilie watoto wanapokuja na mafanikio, jueni mafanikio hayo yamekujaje, sababu mtoto ni bodaboda, anapata hela ya kipande ya kumpa bosi na ya kula mwenyewe, baada ya miezi miwili anakuja na boda yake anakwambia anampa mtu amuendeshee, ulizeni wamepata wapi,” alisema Chongolo.

Hata hivyo, alikemea tabia za jamii kuzingatia mila potofu kwa wagonjwa wakiwemo kinamama wajawazito ambao huwapa dawa na kuacha kuwakimbiza hospitali na kuhatarisha uhai wao.

Aidha aliwatoa hofu wakazi wa vijiji vya eneo hilo kuwa barabara ya Bigwa – Kisaki itajengwa kwa kiwango cha rami na kurahisisha usafiri na usafirishaji bidhaa Wilayani humo ambapo aliagiza TANROADS kuhakikisha wanaweka taa za barabarani kilometa 10 kila panapokuwa na mji.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Morogoro, Mhandisi Alinanuswe Kyamba alisema ujenzi wa barabara ya Bigwa – Mvuha- Kisaki – Bwawa la Mwalimu Nyerere kwa kiwango cha rami unatarajia kuanza mwezi Juni mwaka huu.

Mhandisi Kyamba alisema ujenzi wa barabara hiyo utahusisha ujenzi wa madaraja yote ikiwemo la mto Ruvu na Mvuha.

Naye Meneja wa Wakala wa usambazaji nishati ya umeme (REA) Taifa, Mhandisi Romanus Lwena alisema kwa Sasa wapo katika hatua ya kukamilisha kuweka umeme kwenye vitongoji vyote nchini huku wakiwa tayari wameshaweka umeme kwenye vijiji vyote 12,245 vya Tanzania.

Mhandisi Lwena alisema Tanzania ina jumla ya vitongoji 64 ambapo 32 kati ya hivyo tayari walishaweka umeme na Sasa wanamalizia vijiji Vilivyobaki.

Awali Katibu wa siasa na uenezi CCM NEC Taifa Sophia Mjema aliwataka wanachama wa CCM kuendelea kukiimarisha Chama kwa kutaja na kusema mema yote ambayo yamefanywa ili kuifanya jamii kutokuwa na maswali .

Mjema alisema maendeleo yote yaliyotendeka na yanayotendeka yametokana na mafanikio ya Serikali ya CCM.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles