25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Kalemani azindua ujenzi kituo cha kupoozea umeme Simiyu, atoa maagizo…

Na Derick Milton, Simiyu

Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani ameweka jiwe la msingi ujenzi wa kituo cha kupozea umeme ambacho katika mkoa wa Simiyu ambacho kitagharimu kiasi cha Sh Bilioni 75 hadi kukamilika kwake, huku akitoa maagizo kwa Tanesco kuhakikisha mradi huo ujenzi wake unaanza mara moja na kukamilika kwa wakati.

Kituo hicho kitajengwa eneo la Imalilo mjini Bariadi, ambapo kitakuwa na uwezo wa kitazalisha Megawati 100 huku mahitaji ya mkoa huo yakiwa ni Megawati 12 na ujenzi utafanywa na TANESCO kupitia wataalamu wake wa ndani.

Kabla ya kuweka jiwe la Msingi jana, Dk. Kalemani alisema kuwa mradi huo ni mkubwa ukiwa na kilovolti 220 ambapo utazalisha umeme mkubwa utakaotosha kwa matumizi ya viwanda vikubwa, vya kati na vidogo na hatimaye kukidhi mahitaji ya mkoa wa Simiyu.

“Ujenzi wa mradi huu ni miezi 12 lakini nataka ukamilike kwa muda na si lazima itimie miezi kumi na mbili hata miezi tisa sawa, mradi huu utachochea shughuli za uchumi na umeme utasambaa vijijini na utatosheleza mahitaji ya mkoa…wananchi wanaozunguka mradi huo niwatake kuwa wasimamizi kwa kuulinda na kuutunza lakini TANESCO mtoe kipaumbele cha ajira za kawaida kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo kwenye shughuli za ujenzi,” alisema Dk. Kalemani.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dk. Tito Mwinuka, amesema mradi huo utakapokamilika unatarajiwa kufungua fursa mbalimbali za maendeleo ya uchumi na uwekezaji wa viwanda mkoani hapa na tayari wameshafanya uthamini wa ekari 15.5 zenye thamani ya Sh milioni 46.7.

Akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Simiyu, mkuu wa wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga, amesema kitendo cha umeme kufika maeneo mengi mkoani hapo kitakuwa kichocheo kikubwa cha kukuza uchumi na hivyo kuongeza idadi ya mabilionea.

Kwa upande wake Kaimu Meneja TANESCO Mkoa wa Simiyu, Alistidia Clemence, amesema baada ya utekelezaji wa mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza mkoa umebaki na vijiji 187 ambavyo havijapatiwa huduma ya umeme.

Martin Mata ni mkazi wa Imalilo amesema wamepokea ujio wa kituo hicho kwa mikono miwili na kuahidi kushirikiana na wananchi wenzie kukilinda kituo hicho.

Ujenzi wa kituo hicho mbali na kutajwa kuchochea uchumi wa mkoa kukua, utaondoa kabisa changamoto kubwa ya kukatika katika mara kwa mara kwa umeme katika mkoa huo ambapo sababu kubwa ambazo zimekuwa zikitajwa ni kutokuwepo kwa kituo hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles