29.8 C
Dar es Salaam
Sunday, September 15, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Bashiru ataka barabara za malori kutengwa kuepusha ajali

Ashura Kazinja-Morogoro

KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema ni vyema Serikali ikaona umuhimu wa kutenganisha barabara za kupita magari ya mizigo na ya kawaida ili kuepusha hatari kwa wananchi.

Dk. Bashiru aliyasema hayo jana wakati alipotembelea majeruhi waliopata ajali ya moto wa lori la mafuta lililoanguka mkoani Morogoro.

Mbali kutembelea majeruhi waliolazwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, pia alitembelea chumba cha kuhifadhia maiti, kuomba dua makaburini na eneo la Itigi-Msamvu ambako lori hilo lilipinduka kabla wananchi hawajalivamia kuiba mafuta na baadaye moto kulipuka.

Alisema kutenganishwa huko kutasaidia magari makubwa kutopita maeneo ya makazi ya watu na hata kukitokea majanga kama ya moto, wananchi hawataweza kupata madhara.

Hata hivyo, aliishauri Serikali kuweka utaratibu wa kutoa elimu ya majanga ya moto ili wananchi waweze kuwa na uelewa mara zote na kuweza kukaa mbali na matukio ya moto ikiwemo yanapoanguka magari ya mafuta.

Akizungumza na wananchi jirani na eneo la tukio lilipotokea, Dk. Bashiru aliwataka kutokata tamaa baada ya kufiwa na ndugu zao na watu wao wa karibu ambao ni nguvu kazi ya taifa kwani kifo hupangwa na Mungu.

“Hili ni janga la kitaifa, poleni sana, kwani wengi wamejeruhiwa na kufa, lengo letu ni kuendelea kuwafariji na kuangalia changamoto zilizopo ikiwemo upande wa majeruhi kwa ajili ya kupatikana madawa,” alisema.

Alisema Serikali na wananchi hasa vijana wakiwemo wa CCM wameonyesha ushirikiano mkubwa wa kusaidia mambo mbalimbali, ikiwemo kupeleka maiti na majeruhi hospitali kutoka eneo la tukio kwa haraka.

Aidha aliipongeza Serikali ya awamu ya tano kwa kuimarisha sekta ya afya na kufanya majeruhi wa ajali hiyo kuishia kutibiwa kwenye hospitali za ndani badala ya kupelekwa nje ya nchi, na kwamba hiyo ni hatua kubwa iliyopigwa.

SAMPULI 85 ZA DAMU ZACHUKULIWA

Kaimu Mkurugenzi idara ya Sayansi, Jinai na Huduma za Vinasaba, David Elias, alisema tangu tukio limetokea hadi sasa, wameshachukua sampuli 85 za damu za watu, ili kuwawezesha ndugu kutambua marehemu wao, au walio majeruhi hospitalini.

Elias alisema sampuli hizo zimepelekwa Kitengo cha Kupima Vinasaba (DNA) Dar es Salaam na kwamba majibu yatatolewa wiki mbili baada ya kupelekwa kwenye mashine.

Alisema wananchi waliochukua miili ya ndugu zao na kuizika ni wale walioitambua kutokana na alama mbalimbali za miili yao, na kwamba licha ya kuchukua au kutambua miili hiyo, sampuli zao zimepelekwa kwenye mashine na majibu yatapatikana.

RC ATAKA MAJERUHI WAOMBEWE

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Steven Kebwe, alisema siku ya tukio alilazimika kupanda lori la mawe ili kuwahi kwenye eneo la tukio baada ya gari lake kuwa katika majukumu mengine.

Alisema alijaribu kupiga simu kuita taxi, lakini ilichukua muda mrefu kufika na hivyo kulazimika kupanda lori.

Akizungumzia majeruhi, alisema kiafya mgonjwa aliyeungua moto kwa asilimia 50 nafasi ya kupona kwake hubaki kuwa ni asilimia 2, hivyo ni jambo la busara kuzidi kuwaombea majeruhi waliopo Muhimbili wapone.

Alisema majeruhi 16 waliopo Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro wanaendelea vizuri huku wengine wakiwa na uwezo wa kujieleza.

MAJERUHI ASIMULIA ALIVYOJERUHIWA

Mmoja wa majeruhi, Boniphace Steven, alisema alikuwa akienda kazini kwake Islamic Foundation, na alipofika eneo lori hilo lilipoanguka, alisimama kushangaa ndipo moto ulipolipuka na yeye kujikuta miongoni mwa wahanga.

MADAWA NA VIFAA TIBA

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Morogoro, Dk. Kusirye Ukio, mbali na kupongeza juhudi za Serikali na wanachi katika michango yao ya hali na mali, mchango mkubwa unaohitajika zaidi kwa sasa ni madawa na vifaa tiba ili kuwawezesha madaktari na wauguzi kufanya kazi kwa weledi zaidi.

“Tumeona juhudi za Serikali na wananchi kuunga mkono katika kuchangia zoezi hili, labda niwakumbushe wasamaria wema kuwa tungependa kupata vitu zaidi kuliko fedha kwani tuna imani kuwa hiyo ndiyo dhamira ya kupigania uhai wa wagonjwa,” alisema Dk. Ukio.

SHUKURANI KWA SERIKALI

Mwenyekiti wa Mtaa wa Suma uliopoteza watu 19, Khamisi Totoro, aliishukuru Serikali kwa juhudi walizoonyesha na kuweza kuwapa ushirikiano toka mwanzo wa tukio hadi sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles