25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Bashiru aonya soko la kura CCM

Andrew Msechu -Dar es salaam

KATIBU Mku wa CCM, Dk. Bashiru Ally, amewaonya wanachama wa chama hicho waliogeuza uchaguzi ni sawa na soko la kununua au kuza kura huku akisema sasa hawana nafasi.

Pamoja na hilo amesema chama hicho hakitamwacha yeyote atakayehuska katika rushwa, wakati ikielekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa Oktoba mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Kauli hiyo aliitoa jijini Dar es Salaam jana, alipokuwa akizungumza na wanachama wa CCM Jimbo la Kawe, ambapo alisema kuwa rushwa imekuwa ikifanywa kwenye soko la kura imekuwa chanzo cha mvurugano wakati wa kuelekea katika chaguzi, suala ambalo halitavumiliwa.

Alisema matokeo ya rushwa katika kutafuta nafasi za uongozi yamekuwa na maumivu kwa wagombea na kusababisha kupata vipongozi wasiostahili, ambao mwisho wake hawawezi kuwa watumishi wa wananchi.

“Rushwa inayotumika kwenye soko la kununua kura imewaumiza wengi. Imeumiza wote, walioshinda na walioshindwa kwa sababu wote wanajikuta katika madeni.  Walioshindwa hawana raha wanaendelea kuugulia wakiwa hawajui ni kwa namna gani watarejesha kile walichopoteza.

“Kwa upande wa walioshinda, pia wanakuwa hawana raha, muda wote wanawaza kutafuta fedha kwa ajili ya kulipa madeni. Hawawezi kuwa na muda wa kuwasikiliza na kuwatumikia waliowachagua kwa kuwa wanaona kuwa wamenunua nafasi hizo,” alisema Dk. Bashiru

Alisema kwa sasa chini ya uenyekiti wa Rais Dk. John Magufuli chama hicho kinahakikisha kuwa utaratibu wa soko la kura unakwisha ili kutoa nafasi kwa wanachama wenye uwezo na nia wajitokeze na kuomba kuchaguliwa kupitia mifumo halali isiyoruhusu rushwa.

Kutokana na hali hiyo alitangaza hadharani namba yake ya simu huku akiwataka wanachama kutoa taarifa pindi wanapoona kuna vitendo vya aina hiyo.

Katibu Mkuu huyo wa CCM aliitaja namba yake hadharani yenye namba 0754 …915  ambapo alisema kuwa ipo wazi kila siku kuanzia saa 10 alfajiri hadi saa 12 asubuhi kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi, hivyo kwa yeyote atakayekuwa ana taarifa zinazohusu rushwa katika chaguzi ampe taarifa.

“Ninawapa namba yangu ili kama kuna watu wanapanga bei ya kura mnipe taarifa. Tunataka kukomesha kabisa rushwa, wewe nitaarifu tu, tutaweka mtego tutawakamata,” alisema.

Alisistiza kuwa rushwa katika chaguzi za ndani za chama zimekigharimu chama hicho kwa hiyo ni jambo ambalo halitafumbiwa macho kwa sasa.

MSHIKAMANO

Katibu Mkuu huyo wa CCM alisema kuwa mshikamano wa chama hicho umekuwa ukitatizwa sana wakati wa kuelekea  kwenye uchaguzi kutokana na baadhi ya watu kuunda makundi ya uchaguzi, suala ambalo halitakiwi kuvumiliwa kwa sasa.

Alisema uongozi wa chama hicho unaendelea kukemea na kufuatilia kwa karibu watu wanaoanzisha makundi yenye nia ya kugawa wanachama na chama wakati wakielekea katika chaguzi hizo kubwa zinazokuja.

Alisema ni wazi kwamba makundi wakati wa uchaguzi yamekiumiza chama hicho hasa katika Jiji la Dar es Salaam hivyo kukosa majimbo karibu yote, hivyo kuwapa kazi kubwa ya kutafuta namna ya kuyarejesha.

Alisema japokuwa mwanachama yeyote ana haki ya kuwania au kugombea nafasi yoyoye ya uongozi, ni vyema wale wenye nafasi ndani ya chama wanatakiwa kukaa na kuwajadili wagombea waridhike na nafasi zao kwa kuwa tayari walishapewa dhamana ya uongozi na wanachama.

Alisema kuwa hao ni wale waliochaguliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo ukatibu na uenyekiti katika ngazi zote, ambao kuna taarifa kuwa baadhi yao wanapanga kuachia nafasi hizo ili kugombea nafasi nyingine.

“Mimi nawashauri wenye nyadhifa zao wabaki nazo ili waendelee kuwasimamia wengine. Wale wote ambao walijitokeza katika uchaguzi wa ndani wa chama mwaka 2017 na wakaaminiwa, wakapewa dhamana watulie.

“Hawa ndio wale wanaotakiwa kukaa na kuwajadili wengine, na siyo wao kuomba kujadiliwa. Ni kweli kwamba mwanachama yeyote ana haki ya kugombea, iwapo wataamua kufanya hivyo, msiwanyime fomu, wapeni, halafu wakija kujadiliwa waulizeni, kwanini uko huku wakati sisi tulikupa dhamana na tulitegemea uko kule? Wasiwasi wangu ni kwamba watakosa kote,” alisema.

Alisema ushauri huo una nia ya kujenga umoja katika chama na kuepusha mivutano, ili kukipa ushindi katika chaguzi zijazo.

Alisema pamoja na mivurugano iliyojitokeza, anaona fahari kwa kuwa tayari wamesharejesha majimbo 10 yaliyokuwa yamechukuliwa na upinzani, yakiwemo ya Temeke, Kinondoni na Ukonga jijini Dar es Salaam.

Alisema kazi nzuri ya ‘kutega mitambo’ ambayo amekuwa akiifanya katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita imesaidia kurudisha pia Jimbo la Monduli na kumurudisha Edward Lowassa katika chama hicho, lakini pia kurudisha majimbo mengine ya Liwale na Serengeti.

KUNUNUA WAPINZANI

Katika mkutano huo Dk. Bashiru, aliwapokea wanachama wanane  waliokuwa Chadema ambao  walikuwa viongozi katika Jimbo la Kawe,  ambapo alisema CCM hakinunui wanachama hao kutoka upinzani kama inavyodaiwa.

Alisema ni wazi kwamba wapo watu kutoka upinzani ambao wamekuwa wakijaribu kujinadi kwa kutaka fedha ili warudi lakini chama hicho hakina utaratibu huo.

“Ni kweli kwamba kuna viongozi wengi kutoka upinzani ambao wametambua na kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli, lakini katika wote wakiwemo wabunge 10 waliorejea hakuna hata mmoja tuliyemnunua kwa pesa.

“CCM ni chama cha ukombozi, hakiwezi kununua watu. Wapo wanaojaribu kujiuza, aibu kwao. Waache kujipeleka utumwani, hatuna sababu ya kununua watu. Tena yupo mmoja nitamtaja wakati ukifika,” alisema Dk. Bashiru

Kwa muda wa wiki mbili sasa ziara hiyo ya Katibu Mkuu wa CCM katika Mkoa wa Dar es Salaam imekuwa ni mwiba kwa vyama vya upinzani ambapo vimekuwa vikilalamikia navyo viruhusiwe kufanya mikutano jambo ambalo Jeshi la Polisi lilinukuliwa likisema kwamba mikutano ya ndani haijazuiwa ila kila chama kinatakiwa kufuata utaratibu ikiwamo kutoa taarifa kwa mujibu wa sheria.

Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles