23 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Ashatu: Tanzania ipo tayari kuzalisha bidhaa zake yenyewe

Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk.Ashatu Kijaji, amesema Tanzania ipo tayari kuzalisha bidhaa zake  yenyewe na zenye kiwango cha juu na kuweza kuhudumia Afrika na dunia.

Dk. Ashatu amebainisha hayo leo Januari 4, 2024 wakati alipofanya ziara katika kiwanda cha Multi Cable Limited (MCL) kinachozalisha vifaa vya umeme kilichopo Keko, jijini Dar es Salaam.

Amesema lengo la ziara hiyo ni kutaka kuona kinachozalishwa katika  viwanda  vya ndani,  mazingira ya watumishi wanaofanya kazi huko ili kuweza kuboresha na wataendelea kwa mwaka mzima.

Amesema kutokana na kile alichokiona katika kiwanda hicho na bidhaa zinazozalishwa  kuwa na nembo ya TBS ya Tanzania, ni muda wa wazalishaji wa ndani kuingia kwenye soko la  eneo huru la Afrika.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk.Ashatu Kijaji (katikati) akishika aina ya nyaya ya umeme inayozalishwa na kiwanda cha MCL.

“Niupongeze uongozi wa MCL kwa kazi wanayoifanya kwa Taifa letu, nimeona wanazalisha bidhaa mbalimbali na vifaa vya umeme na wapo kwenye miradi mbalimbali wakisambaza kwa Shirika letu la  Tanesco, lakini kwa ndugu zetu wa REA wanachukua nyaya za umeme kutoka hapa, hii inamaanisha kwamba  Taifa letu sasa tupo tayari kuzalisha bidhaa  za kwetu za kiwango cha juu,” amesema.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk.Ashatu Kijaji, akitazama sufuria zinazozalishwa na kiwanda cha MCL.

Ameeleza kuwa Tanzania ipo katika masoko ya kikanda, Afrika Mashariki na nchi za Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, pia soko la eneo huru la Afrika, hivyo ni kuhakikisha bidhaa zinafika katika masoko hayo.

“Leo hii nimewaelekeza wenye kiwanda hiki, tunapomaliza ziara hii, twende ofisini tukutane ili tuweze kuwaelekeza tunaingiaje kwenye Soko la Eneo Huru la Afrika,” amesema Dk. Ashatu.

Waziri Dk. Ashatu amesema mwaka 2023 walikaa ofisini lakini sasa ni muda wa utekelezaji na dhamira ya   Serikali ni kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa zinafika katika masoko hayo na wapo tayari kuwatafutia masoko wazalishaji.

“Tumeona watumishi zaidi ya 1000 ambao wapo kwenye viwanda hivi vinavyomilikwa na wenyeji wetu hawa MCL, hizi ni jitihada kubwa na zinaonyesha kwamba Serikali ya awamu ya Sita chini ya Dk. Samia Suluhu Hassan imeweza kutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya wawekezaji wetu wawekeze kwenye viwanda na kufanya biashara,” amefafanua Dk. Ashatu.

Aidha ameutaka uongozi wa kiwanda hicho kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji kazi na maslahi ya wafanyakazi wao.

Kwa upande wake Mwanasheria wa kampuni ya MCL, Kassmary Ahmed, amesema wanatengeneza vifaa vyote vya umeme ikiwamo transifoma, mita, nyaya za umeme tangu mwaka 2002.

Amesema wamefurahia ujio wa waziri wa viwanda kwani lengo lao ni kuongeza ajira kwa vijana na kuinua uchumi wa Taifa.

“Tunaungana na wizara katika kukuza, uboreshaji na kuongeza ubora wa bidhaa tunazozalisha. Kampuni hii pia inajihusisha na masuala ya kijamii,” amesema.

Amesema changamoto inayowakabili ni umeme kwani inawafanya washindwe kuwafikishia  wateja  wao bidhaa kwa wakati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles