28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

DCEA yawanoa maofisa Takukuru kupambana na dawa za kulevya

Na Mwandishi wetu, Dodoma

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imehitimisha mafunzo ya Maofisa  waelimishaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru} yaliyokuwa na lengo la kujengeana uwezo na kupeana mbinu za  uelimishaji umma katika mapambano dhidi ya rushwa na dawa za kulevya nchini .

Akizungumza jana Februari 22,2024 jijini Dodoma wakati wa kufunga mafunzo hayo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo, amesema tatizo la dawa za kulevya na vitendo vya rushwa ni tatizo mtambuka linalohitaji ushiriki wa pamoja katika kukabiliana nalo.

“Yapo mahusiano makubwa kati ya vitendo vya rushwa na biashara ya dawa za kulevya, kwani kwa kiasi kikubwa wafanyabiashara ya dawa za kulevya hutumia rushwa kufanikisha uhalifu wao. Hivyo, ili kuhakikisha tunapinga vitendo vya rushwa na dawa za kulevya, tumeona ni vema elimu juu ya rushwa na dawa za kulevya ikatolewa pamoja,” amesema Lyimo.

Ameongeza kuwa,  DCEA na Takukuru ziliingia makubaliano ya kutumia klabu za rushwa zilizopo shuleni na vyuoni kutoa elimu kuhusu rushwa na dawa za kulevya ili kuwafikia walengwa kwa urahisi na kutumia rasilimali chache za serikali hali itakayoleta tija zaidi katika kujenga uzalendo kwa vijana kuchukia vitendo vya rushwa na dawa za kulevya.

“Tumeshuhudia maafisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wakishirikiana kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya kijamii nchini hali ambayo itasaidia kuongeza uelewa juu ya athari za ya rushwa na matumizi na biashara ya dawa za kulevya,” amesema Lyimo.

Aidha, Kamishna Jenerali Lyimo ametoa wito kwa wadau wote kutambua kwamba elimu ni moja nyezo muhimu ya kukabiliana na changamoto ya dawa za kulevya na rushwa. hivyo, maafisa wa DCEA, maafisa wa Takukuru, wakuu wa shule na vyuo, walimu, walezi wa vilabu, vyombo vya habari, wasanii, vyombo vya ulinzi na usalama na wananchi wote washirikiane katika kupinga rushwa na dawa za kulevya.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Neema Makalyelye amesema matunda ya mafunzo hayo yataonekana katika utendaji kazi wa waelimishaji wetu mara watakaporejea katika vituo vyao vya kazi.

“Katika siku tatu za mafunzo washiriki waliweza kujifunza kuhusu tatizo la dawa za kulevya, makundi ya dawa za kulevya, sababu za matumizi, namna ya kumtambua mtumiaji wa dawa za kulevya, kuzitambua dawa tiba zenye asili ya kulevya, uraibu wa dawa za kulevya, magonjwa ambukizi, na tiba saidizi kwa kutumia dawa, namna ya kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na  uwepo wa huduma katika nyumba za upataji nafuu,” amesema Mwakalyelye.

Ameongeza kuwa, washiriki wamepitishwa katika andiko maalum la kampeni ya kutokomeza rushwa na dawa za kulevya katika shule na vyuo nchini, muongozo wa utoaji elimu kuhusu rushwa na dawa za kulevya shuleni na vyuoni, na kuelimishwa kuhusu uhusiano uliopo kati ya dawa za kulevya na rushwa ili waweze kutumia nyenzo hizo katika vituo vyao kufanya kazi.

“Ni matarajio yetu kuwa, mafunzo haya yataleta mabadiliko chanya katika utendaji kazi na hatimaye kuifanya jamii ya kitanzania kuichukia rushwa na dawa za kulevya kwani hivi vyote vina madhara kwa mtu, jamii na taifa kwa ujumla” ameongeza Mwakalyelye.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles