27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Msichana Initiative yatoa mafunzo

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Shirika lisilo la kiserikali la Msichana Initiative, limeiomba Serikali kuliunga mkono katika harakati za kumkomboa mtoto wa kike, kutambua haki zake na kupinga ukatili wa kijinsia.

Akizungumza leo Februari 23, 2024 jijini Dar es Salaam katika mafunzo yanayohusisha viongozi wasichana 20, Msimamizi wa Mradi wa Sauti Yetu, Nguvu Yetu, Rosemary Richard amesema mikoa minne inashiriki mafunzo hayo kwa lengo la kuwawezesha kubeba ajenda zao na kuzipigania.

Msimamizi wa Mradi wa Sauti Yetu Nguvu Yetu, Msichana Initiative, Rosemary Richard akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema mradi huo umelenga kutengeneza jukwaa la wasichana kwa kuwakutanisha na kutambua ajenda zao na kuimarisha nguvu ya pamoja.

“Lengo la kukutana na wasichana hawa ni kupeana mafunzo, na mikakati ya namna gani wasichana hawa wanapokwenda kutekeleza majukumu yao huku wakiwa wamebeba ajenda mbalimbali ikiwemo kupinga ndoa za utotoni, kuhamasisha usawa wa kijinsia sambamba na kuwawezesha ili waweze kuwa chachu ya uongozi,”amesema Rosemary.

Amesema mradi ni wa miaka miwili ambao umeanza mwaka 2023 na unatarajia kumalizika Oktoba, 2024.

Amesema Mradi wa Sauti Yetu, Nguvu Yetu, umewafikia viongozi wasichana 20 kutoka mikoa wa Pwani unaohusisha Wilaya ya Bagamoyo, Tabora Wilaya Nzega, Dodoma Wilaya ya Kongwa na Dar es Salaam.

“Kupitia viongozi hawa wasichana 20 kutoka katika mradi huu wameweza kuunda vikundi ambavyo vimefikia wasichana 240,”amesema.

Aidha amesema katika uendelevu wa mradi wamekuwa wakitoa mafunzo mbalimbali kwa wasichana hao huku wakijikita zaidi katika dhana nzima ya uwanaharakati pamoja na mambo ya uongozi.

Naye kiongozi wa msichana kutoka Bagamoyo, Leonardina Sosthenes amesema katika Mkoa wa Pwanj kumekuwa na wimbi kubwa la ndoa za utoto ambapo chanzo kikubwa ni tamaa za mali na kukosekana kwa elimu ya ukatili kwa watoto.

Amesema kupita shirika hilo wameweza kuokoa watoto watatu ambao waliingia kwenye ndoa na kufanikiwa kurudi shule.

“Suala la ndoa za utotoni limekuwa changamoto sana katika mkoa wetu tumeokoa watoto wa tatu ambao waliolewa wenye umri mdogo na tumewarudisha shule, kuna mmoja yeye alikuwa mjamzito tulimsaidia akafanya mitihani ya darasa la saba,amejifungua Desemba na sasa yupo kidato cha kwanza,”amesema Leonardina.

Naye,msichana kiongozi Ubungo, Dar es Salaam, Mwajuma Hima ametoa rai kwa wazazi kuwa karibu na watoto na kutokuwaamini ndugu na kuwaachia watoto kwani wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa ukatili kwa watoto.

Amesema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo vitendea kazi vya kuwatambulisha wanapokuwa wanakwenda kutoa elimu kwenye jamii .

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles