25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Biashara ya intaneti Tanzania – Burundi kuineemesha TTCL

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) linatarajia kuongeza mapato yake baada ya kuingia mkataba mwingine na Kampuni ya Mawasiliano ya Mkongo wa Taifa Burundi (BSS) kwa ajili ya kupeleka huduma ya intaneti nchini humo.

Mkataba huo ambao ni wa pili baada ya ule wa awali wa mwaka 2019 una thamani ya Sh bilioni 8.3 na utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano.

Akizungumza leo Februari 23,2024 baada ya kusaini mkataba huo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amesema utaboresha huduma za mawasiliano na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa nchi hizo.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, akizungumza wakati wa hafla ya kusaini mkataba baina ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Kampuni ya Mawasiliano ya Mkongo wa Taifa Burundi (BSS) kwa ajili ya kupeleka huduma ya intaneti nchini humo.

“Serikali imeonyesha dhamira ya kusimamia sekta ya mawasiliano kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji na kufungua fursa katika Ukanda wa Afrika Mashariki na SADC kutumia miundombinu yetu ya mawasiliano.

“Uamuzi huu wa Burundi una faida kwa nchi zetu hivyo tutaendelea kuwekeza katika teknolojia na kuongeza uwezo wa shirika kuendelea kutoa huduma,” amesema Nnauye.

Amesema pia Serikali imekusudia kuongeza uwezo wa mkongo kwa lengo la kuhakikisha wanapunguza gharama za matumizi na kuchochea maendeleo kwa nchi jirani na tayari wametenga fedha.

Amesema mkongo huo una uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko chanya kwa nchi, kuongeza fursa mpya za biashara na uwekezaji katika nyanja mbalimbali.

Waziri huyo ameiomba Burundi kutumia kituo cha kuhifadhi data kimtandao kilichopo nchini kwani ni salama, kina ubora na kinatumia teknolojia za kisasa.

Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga, amesema wanabadilisha sura ya Mkongo wa Taifa kuhakikisha unakuwa wa kikanda zaidi na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi kwa nchi.

“TTCL inaendelea kusimamia na kuendeleza miundiombinu ili iweze kutoa huduma Tanzania na nchi jirani, mazungumzo yanakamilishwa ili mkongo uweze kuunganishwa Mombasa,” amesema Mhandisi Ulanga.

Mkurugenzi huyo amesema kabla ya Oktoba mwaka huu watakuwa wamefika kwenye halmashauri zote za Tanzania Bara na Visiwani

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles