24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

DC Mbinga awakumbusha Wafanyabiashara kulipa kodi kwa wakati

Na Mwandishi Wetu, Mbinga

Wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wamekumbushwa kulipa kodi kwa wakati kwasababu kodi hiyo hurudi kwao kupitia miundombinu na miradi mbalimbali ya maendeleo.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Aziza Mangosongo wakati akizungumza na timu ya maofisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Dar es Salaam walipowasili wilayani humo kwa ajili ya kufanya kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango.

Aziza amesema kuwa, kodi hulipwa na watu wote wakiwemo watumishi wa serikali na wa sekta binafsi, wakulima, wafugaji, wavuvi pamoja na wafanyabishara, tofauti ni kwamba, kodi inayolipwa na watumishi hukatwa moja kwa moja kupitia mishahara yao.

“Napenda kuchukua fursa hii kuwahamasisha na kuwakumbusha wafanyabiashara na wananchi wote kulipa kodi kwa wakati ili kuinua uchumi wa nchi yetu na tuondoe ile kasumba ya kusema kwamba watumishi wa serikali hawalipi kodi, watumishi tunakatwa kodi moja kwa moja kupitia mishahara yetu,” amesema Mangosongo.

Aidha, Aziza amewataka wananchi kuwafichua watu wanaokwepa kulipa kodi kwa kutoa taarifa sahihi za wahusika hao katika maeneo mbalimbali ili washughulikiwe.

“Pia, nawaomba tusisite kuwataja watu wote wanaokwepa kulipa kodi na tujitahidi kutoa taarifa sahihi za wakwepa kodi katika maeneo yetu kwa maana kodi ni afya na ni uhai wetu,” amesema Aziza.

Naye, Meneja wa Huduma kwa Mlipakodi kutoka TRA Makao Makuu Honester Ndunguru amesema kuwa TRA imejipanga kuhakikisha inawafikia idadi kubwa ya wafanyabiashara nchini kwa ajili ya kuwaelimisha kuhusu haki na wajibu wao katika suala zima la ulipaji kodi.

“Sisi kama TRA, tumejipanga kufika maeneo mbalimbali kuhakikisha tunawaelimisha walipakodi wetu kujua haki na wajibu wao na leo tumekuja hapa Mbinga kwa lengo hilohilo la kuhakikisha tunawafikishia elimu ya kodi wafanyabiashara wa wilaya hii,” amesema Ndunguru.

Timu ya maofisa wanaofanya kampeni ya elimu kwa mlipakodi mkoani Ruvuma wako wilayani Mbinga wakiendelea kutoa elimu ya kodi na baada ya wilaya hiyo wataelekea Wilaya za Nyasa, Namtumbo na Tunduru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles