24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

DALADALA YAGONGA TRENI, MTU MMOJA AFARIKI DUNIA

TUNU NASSOR Na HAPPY MOYO (RCT)-DAR ES SALAAM

MTU mmoja amefariki dunia na wengine 23 wamejeruhiwa baada ya daladala la Eicher   walilokuwa wamepanda kutoka Gongo la Mboto kwenda Mnazi Mmoja kuigonga treni ya abiria katika eneo la Gerezani Kariakoo  Dar es Salaam jana.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Atilio Peter, alisema ajali hiyo ilitokea alfajiri wakati basi hilo   lilipoigonga treni lilipokuwa likijaribu kuvuka reli huku treni ikiwa imekaribia.

Kamanda wa Kikosi cha Reli, Simon Chillery,   alisema ajali  ilitokea saa 10:45 alfajiri katika makutano ya barabara ya Nkurumah na reli ya kati Kariakoo wakati treni hiyo ikitoka Stesheni kwenda Pugu.

Alisema daladala hilo liliiigonga treni inayojulikana kama treni ya ‘Mwakyembe’ iliyokuwa ikielekea Pugu kubeba abiria katika safari zake za mjini.

“Mtu mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 35 amefariki dunia na wengine 23 wamejeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea alfajiri ya leo (jana),” alisema Chillery.

Awali, akizungumza na MTANZANIA, Meneja Mawasiliano kwa Umma wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), Midladjy Maez, alisema majeruhi 16 walipelekwa katika Hospitali ya Taifa   Muhimbili na wawili kati yao walikuwa na hali mabaya baada ya kupata majeraha kichwani.

  Maezi alisema baada ya ajali hiyo treni iliendelea na safari kuelekea Pugu kuendelea kutoa huduma kama kawaida," alisema Maez.

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH) ilikiri kupokea mwili wa mtu mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Clavery (35) mkazi wa Kitunda Wilaya ya Ilala   pamoja na majeruhi 19.

Ofisa Uhusiano wa MNH, Neema Mwangomo, alisema kati ya majeruhi hao, saba walipelekwa katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) na mmoja alilazwa katika wodi ya Kibasila.

“Watano wameruhusiwa baada ya kufanyiwa uchunguzi na wengine bado wanafanyiwa vipimo na matibabu,” alisema Neema.

Aliwataja majeruhi waliopelekwa MOI kuwa ni Joshua Mlaga (22), Emmanuel Ngowi (25), Bakari Salim (38), Sophia Nassor (46), Magreth Mugata (48), Maya Yakoub na mwingine ambaye hakufahamika jina lake.

“Katika orodha hiyo,  yumo Makame Ally (40), Elizabeth Balagida (28), Mohamedi Likwata (54), Hamisi Mbwana (39), Leonard Legembo (39), Islam S. Islam (30), Yusta Mgan (44), Gilberth Ernest (32), Fadhira Ramadhan (27), Mwajuma Makunganya (46) Lydia Maduka (29) na James Kibaha(55),” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles