23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 21, 2022

Daktari aeleza wanafunzi shule za msingi wanavyotumia dawa za uzazi kukwepa mimba

RAMADHAN HASSAN -CHAMWINO

BAADHI ya wazazi wa wanafunzi wa kike wenye umri wa kuanzia miaka 14 wanaosoma katika shule za msingi na sekondari, wamekuwa wakilazimisha watoto wao  kutumia njia za uzazi wa mpango ikiwemo vidonge, vitanzi na vipandikizi ili wasipate ujauzito wakiwa shuleni.

Hayo yalielezwa jana na  Mganga wa Kituo cha afya Mpwayungu, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Ambaliche Boniface, wakati kikao kazi cha kupanga mikakati kwenye mradi kutokomeza ukatili kwa kupunguza mimba na ndoa za utotoni.

Mradhi huo unatekelezwa na shirika lisilokuwa la Kiserikali la Women Wake Up (WOWAP) kwa ufadhili wa The Foundation For Civil Society.

Boniface  alisema  baadhi ya wazazi wamekuwa wakifika kituo cha afya kuomba watoto wao watumie uzazi wa mpango kama njia ya kuwakinga wasipate mimba wakiwa shuleni.

“Mzazi anaona ni bora ampe mtoto wake vidonge vya kupanga uzazi, au awekewe kipandikizi au kitanzi, anaona heri mtoto apate maradhi mengine kuliko mimba,” alisema

Alisema njia hiyo si salama kwani mtoto anapowekewa njia za kumkinga asipate ujauzito, atazidi kufanya ngono zaidi kwani atajihakikishia yuko huru zaidi.

“Wazazi hawatimizi wajibu wao, hawakai kwenye nafasi zao anaona ni  heri mtoto afuate uzazi wa mpango, kama ngono afanye tu ili mradi asipate mimba akafukuzwa shule,” alisema.

Alisema watoto wanaofikishwa kituoni hapo ni  wale wenye umri wa kuanzia miaka 14 na kuendelea lakini kituo hicho hakitoa huduma ya kuwafunga watoto uzazi au kutoa vidonge vya uzazi wa mpango.

Alisema sasa hivi wanashauriana na viongozi wa vijiji  ili watoe elimu katika shule za msingi na sekondari ili kuondoa dhana hiyo ambayo imekuwa imeshamiri katika maeneo mengi.

“Sio vizuri mtoto wa miaka 14 au 16 kuanza kutumia njia za uzazi wa mpango anaweza kupata athari za kiafya hapo baadaye,” alisema.

Mratibu wa dawati la  mtoto kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Sophia Swai alisema  changamoto hiyo wanaipata watumishi wa kada ya afya waliopo kwenye  vituo vya afya na zahanati.

Alisema kutokana na zahanati na vituo vya afya vya serikali kutotoa huduma kwa wanafunzi wanaohitaji huduma, lakini wanaweza kupata huduma kwenye baadhi za zahanati na hospitali zinazokiuka maadili.

Katekista wa Kanisa la Anglikana Kata ya Mpwayungu, Grace Omari alisema  wazazi wanaogopa mimba kuliko tatizo zima la ngono zembe ndio maana wanashauri watoto wao kutumia kipandikizi, kitanzi na vidonge vya uzazi wa mpango.

Mkazi wa Mpwayungu Janeth Ndahani alisema  baadhi ya wazazi wamekuwa hawaoni umuhimu wa elimu na hivyo kushindwa kuhamasisha watoto wafanye vizuri darasani ili wakifeli wakaolewe.

“Mtoto ananunuliwa kioo, wanja, rangi ya mdomo, nguo mpya na vingine na anaambiwa usipofaulu nitakununulia vingi zaidi ya hivyo? Kwenye mazingira kama hayo mtoto ataona umuhimu wa shule?alihoji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
191,642FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles