26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 29, 2023

Contact us: [email protected]

Ummy achambua miaka mitano ya mafanikio katika sekta ya afya

RAMADHAN HASSAN -DODOMA

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amechambua mafanikio yaliyopatika ndani ya miaka mitano kwenye sekta ya afya ikiwa ni pamoja na eneo la afya ya uzazi na mtoto ambapo vituo vya huduma za upasuaji wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni vimeongezeka kutoka 192 hadi 586.

Alisema pia kumekuwa na ongezeko la bajeti ya dawa katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wazee ambalo limeongeza upatikanaji dawa muhimu kwa ajili ya afya ya uzazi na mtoto kutoka asilimia 53 mwaka 2015 hadi asilimia 96 Juni mwaka 2020.

Ummy alitoa kauli hiyo jana jijini hapa wakati akitoa taarifa ya afya ya uzazi na mtoto nchini kuanzia mwaka 2015-2020.

Alisema katika kipindi hicho Tanzania imeendelea kupiga hatua katika utoaji wa huduma za afya hususan afya ya uzazi na mtoto.

Alisema uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya wamu ya tano kwenye miundombinu ya utoaji wa huduma za afya umeongeza vituo vya huduma  za afya ngazi ya msingi vinavyotoa huduma za upasuaji  wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni vimeongezeka kutoka 192 hadi 586 sawa na ongezeko la vituo 394.

Vilevile, Serikali imeongeza idadi ya vituo vya huduma kwa ajili ya watoto wachanga  wanaozaliwa wakiwa na shida ya kupumua, uzito pungufu, na maambukizi ya bakteria  kutoka vituo 14 mwaka 2015 hadi vituo 104 mwaka 2020  sawa na ongezeko la vituo 90.

“Vituo vinavyotoa huduma ya Kangaroo ikiwa ni njia  ya kiasili ya kumtunza mtoto aliyezaliwa njiti vimeongezeka kutoka 80 mwaka 2015 hadi kufikia 104 mwaka 2020,”alisema Waziri Ummy.

Ummy alisema katika kipindi cha miaka mitano Serikali imeweza kufanya upanuzi wa Hospitali 3 za rufaa za Kanda, Hospitali ya Mtwara, Burigi ambayo ni ujenzi mpya  na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambapo jengo kubwa la ghorofa tano lenye uwezo wa vitanda 223 maalum kwa ajili  za huduma za mama na mtoto.

Alisema Serikali imeongeza vituo vya upimaji wa saratani ya mlango wa kizazi kutoka vituo 176 mwaka 2015 hadi kufikia 650 mwaka 2020 ambapo ni sawa na ongezeko la vituo 474.

Vilevile, alisema Serikali imeendelea kuimarisha vituo saba vya kanda ya damu salama na kuongeza vituo 14 vya damu salama  ambapo vituo vitano ujenzi wake unakamilishwa.

“Hii ni pamoja na kujengea uwezo timu za Halmashauri 184 katika ukusanyaji wa damu  kwa ajili ya kukoa maisha ya mama na mtoto pamoja na wagonjwa wengine,”alisema Ummy.

 Alisema upatikanaji wa damu salama kwa ajili ya kina mama na watoto  umeongezeka kutoka chupa 196,735 mwaka 2015 hadi chupa 309,396 mwaka 2020 sawa  na ongezeko la asilimia 57.

Ummy alisema kipindi cha mwaka 2016   watoa huduma za afya 14,479 wenye ujuzi waliajiriwa na kufikia watumishi 100,631 mwaka 2020 ikilinganishwa na watumishi 86,152 mwaka 2015.

“Watumishi hawa ni pamoja na madaktari, wauguzi, wafamasia, wataalamu wa maabara, watumishi hawa walipelekwa katika vituo mbalimbali vya utoaji huduma  nchi nzima kulingana na mahitaji ya kila Mkoa na Wilaya na kuweza kuimarika kwa utoaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto,”alisema Ummy.

Alisema Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, vifaa na vitendanishi kwa ajili ya huduma za afya nchini ambapo kumekuwa na ongezeko la bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015 hadi kufikia Sh bilioni 270 mwaka 2020.

Alisema ongezeko hilo limewezesha kuimarika kwa hali ya upatikanaji wa dawa  muhimu kwa ajili ya afya ya uzazi na mtoto kutoka asilimia 53 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 96 Juni mwaka 2020.

“Dawa hizo ni pamoja nay a kuzuia kuvuja damu baada ya kujifungua aina ya Oxytocin, dawa za kudhibiti  kifafa cha mimba zinzotolewa kwa njia ya sindano aina ya Magnesium sulphate,dawa za kuongeza  damu aina ya Febo na pia upatikanaji wa njia  za kisasa za uzazi wa mpango,”alisema Ummy.

Pia, alisema Serikali imeendelea kuboresha afya ya uzazi na mtoto kwa kununua magari kubebea wagonjwa 152 ambayo yamesambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya katika halmashauri mbalimbali nchini.

Ummy alisema katika kuimarisha uhifadhi na usambazaji wa chanjo Serikali imeendelea kutoa fedha za kununulia chanjo pamoja na ukarabati  wa mgahala ya kuhifadhi chanjo katika eneo la mabibo Jijini Dar es salaam.

“Pia ununuzi wa magari 74 ya kubebea chanjo, ununuzi wa majokofu 1,385 yanayotumia nguvu za jua ambapo magari hayo na majokofu yalisambazwa ngazi ya Halmashauri na taifa.

Vilevile, alisema kutokana na maboresho hayo idadi ya wanawake wanaotumia huduma za afya ya uzazi kabla ya ujauzito na baada ya kujifungua imeongezeka kutoka asilimia 32 mwaka 2015-2016 hadi asilimia 43 mwaka 2020.

Aidha, kuimarishwa kwa ubora wa huduma za kliniki kwa wajawazito na watoto kumeleta ongezeko  la kina mama wanaohudhuria mara nne ama zaidi kwenye kliniki ya wajawaziti kutoka akinamama 747,524 sawa na asilimia 39 mpaka kufikia akina mama zaidi ya milioni  1.7 sawa na asilimia 81 mwaka 2020.

Alisema kiwango cha kina mama waliojifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma kimeongezeka kutoka akina mama 1.226,603 sawa na asilimia 64 mwaka 2015 mpaka akinamama 1.801,603 sawa na asilimia 83 Juni mwaka 2020.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles