27.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 1, 2023

Contact us: [email protected]

Daktari aeleza ‘mateja’ walivyo hatarini kukumbwa homa ya ini

AVELINE KITOMARY -DAR ES SALAAM 

UTAFITI uliofanywa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Temeke, unaonesha asilimia 70 ya watumiaji wa dawa za kulevya – ‘mateja, wameathirika na homa ya ini (hepatitis C).

Akizungumza katika mahojiano maalum na MTANZANIA jana, bingwa wa magonjwa ya ini na mfumo wa chakula, Dk. Masolwa Ng’wanasayi, alisema hali hiyo inatokana na watumiaji hao kutumia sindano moja wakati wanapotumia dawa hizo kwa kujidunga.

“Homa ya ini ipo ya aina nyingi, kuna A na E ambayo inaambukizwa kwa njia ya chakula kichafu na kuna B, C na D zinaambukizwa kwa mfumo wa damu na virusi vya homa ya ini.

“Utafiti uliofanywa na Muhimbili na Temeke unaonesha asilimia 70 ya waathirika wa hepatitis C ni watumiaji wa dawa za kulevya, hasa wale wanaojidunga kwani huwa wanatumia sindano moja hali inayopelekea kuenea kwa virusi kutoka mtu mmoja hadi mwingine,” alisema.

 Dk. Ng’wanasayi alisema kuwa kwa sasa takwimu za Shirika la Utafiti wa Taifa inaonesha hali ya hepatitis C imefikia asilimia 2.

Alisema homa ya ini (hepatitis B) ndiyo inayoambukizwa kwa kiasi kikubwa, huku waathirika wakubwa ni wale waliopata wakiwa utotoni ambapo asilimia 23 wanaonesha dalili mwanzoni.

“Hepatitis B ndiyo unaongoza kwa kuathiri watu wengi ambapo waathirika wengi wanaanzia utoto na dalili za mwanzo zinaonekana asilimia 23 huku robo tatu wanaweza kuona dalili hata miaka 25 mpaka 30,” alieleza Dk. Ng’wanasayi.

Hata hivyo, Dk. Ng’wanasayi alisema kwa sasa Muhimbili inaendelea kujiandaa kufanya upandikizaji wa ini ambapo mpaka mwanzo mwa mwaka 2022 utakuwa umekamilika.

“Tunaendelea kufanya jitihada za kupandikiza ini ambapo wataalamu saba wameshapata mafunzo India, wengine tisa wako nchini China huku tukiendelea na mafunzo ya ndani.

“Kuna baadhi ya vifaa vimeshanunuliwa na vingine vya kupandikiza figo na uloto pia vitatumika katika kupandikiza ini,” alisema Dk. Ng’wanasayi. 

Alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kupima ugonjwa wa homa ya ini ili waweze kupata matibabu na chanjo kabla haujaleta madhara zaidi.

“Ugonjwa huo hauna dalili za moja kwa moja mfano homa, miguu kuvimba, uchovu, homa ya njano  na mengineyo,” alisema. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,406FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles