Daktari aeleza kilichokatisha uhai wa mbunge CCM

0
1484

Andrew Msechu -Dar es salaam

DAKTARI aliyesimamia uchunguzi wa kifo cha Mbunge wa Newala Vijijini, Rashid Akbar (CCM), amesema uchunguzi wa kitaalamu umebaini kuwa alifariki dunia kwa ugonjwa wa moyo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Dk. Nicolaus Mmuni ambaye mwili wa mbunge huyo ulipofikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi Sokoine, alikaimu nafasi ya daktari mfawidhi, alisema uchunguzi wa kitaalamu ulionyesha kwamba hakuna kitu chochote kilichomdhuru, bali lilikuwa ni tatizo la kiafya la kawaida.

Taarifa za kifo cha Akbar (59), akiwa mkoani Lindi zilitolewa juzi, na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Predunciana Protas pia alikiri kupokea taarifa hizo na kwamba atatoa taarifa rasmi baada ya uchunguzi kukamilika.

Mbunge huyo alizikwa rasmi jana, nyumbani kwake Newala Mjini mkoani Mtwara, katika maziko yaliyoongozwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa.

Dk. Mmuni alisema mwili wa mbunge huyo ulifikishwa hospitali na wataalamu walibaini kuwa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo na mara kadhaa alikuwa akipata huduma katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

“Katika huduma alizokuwa akizipata, pia aliwekewa kifaa maalumu cha umeme kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa moyo kijulikanacho kama ‘pace maker’ na wiki iliyopita inaonekana alikuwa akipata huduma Muhimbili, na inasemekana hali yake ilikuwa bado dhaifu.

“Hadi jana (juzi) alikuwa katika Kitongoji cha Mnazi Mmoja ambako anamiliki Hoteli ya Mingoyo Bay na hapo pia ana ofisi zake na ana mahala pa kupumzika.

“Inasemekana majira ya saa nne asubuhi mmoja wa wahudumu kwenye hoteli hiyo, ambako alikuwa akipumzika, alimpelekea chai, lakini alipofika aligonga mlango lakini haukufunguliwa.

“Alipata wasiwasi aliposikia kitu kama maji yanamwagika bafuni na ndipo alipowaita walinzi, ambao walitoa taarifa polisi na walivunja mlango ili kuona kulikoni.

“Walipoingia chumbani hawakukuta mtu, ila walipoangalia bafuni walimkuta akiwa amelala chali huku maji yakiendelea kummwagikia na yeye akiwa anakoroma.

“Ndipo walipochukua hatua ya kumchukua na kumwahisha hospitali na walipomleta kwetu ulifanyika utaratibu tu wa kuthibitisha baada ya kubaini kwamba tayari umauti ulishamfika,” alisema Dk. Mmuni.

Alisema uchunguzi wa kidaktari katika mwili wa marehemu ulibaini kuwapo kwa kifaa hicho cha umeme kwenye moyo na inaonekana hakuna kitu kilichomdhuru zaidi ya matatizo ya kawaida ya maradhi ya moyo yaliyokuwa yakimsumbua.

Dk. Mmuni alisema katika taarifa ya awali, polisi walithibitisha kuwa walikuta aina tofauti za dawa za moyo ambazo walizifikisha hospitali na madaktari walithibitisha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here