27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Dar yapata mwarobaini kukabili mafuriko

Mwandishi Wetu -Dar es salaam

WAKATI mafuriko yakiendelea kwa wakazi wa Dar es Salaam kila mvua inaponyesha, Serikali ya mkoa huo imesema mwarobani wa kukabiliana na tatizo hilo uko mbioni kukamilika, huku tayari ujenzi kwenye baadhi miundombinu ya madaraja ya mito mikubwa ukiendelea.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge alisema sababu za mafuriko kuwa kwa kiwango kikubwa zinasababishwa na wananchi wenyewe, lakini suluhisho sasa limepatikana na wako mbioni kuondoa adha hiyo.

Kunenge alisema sehemu ya utatuzi huo ni mradi mkubwa wa ujenzi na upanuzi wa mito mikubwa ya Msimbazi, Mto Ng’ombe na Mto Sinza utakaogharimu Sh bilioni 32 na tayari Sh bilioni 4.1 zimeshatolewa.

Alisema pamoja na miradi hiyo ya ujenzi, viongozi wa Serikali za mitaa na wananchi wanahimizwa kutoa ushirikiano kwa kuacha kutupa taka ovyo katika mifereji na mito hiyo, kwa kuwa ni sehemu ya chanzo cha mito na madaraja kuziba na kusababisha maji kukosa njia.

“Tunaendelea kushughulikia tatizo hilo, tunaendelea kujenga mito ya Kinondoni, Ilala na Temeke, kupitia mradi huo mkubwa. Hii ni hatua ya kwanza, lakini pia wananchi wanatakiwa kutoa ushirikiano kupitia Serikali zao za mitaa kuacha kutupa taka ambazo hubebwa na mvua na kuziba njia za maji,” alisema.

Kauli hiyo ya Kunenge imekuja baada ya mvua kubwa zilizonyesha Dar es Salaam kuanzia saa 10 alfajiri ya jana, ambazo zilikwamisha shughuli za wakazi wa jiji kwa muda wa karibu saa sita, baada ya barabara kadhaa kulazimika kufungwa kutokana na mafuriko.

Mvua hizo zilizosasababisha mafuriko katika maeneo yote yenye makutano ya barabara zinazopita mito ya Msimbazi, Tenge, Kigogo na Ng’ombe zilikuwa zikipitika kwa shida, huku baadhi, ikiwemo Barabara ya Morogoro eneo la Jangwani kufungwa kwa muda.

MTANZANIA lilishuhudia baadhi ya nyumba kwenye maeneo ya Bonde la Msimbazi, Bonde la Mkwajuni, Bonde la Kigogo na maeneo ya Kwa Mtogole maji yakiwa yamefunika baadhi ya nyumba na kuacha sehemu ya paa pekee, huku nyumba nyingine maji yakiwa kimo cha madirisha kutokana na wingi wa maji ya mafuriko katika maeneo hayo.

Mmoja wa wakazi wa eneo la Jangwani, jirani na daraja la Kigogo Sambusa, Bethuel Kaftani, alisema eneo hilo la makazi mbalo liko jirani na soko la Kigogo Sambusa, limekuwa likiathiriwa na mafuriko kila mvua zinaponyesha na sasa hawana la kufanya.

Alisema mara kadhaa wameiomba Serikali iwasaidie kwa kuimarisha miundombinu ya eneo hilo ili maji yapate njia maalumu ya kupita katika makazi yao, lakini hakuna hatua za wazi ambazo zimechukuliwa.

“Sasa tumeshachoka, lakini hatuna namna, tunaendelea kusubiri tu mvua zinyeshe, maji yajae, tukimbie makazi yetu kwa muda, maji yakipungua tunarudi, tunafanya usafi tunaendelea na maisha, basi, hatuna la kufanya, kwa sababu hatuna kwa kwenda,” alisema Kaftani.

Alisema wamekuwa wakisikia taarifa kutoka kwa Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda kuwa kuna mpango maalumu wa kuboresha miundombinu ikiwamo upanuzi na ujenzi wa Mto Msimbazi ambao ndio unaoelekeza maji yake katika eneo hilo la Jangwani, lakini hawajui umeishia wapi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles