24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Daktari aandika kitabu akianisha sababu nne za kansa

AVELINE  KITOMARY NA BRIGITHA MASAKI, DAR ES SALAAM

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk. Julius Mwaiselage amezindua kitabu kipya  ambacho pamoja na mambo mengine kimeainisha vyanzo vikuu vinne vya ugonjwa wa Saratani.

Mwandishi wa kitabu hicho ambaye ni Daktari Bingwa wa Saratani, Dk. Hellen Makwani amevitaja vyanzo  hivyo kuwa ni maambukizi, kutokuzingatia mtindo bora wa maisha,mionzi na urithi wa vinasaba katika familia.

Kwa mujibu wa mwandishi Chanzo cha maambukizi  husababishwa na virusi,bakteria na parasaiti,Chanzo cha mionzi husababishwa miale ya jua ambayo inaathiri ngozi na chanzo cha vinasaba husababishwa na kizazi au ukoo wenye vinasaba vya saratani ya matiti na utumbo.

Chanzo kingine kilichoainishwa ni ile ya aina ya mtindo wa maisha kama matumizi ya tumbaku na bidhaa zake ,kula vyakula ambavyo sio bora, kunywa pombe kupitiliza, matumizi ya dawa za kulevya na mengineyo.

Akizungumza katika uzinduzi huo jana Dar es Salaam Dk. Mwaiselage,alisema kitabu hicho chenye kurasa 92 kimeweza kuelezea aina 40 za saratani, kitasaidia jamii kuelewa kuhusu ugonjwa huo.

“Sisi kama taasisi tumehakikisha kuwa Dk. Hellen anapata ushirikiano wa kukamilisha kitabu hiki,lengo ni kuelimisha wananchi wa kawaida, kwa muda mrefu hivi vitabu vimekuwa vikitumiwa na wataalam wa afya tu lakini sasa kila mtu ana uwezo wa kupata  kusoma na kuelewa.

“Tunampongeza sana kama taasisi hiki ni kitabu cha kwanza kuandikwa kwa lugha ya kiswahili rahisi, nategemea kitafaa sana kwa watanzania kuelewa ugonjwa wa saratani,”alisema Dk. Mwaiselage.

Kwa mujibu wa Dk. Mwaiselage familia nyingi za kitanzania zimeathirika na ugonjwa wa saratani na kwa sasa kuna ongezeko la ugonjwa huo.

“Ongezeko la saratani ni kubwa na bado watu hawana uelewa wa kutosha kuhusu ugonjwa huo hivyo kitabu pia kinaelezea dalili za mwanzo za saratani.

“Mtu akijua dalili mapema akiwahi anaweza akatibiwa ila wengi wanakuja wakati saratani iko katika hatua ya tatu au nne hii imewagharimu watu wengi,wengine wanaamini kuwa saratani ni ushirikina,”alieleza Dk. Mwaiselage.

Kulingana na takwimu za kitabu hicho saratani inayongoza kuathiri wanaume ni saratani ya ngozi (Kaposi Sarcoma) kwa sailimia 20.3 na saratani inayoathiri zaidi wanawake ni ile ya mlango wa kizazi kwa asilimia 56.5.

Kwa upande wake Dk. Hellen alisema kitabu hicho kimefafanua kwa undani aina za saratani hivyo kitampa mwanga na wepesi wa msomaji kuelewa.

“Nimeainisha aina ya saratani na visababishi vyake, dalili, vipimo, matibabu na jinsi ya kuzui pia nimeandika angalizo kwa kila aina ya saratani hii itawapa wepesi kwa wasomaji kuelewa haraka,” alisema.

Hata hivyo Dk Hellen alisema kuwa kitabu hicho pia kitasaidia kulipia baadhi ya gharama kwa wale wagonjwa ambao wanauwezo mdogo kiuchumi.

“Nimechapisha nakala 500 , kinauzwa Sh 10,000 kwa kila kitabu Sh 2,000 itatolewa na kuwekwa katika akaunti maalumu ya Ocean road fedha hizo zitawasidia wale wagonjwa  ambao wanahitaji msaada kama nauli na vitu vingine,”alieleza Dk. Hellen.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles