24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

CUF yawapeleka mahakamani waliochoma bendera zake

OSCAR ASSENGA-TANGA

CHAMA cha Wananchi (CUF), Wilaya ya Tanga, kimefungua kesi mahakamani kwa ajili ya kuwachukulia hatua za kisheria waliokuwa wanachama wa chama hicho waliohamia Chama cha ACT- Wazalendo kwa madai ya kuchoma bendera na kadi za chama hicho.

Hayo yalibainishwa jana kwenye kikao maalumu kilichoshirikisha wanachama na madiwani wa chama hicho ambao walikuwa na ajenda ya kujadili mustakabali wao baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad, kuhamia ACT Wazalendo mapema wiki hii.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Naibu Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CUF Taifa, Masoud Mhina, alisema dhumuni la kikao hicho ni kujitathmini na kuchukua hatua kwa wale waliochoma bendera na kadi kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Mhina alisema kikao hicho cha kamati tendaji pia kimetoa tamko la kumtaka aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Mkoa wa Tanga, Rashidi Jumbe, kuhakikisha mali zote za CUF  alizokuwa anazishikilia anazirudisha kabla hatua kali hazijachukuliwa dhidi yake.

Alisema miongoni mwa mali za chama hicho zinazoshikiliwa na Jumbe ni pamoja na pikipiki tatu, spika, samani za ofisi na mafaili.

 “Tunaheshimu maamuzi yao ya kujiunga na chama mbadala, lakini kuhama kwao hakuhalalishi kuondoka na mali za chama chetu, mali zote za CUF zirejeshwe kwa mustakabali wa chama hicho,” alisema.

Mbali na hayo pia alizungumzia fununu zilizozagaa kuwa baadhi ya madiwani wa chama hicho wanaweza kufutwa uanachama na kupoteza sifa zao za udiwani na kusema jambo hilo halipo na wako huru na uamuzi wowote wa kwenda kwenye chama chochote.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Tanga Mjini, Mwambea Pashua, alisema hawatakuwa na kinyongo na mwanachama yeyote aliyehamia chama hicho na kuwahakikishia wananchi wa Tanga kuwa madiwani bado wapo na wanakitumikia chama chao.

Pashua alisema kwa mujibu wa taratibu za kidemokrasia, kila mwanachama ana hiari ya kuhamia chama chochote hivyo alisisitiza amani itawale zaidi ili kujenga vyama imara vya upinzani nchini.

Awali akizungumza katika mkutano huo, Diwani wa Kata ya Tangasisi, Mohamed Haniyu, alisema walichokuwa wanasubiri ni maamuzi ya mahakama katika kesi iliyokuwa ikimkabili Maalim Seif na Prof. Ibrahim Lipumba, hivyo baada ya uamuzi wa mahakama jukumu lililopo mbele yao ni kukijenga chama chao.

Haniyu ambaye pia ni Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, alisema madiwani wote 11 wa kuchaguliwa na watatu wa viti maalumu wapo na hakuna aliyeonyesha nia ya kuhamia chama chochote na wameazimia kukiimarisha chama hicho.

“Hatuna taarifa ya diwani yeyote kuhamia ACT Wazalendo, lakini suala la kuhama ni demokrasia kila mwanachama anao uhuru wa kuhamia chama atakacho bila ya kushinikizwa na kitu chochote,” alisema Haniyu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles