CUF kuanza mikutano ya hadhara nchi nzima

0
1052
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano wa CUF, Abdul Kambaya, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu maandalizi ya chama hicho kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Kulia ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Bunge na Sera, Mohammed Ngulangwa.

LEORNAD MANG’OHA Na AVELINE KITOMARY-DAR ES SAALAM

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimetangaza kuanza mikutano nchi nzima kwa lengo la kutoa elimu ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa CUF, Abdul Kambaya, alisema yapo matukio mengi na ya wazi ya vyama vya upinzani kuzuiwa na polisi kufanya mikutano kwa madai ya kuwapo zuio la Serikali.

Alisema Agosti 3, mwaka huu chama hicho kilipanga kufanya mkutano wa hadhara eneo la Vingunguti Relini, Manispaa ya Ilala na kuomba kibali cha polisi kwa barua yenye kumbukumbu namba CUF/W/IL/VOL.36/2019 ya Julai 29, lakini Jeshi la Polisi likapiga marufuku kwa maelezo kuwa kuna zuio la Serikali.

Kambaya alisema kwa muda mrefu vyama vya upinzani vimekuwa vikipiga kelele kuhusu zuio hilo alilodai kuwa linavunja katiba na sheria za nchi na kutaka viruhusiwe japo kufanya mikutano ya hadhara katika kipindi hiki cha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kuwahamasisha wananchi wajitokeze kujiandikisha jambo ambalo halijatekelezwa.

“Utekelezaji wa zuio la mikutano ya hadhara unasimamiwa na Jeshi la Polisi nchi nzima, jeshi ambalo linadai haijawahi kupata malalamiko. Hapa panatia shaka juu ya utendaji baina ya wizara na Jeshi la Polisi lililo chini yake,” alisema Kambaya.

Pia chama hicho kilimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, kuhakikisha yanapatikana mazingira ya usawa kipindi hiki cha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Aidha alisema chama hicho kinatarajia kuanza leo ziara zake za nchi nzima kama maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kueneza kaulimbiu yake ya haki sawa na furaha kwa wote.

Alisema ziara hizo zitakazoongozwa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, zitahusisha mikoa ya Tabora, Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Geita, Kagera, Mara na Kigoma, ambayo watafanya makongamano na shughuli nyingine.

“Pia Makamu Mwenyekiti Bara, Maftaha Nachuma, atafanya ziara katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi, hali kadhalika Naibu Katibu Mkuu atafanya ziara kama hiyo katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Manyara na Singida,” alisema Kambaya.

Katika hatua nyingine, CUF imeitaka  Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuondoa hitaji la namba ya simu kama moja ya kigezo cha mtu kujiandikisha katika Daftari la Wapigakura.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here