23.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

CHEGENI: MWANAFUNZI ATAKAYEFAULU KUPEWA 500,000/-

Na MWANDISHI WETU, BUSEGA


MBUNGE wa Busega Mkoa wa Simiyu, Dk. Raphael Chegeni, ametangaza mkakati wa kuchochea zaidi ukuaji wa sekta ya elimu jimboni humo kwa kutoa Sh  500,000 kwa kila mwanafunzi wa sekondari.

Alisema  fedha hizo atazikabidhi kwa mwanafunzi atakayepata daraja la kwanza  katika mitihani ya kidato cha nne, mwaka huu.

Dk. Chegeni alitoa kauli hiyo hivi karibuni alipozungumza wakati mahafali ya wanafunzi wa Kijeleshi Sekondari wilayani hapa.

Alisema ameamua kutoa ‘bingo’ hiyo ikiwa ni lengo lake la kumuunga mkono Rais John Magufuli katika kuboresha sekta ya elimu nchini.

“Serikali imekuwa ikitumia zaidi ya Sh bilioni 18 kutekeleza mpango wake wa elimu bure. Fedha hizi zinatolewa kila mwezi.

“Mbunge wenu natangaza kila mwanafunzi wa Kijeleshi Sekondari atakayepata daraja la kwanza, nitamzawadia Sh 500,000,” alisema Dk. Chegeni.

Mbunge huyo wa Busega alikwenda mbali zaidi na kusema: “Nawaombeni sana wananchi na wazazi tuwasaidie watoto wetu hasa wa kike kusoma ili waweze kufikia malengo yao.

“Naomba sana tuwapunguzie majukumu majumbani watoto wetu wa kike,” alisema Dk. Chegeni katika hafla hiyo.

Katika mahafali hayo, mbunge huyo kutoka CCM aligawa vitabu vya masomo yote vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni tano.

Alitumia fursa hiyo kutoa Sh milioni moja kwa ajili ya kuiwezesha shule hiyo ya Kijeleshi Sekondari kupata nishati ya umeme.

“Naomba sana wanafunzi msome kwa bidii, hasa masomo ya hesabu na sayansi,” alisema Dk. Chegeni na kuongeza:

“Nawashauri wananchi tuendelee kushirikiana na Serikali yetu iliyopo madarakani. Rais Magufuli amejitoa kuisaidia nchi.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles