31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema yaja na mwelekeo mpya

Na ELIZABETH HOMBO -DAR ES SALAAM

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimezindua sera mpya ya mwaka 2018, ambayo imejikita kuangalia uhuru wa watu, uchumi na huduma za jamii huku kikiishauri Serikali kuchukua wanayoona inaweza kuyatekeleza.

Sera ya kwanza ya chama hicho ilianza kutumika mwaka 1993, ikiwa ni miaka miwili kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995.

Safari hii chama hicho kimeiboresha tena sera yake hiyo ikiwa ni miaka miwili kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Akizindua sera hiyo Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema imejikita kwenye maeneo makuu matatu na kufafanuliwa katika maeneo 12.

Alisema wametumia mwaka mzima kufanya tafiti na kukusanya mawazo kutoka kwa watu mbalimbali wakiwamo wataalamu.

Pamoja na mambo mengine, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema sera hiyo itakuwa ikifanyiwa marekebisho kulingana na wakati.

Alisema eneo la kwanza la sera hiyo ni inayohusu uhuru wa watu, kwamba hata Mwalimu Julius Nyerere alipata kuzungumzia suala la maendeleo ya watu.

“Hili la maendeleo ya watu tumelifafanua vizuri kwenye sera zetu, kwa sababu watu wakiwa na maendeleo ‘automatically’ maendeleo ya vitu vitakuja vyenyewe, lakini ustawi wa watu ndio unaanza kwanza.

“Pia maeneo yanayotoa haki za msingi, je katiba inakidhi matamanio ya walio wengi? Kwenye utawala wa sheria, kuna mihimili mitatu je kila mhimili ni namna gani uko huru?” alihoji Mbowe.

Alitaja eneo la pili la sera hiyo kuwa ni lile linalolenga misingi ya uchumi.

“Katika eneo hili tumeainisha ni kwa namna gani wananchi wanapata huduma za kijamii, namna uchumi utakavyokuwa endelevu badala ya kuhodhiwa na Serikali.

“Huduma za jamii haziwezi kuwa endelevu kama kuna uchumi usiokuwa imara na si uchumi hodhi, bali ni ule unaoheshimu uwekezaji wa ndani nje ya nchi,” alisema.

Alitaja eneo jingine la sera hiyo kuwa ni linalolinda na kuihuisha jamii kupata huduma ya maji na barabara.

“Yasiwe mambo yanayofanywa na sekta binafsi bali yafanywe na Serikali. Haya mambo lazima yasimamiwe na Serikali kwa sababu sasa kumejengeka dhana kuwa Serikali ikijenga shule, zahanati, barabara inakuwa ni zawadi kutoka kwa Serikali au CCM, hii ni haki ya msingi ya wananchi na si msaada,” alisema.

Kutokana na hilo, Mbowe alisema anaikaribisha Serikali iliyoko madarakani kunakili sera zao kwa yale ambayo wataona yanawafaa, lakini wawe na ujasiri wa kukiri kuwa ni sera ya Chadema.

“Tunawakaribisha walio madarakani ‘wa-copy’ yale ambayo wataona yanawafaa, lakini wawe na ujasiri wa kutushukuru, wasione aibu kuja kwetu kwa sababu siku zote kitu cha kuchakachua unakuwa huipati vizuri, hivyo waje tutawasaidia,” alisema.

Pia aliwataka Watanzania, wanazuoni kuisoma sera yao hiyo mpya na kuichambua ili waweze kupata maoni yao.

 

SABABU ZA KUTOA SERA

Mbowe alisema wameamua kutoa sera ya namna hiyo kwa sababu hawaoni mafanikio ya watu kama taifa kwa sababu wananchi walisababishiwa umasikini wa kifikra.

Alisema uchumi wa kijamaa ulikuwa na tatizo kubwa, kwamba kiongozi mzuri ni yule ambaye ni masikini jambo ambao si sahihi.

Katika hilo alisema Chadema inaamini katika mafanikio ya mtu mmoja mmoja ambayo yanatengeneza mafaniko ya taifa kwa ujumla.

“Umasikini si sifa ni laana, huu ni ugonjwa mkubwa wa taifa letu… Eti kiongozi wa watu lazima awe masikini, sisi Chadema tunakataa, tunaamini kiongozi ni yule mwadilifu, mwaminifu.

“Lazima tujikite katika kunyanyua uwezo wa watu, tuwasukume kutafuta mali kukuza uchumi wa taifa zima,” alisema Mbowe.

 

  1. MASHINJI

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, alisema wametumia mwaka mmoja kufanya utafiti kuandaa sera hizo.

“Tulijiuliza maswali kadhaa kwamba; je tupo njia sahihi kama taifa? Uchumi wa taifa letu uko vizuri? Pia tukaangalia tuna vikwazo gani kama taifa.

“Pamoja na yote hayo sisi Chadema tunaamini haijalishi unatoka wapi, una rangi gani, kikubwa tunamwangalia mtu ambaye ana mchango kwa maendeleo ya Watanzania ndiyo maana hatuna shaka kabisa kuwa na uraia pacha,” alisema.

Dk. Mashinji alisema hakuna mkakati wowote ambao umeandaliwa na Serikali kuhusu viwanda.

 

SUMAYE

Akitoa neno la shukrani baada ya uzinduzi huo, mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho ambaye pia ni Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, aliipongeza sera hiyo akisema hata CCM haijapata kutoa sera ya aina hiyo.

Alisema wakati akiwa CCM pale wanapotoa sera inaishia kwenye Kamati Kuu ya chama, lakini haipati mawazo ya watu wengine kama ambavyo Chadema imefanya.

Akigusia baadhi ya maeneo ya sera hiyo, Sumaye alisema kama Serikali haijaweka sera na kama uchumi umeelemewa haiwezi kuzungumzia kuhusu viwanda.

“Huduma za jamii ni ‘product’ za uchumi, hujaweka sera na uchumi uko vibaya halafu unazungumzia viwanda, ndio vile inaishia mtu kusema kuwa cherehani nne eti ni viwanda,” alisema Sumaye.

Maeneo muhimu 12 ya misimamo ya kisera yaliyoanishwa na chama hicho ni pamoja na katiba, utawala, uchumi wa soko jamii, siasa za ndani, siasa kijamii, elimu na sayansi, afya, usimamizi wa ardhi, kilimo, miundombinu, mazingira na mambo ya nje.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa pia na mwakilishi kutoka ubalozi wa Marekani nchini, Nigeria, mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), wanaharakati na viongozi waandamizi wa chama hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles