23.8 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

Chadema wawaganda Pinda, Ghasia

 

tz

 

NA GRACE SHITUNDU, DAR ES SALAAM,
KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imetaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia, wajiuzulu kutokana na kasoro nyingi zilizojitokeza katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14 mwaka huu.
Shinikizo hilo lilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, wakati wakitoa taarifa ya maazimio ya Kikao Maalumu cha Kamati Kuu ya Chama hicho yaliyofikiwa juzi.
Dk. Slaa alisema licha ya kuwachukulia hatua baadhi ya wakurugenzi bado mawaziri Pinda na Ghasia wanatakiwa kuwajibika kutokana na kasoro zilizotokana na kanuni mbovu iliyotungwa na waziri mwenye dhamana.
“Kanuni iliyotumika haitungwi na Bunge bali inatengenezwa na waziri mwenye dhamana ambaye alitunga kanuni mbovu iliyosababisha demokrasia kupuuzwa.
Vitendo vya hila, hujuma, uzembe wa makusudi, mapingamizi, ukataji wa rufaa, kampeni na hatimaye upigaji kura vilijaa njama dhidi ya haki ya msingi ya kuchagua na kuchaguliwa, alisema Dk. Slaa.
Alisema toka mwaka 2004 wamekuwa wakisema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu haina uwezo wa kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuwa watendaji wake wengi wanatoka katika CCM
Dk. Slaa alisema pamoja na wananchi kujitokeza kutumia haki yao lakini kulikuwa na hujuma za wazi zilizofanyika ikiwa ni pamoja na kutokuwepo na masanduku vituoni, ukosefu au upungufu wa karatasi za kupigia kura na hakukua na usimamizi salama wa kura.
“Jamii yetu inaendelea kubaki nyuma kwa sababu tu uchaguzi ambao ndiyo fursa ya wananchi kutoa sauti na kupunguzia manung’uniko yao haiheshimiwi,” alisema Dk. Slaa.
Alisema haki hiyo ikiendelea kupuuzwa kama ambavyo inazidi kuoneshwa na watawala chini ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), itawafanya wananchi kupuuza uchaguzi na kuona hauna maana kabisa.
Aliongeza kuwa licha ya wananchi kujitokeza kupiga kura, wasimamizi kwa makusudi katika baadhi ya maeneo hwataki kutangaza matokeo au kuvuruga uchaguzi kwa sababu tu CCM imeshinda.
Alisema pamoja na hayo, Kamati kuu ilifikia maazimio mengine ambayo ni kuhakikisha kambi ya upinzani bungeni inapeleka muswada wa marekebisho ya sheria ya usimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili usimamiwe na Tume huru ya Uchaguzi.
“Suala la kupita bila kupingwa ni kinyume na demokrasia na haki ya msingi ya raia ya kuchagua, hivyo utamaduni huo ufe na kama ikitokea basi zipigwe kura za ndio na hapana,” alisema Slaa.
Aidha, katika hatua nyingine, Dk. Slaa alisema kuwa hadi sasa Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Uchaguzi haionekani kujipanga kuweza kufanikisha Uchaguzi Mkuu ujao.
Alisema tayari kasoro nyingi zimejitokeza katika zoezi la majaribio ya uandikishaji wapiga kura linaloendelea katika majimbo ya Kawe, Kilombero na Mlele.
Alisema mashine zile kutokana na mazingira zinaharibika hali inayoashiria matatizo makubwa zaidi wakati wa kuendelea na zoezi katika nchi nzima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,719FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles