Elizabeth Mjatta na Aziza Masoud,Dar es Salaam
KAULI ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka kwamba hatojiuzulu na kwamba yeye na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo bado wanategemewa na Rais Jakaya Kikwete imeonekana kutibua nyongo za wasomi, wanasiasa na watu wa kada mbalimbali.
Mbali na wasomi, wanasiasa na watu wa kada mbalimbali waliozungumza na gazeti hili, kuhusiana na kauli hiyo aliyoitoa juzi mbele ya waandishi wa habari akijisafisha baada ya jina lake kutajwa kwenye kashfa ya Escrow, lakini pia mijadala ya watu mbalimbali katika maeneo na kwenye mitandao ya kijamii imetoa taswira inayoonyesha kuwa kauli yake hiyo haiwezi kumsafisha machoni mwa jamii.
Akizungumzia kauli hiyo, Mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila ambaye pia ni muasisi wa hoja ya sakata hilo la Escrow ndani ya Bunge alisema kitendo cha Ikulu kukaa kimya ndiyo kinatoa mwanya kwa watuhumiwa kuendelea kujitetea.
“Hawa wanamtega Rais Kikwete kwasababu wanajua Ikulu inahusika na jambo hili, wanataka kuona Rais Kikwete atawafanya nini wakati jambo zima linaloendelea na yeye anafahamu kila kitu,”Alisema Kafulila.
Alisema Profesa Tibaijuka amekosa uadilifu na ndiyo maana anaendelea kung’ang’ania madaraka “Lakini ukiangalia kauli yake kwamba ikibainika zile fedha ni chafu atazirudisha ni kwamba anaona kabisa kuna tatizo, tayari ripoti ya CAG imeshaeleza kila kitu sasa anasubiri nini kuzirudisha,”alisema Kafulila.
Kafulila alisema kinachoonekana Profesa Tibaijuka anatumia mgongo wa Ikulu kujitetea kwa maelekezo ya Ikulu.
“ Ikulu yenyewe inataka kuwatetea hawa watu na ndiyo maana umeona hata taarifa ya CAG imechapishwa katika magazeti, lakini hawa watu siyo wasafi hata wajitetea vipi wanatakiwa kurudisha fedha za umma,”alisema Kafulila.
Kwa upande wake Mbunge wa Mwibala Kangi Lugola alisema kitendo cha Tibaijuka kusema hawezi kujiuzulu kwa sababu ni tegemeo kubwa la rais Jakaya Kikwete ni kuwatukana Watanzania na kutafuta huruma ya rais wakati akiwa katika harakati za kutimiza maazimio ya Bunge.
Mbunge huyo wa Chama Cha Mapinduzi ambaye kauli zake mara nyingi zimekuwa si za kukilinda chama kwa uovu, alisema Profesa Tibaijuka anajidanganya kwakuwa rais Kikwete hawezi kumtegemea mtu ambaye ana kashfa ya kuchukua fedha chafu ambazo zimetokana na kodi za wananchi.
“Tibaijuka aache kutapatapa niliposikia kauli yake jana(juzi) nilimfananisha na mtu aliyekunywa uji wa moto ukamchoma kwenye ulimi, akaupeleka kwenye tama la kushoto na kulia mwisho anajikuta anautema kwa sababu ulimi unakuwa umeungua.
Hawezi kusema nategemewa na rais Kikwete wakati fedha alizochota hana maelezo ya kuzitolea akaeleweka, ameongea hivyo ili aonewe huruma, rais hawezi kuwa na huruma na watu wanaokula fedha za wananchi,”alisema Lugola.
Alisema kuendelea kuilaumu Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwa haikumtendea haki kwakuwa haikumuhoji ni kutapatapa kwakuwa fedha hizo aliingiziwa katika akaunti yake binafsi na si katika akaunti ya shule kama alivyoelezea matumizi ya fedha hizo.
Alisema sakata la Escrow limemkamata pabaya Profesa Tibaijuka na kuendelea kujitetea ni kuwarubuni watanzania ili aonekane hana hatia wakati ameshiriki kuchukua fedha chafu.
Aliyekuwa Naibu Katibu mkuu CUF Bara, Julius Mtatiro alindika katika ukurasa wake wa Facebook kuwa kitendo cha Profesa Tibaijuka kusema hatajizuru kinaashiria kauli ya Rais Kikwete haitakuwa na uamuzi mgumu.
“Hata kama ulifeli magazijuto, huwezi kujua fomula hii, kwa wanaojua maana ya “pre-emption” watakubaliana nami kwamba taarifa ya Ikulu juu ya Mwanasheria mkuu kuachia ngazi, iliyokuwa imejaa bashasha na sifa kuu kwake ilikuwa na maana ya kuanza safari ya kulinda wezi wa fedha za umma.
“Tena, kujitokeza hadharani kwa waziri mmoja Kigogo (Tibaijuka), mnufaika wa fedha za Escrow na kueleza kuwa “hatathubutu kujiuzulu” jumlisha na ukimya wa waziri Muhongo.
Mtatiro aliendelea kuandika kuwa hotuba ya Rais Kikwete inayosubiriwa, haitakuwa na uamuzi wowote mgumu, atahutubia na kutetea wezi wake, atasema vyombo vyake viachwe vichunguze kwa uhuru na kwamba Bunge lisiiwekee serikali ‘bunduki kichwani’
Mhadhiri na mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk.Benson Bana alisema Profesa Tibaijuka anatakiwa kukomaa kisiasa kwani kuna wakati mwanasiasa inabidi awajibike hata kwa jambo asilolifanya.
“Nafikiri Profesa anatakiwa kusoma alama za nyakati, anatakiwa kuona kwamba jamii tayari imekwishawahukumu, lakini pia anatakiwa kufahamu kuwa wakati mwingine kama mwanasiasa unapaswa kuwajibika kwa ajili ya kujenga heshima yako,”alisema Dk.Bana.
Dk. Bana alisema hata ikitokea Rais ameacha kuwachukulia hatua jamii itaendelea kuwahukumu.
“Nimesoma mambo yote aliyojitetea nafikiri kauli yake ni ya kupaniki, hofu na iliyojaa uoga wa kuwajibika, sijaona athari chanya aliyoileta kwa jamii, bado hajaweza kuishawishi jamii,”alisema Dk. Bana.
Kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh Bilioni 306 katika akaunti ya Tegeta Escrow imeonekana kuitwika serikali ya Rais Jakaya Kikwete mzigo mkubwa hasa baada ya Bunge kutoa maazimio yanayomtaka awawajibishe mawaziri wawili ambao ni Tibaijuka na Muhongo
Mbali na mawaziri hao pia Bunge linamtaka Rais Kikwete awawajibishe watendaji wake wawili ambao ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ambaye tayari amejiuzulu akisema kuwa ushauri wake katika sakata hilo haukueleweka pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini.