24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema watunisha msuli

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeendelea na msimamo wake wa kufanya maandamo na migomo isiyo na mwisho kwa nchi nzima na leo kinatarajia kutoa ratiba yake.

Hayo yalibainishwa jana na Ofisa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene wakati akizungumza na MTANZANIA Jumapili pembezoni mwa mkutano wa vijana wa vyama vya siasa barani Afrika (DUA) uliokuwa ukifanyika katika Hoteli ya Giraffe jijini Dar es Salaam.

Makene alisema chama hicho kitatoa ratiba hiyo kwa waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho leo saa sita mchana.

Chadema imeendelea kusisitiza kwamba lengo lake la kufanya maandamano kushinikiza kusitishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba liko palepale, licha ya vitisho vinavyotolewa na Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali nchini.

Kauli kama hiyo pia ilitolewa jana na Mwenyekiti mpya wa Baraza la Vijana (Bavicha), Paschal Patrobas, ikiwa ni siku chache tu baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kuitwa na kuhojiwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutoa kauli ya uchochezi kutokana na kitendo chake cha kuhamasisha migomo na maandamano nchi nzima kupinga Bunge hilo.

Patrobas alisema kazi wanayofanya sasa ni kuratibu maandamano hayo yasiyokuwa na ukomo nchi nzima ili kuzuia kuendelea kwa uchakachuaji wa fedha unaoendelea kufanywa na Bunge hilo linaloongozwa na Mwenyekiti wake Samuel Sitta.

“Chadema hatutakuwa tayari kuona fedha za Watanzania masikini zikiliwa wakati Katiba inayotengenezwa imewabagua wanasiasa wa upinzani, hivyo hatutakuwa tayari kuona uchakachuaji huu unaendelea kutengeneza Katiba isiyokidhi ubora, huku tukitambua kuwa Katiba ndiyo sheria mama,” alisema.

Wakati akifungua mkutano huo wa vijana, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alitoa wito kwa Rais Jakaya Kikwete kusitisha Bunge Maalumu la Katiba ili kujiepusha na mashtaka ya mauaji kama yale yanayomkabili Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC).

Alisema kama akiendelea kuacha Bunge hilo halafu akapelekwa ICC, asije akawalaumu wapinzani kwamba ndio sababu ya kufikishwa huko kutokana na maandamano yatakayofanyika.

Mnyika alitoa wito kwa vijana kuendelea kuzungumzia matatizo ya Katiba za nchi hizo.

“Kenya pamoja na kuwa na Katiba nzuri, lakini imekuwa na tatizo katika utekelezaji wa sera ya majimbo, imekuwa ni changamoto kubwa” alisema Mnyika.

Wakati huo huo, kamata kamata inayoendeshwa na Jeshi la Polisi nchini dhidi ya wanachama na viongozi wa Chadema, imeonekana kuwarudisha nyuma viongozi wa chama hicho mkoani Mwanza.

Hadi sasa hakuna maandalizi yoyote yanayofanywa na viongozi wa Chadema kama walivyoagizwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Mbowe katika Mkutano Mkuu uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Kiongozi wa Operesheni Kanda ya Ziwa Magharibi, Njugu Tungaraza, alisema hadi sasa hakuna maandalizi yoyote ya kuandaa maandamano katika Mkoa wa Mwanza.

Tungaraza alisema licha ya Mkutano Mkuu kuagiza kuanza maandalizi ya kuandaa maandamano nchi nzima, lakini wanashangazwa na nguvu kubwa inayotumiwa na polisi kwa kuwakamata.

“Hapa Mwanza hatuna maandalizi ingawa tulipewa maagizo na Mbowe, hatujakaa kama viongozi kuona namna ya kuandaa maandamano hayo kwa sababu tunaona polisi wanatumia nguvu kutubana.

“Kwa kuwa tumepewa maagizo, tutayatekeleza baadaye, kama unavyoona maandamano yanaendelea kufanyika baadhi ya mikoa, tumeona wafuasi na viongozi wa Dar es Salaam, Dodoma na Morogoro, Pwani   wanakamatwa, lakini nikuhakikishie tutaandamana tu,” alisema.

Habari hii imeandaliwa na Shaban Matutu (Dar) na Benjamini Masese (Mwanza)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles