22.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Wazanzibari watishwa bungeni

Bunge
Bunge

NA WAANDISHI WETU, DODOMA

WAJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba waliotokana na kundi la 201, wameanza kupokea ujumbe wa vitisho.

Ujumbe huo ambao MTANZANIA Jumapili iliupata, umeanza kusambazwa jana asubuhi kwa simu za mkononi na unawalenga wajumbe wa kundi hilo wanaotoka Zanzibar.

Unawataka wajumbe hao wasishiriki katika hatua ya kupiga kura ya kupitisha Rasimu ya Katiba inayotarajia kuanza Septemba 2 hadi Oktoba 4.

Ujumbe huo ambao haujajulikana ulianzia wapi na umesambazwa na kundi gani, unawataka wajumbe hao kujiondoa mapema bungeni ili kukwamisha theluthi mbili inayotakiwa kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar kabla ya kupitisha sura za rasimu hiyo.

Kwa mujibu wa ujumbe huo, rasimu hiyo imeandaliwa na CCM kwa ajili ya kuiangamiza Zanzibar jambo ambalo Wazanzibari hawatakiwi kulikubali kwa namna yoyote ile.

Ujumbe huo ambao umebeba kichwa cha habari “SAA YA KUWAFICHUA WANAFIKI NA WASALITI WA ZANZIBAR KATIKA BUNGE LA KATIBA IMEFIKA” baadhi ya vipengele vinasomeka hivi:

“Wazanzibari tunatambua kwamba, shoka halifanyi kazi bila ya mpini. Hivi sasa mipini ipo Dodoma inajiandaa na nukta ya mwisho ya kuimaliza Zanzibar ambayo ni upigaji kura ili kuipitisha rasimu ya CCM ya kuiangamiza Zanzibar.

“Wazanzibari hatuko tayari kupoteza nchi yetu na vizazi vyetu kwa maslahi ya wanafiki wachache walioamua kwa njaa zao kufakamia mamilioni ya fedha kwa thamani ya kuiangamiza nchi yetu tukufu.

“Sote tunafahamu kwamba theluthi mbili (2/3) ya Zanzibar haipo ndani ya Bunge la Katiba kama kundi hili la 201 kutoka Zanzibar lisingeshiriki kutopiga kura.

“Hivi sasa tunatambua Bunge hilo la Intarahamwe linafanya juu chini kukamilisha umafya wao ili wapige kura kuhalalisha haramu yao.

“Sisi Wazanzibari, kamwe hatulii na wajumbe wa CCM kwa kuwa wao walishatangaza wazi vita vya kuiangamiza Zanzibar hadharani, ila linalotusikitisha ni sehemu ya hili kundi la wajumbe 201 kutoka Zanzibar ambayo wajumbe wake kwa nje (kinafiki) wanaonyesha kuunga mkono madai ya Wazanzibari, lakini kwa ndani wanaonekana kumbe na wao ni mipini, wanalitumikia shoka kuimaliza Zanzibar.

“Hivyo basi, tunawaambia wazi wajumbe hao wa kundi la 201, watoke katika Bunge la Katiba mara moja kabla ya upigaji kura, vinginevyo hatuwaelewi. Hatuhitaji wapige kura ya siri wala ya wazi. Tunachohitaji ni theluthi mbili (2/3) ya Zanzibar isipatikane kabla ya hata huo upigaji kura wenyewe.

“Na kama hawakutoka, tunawataka Wazanzibari wawatambue wasaliti hawa, wawalaani kwa nguvu zote na wawaorodheshe katika daftari na wasaliti wa Zanzibar kama wenzao akina Balozi Seif Ali Iddi.

“Tafadhali eneza taarifa hii kwa Wazanzibari wote walio ndani na nje ya nchi.”

Mmoja wa wajumbe wa Bunge hilo ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema hakuwa na taarifa za ujumbe huo.

Hata hivyo, Katibu wa Bunge hilo, Yahaya Hamis Hamad, alipozungumza na MTANZANIA Jumapili kwa simu, alisema alikuwa hajauona ujumbe huo ingawa ameshapigiwa simu na baadhi ya waandishi wa habari wakitaka kujua ukweli kuhusu ujumbe huo.

“Sijaupata ujumbe huo ila wewe ni mwandishi wa habari wa pili au wa tatu kuniuliza juu ya ujumbe huo.

“Lakini, nashukuru kwa kuniuliza, ngoja na sisi tuufuatilie tujue umeanzia wapi,” alisema Hamad.

Kitendo cha Bunge Maalumu la Katiba kuendelea na vikao vyake mjini hapa, huku upande wa wajumbe wanaotoka katika vyama vya upinzani wakiwa wamesusia vikao vyake, kimekuwa kikipingwa na watu mbalimbali ambao wamekuwa wakihoji uhalali wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles