22.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Chada Boy: Gigy Money, Amber Lulu walitaka kuniharibia shoo

JUMA3TATA RIPOTA

MIONGONI mwa wasanii wanaokuja kwa kasi kwenye ulimwengu wa Bongo Fleva ni Joseph Januari maarufu kama Chada Boy, ambaye mbali na kufanya muziki amekuwa akifanya matukio kadha wa kadha ya burudani.

Mwishoni mwa wiki Chada Boy, amefanikiwa kufanya mahojiano na ripota wa Juma3tata ili mashabiki waweze kufahamu mengi kuhusu muziki na maisha yake ya kawaida, karibu.

Juma3tata: Kuna dili ulipata la kwenda kufanya shoo Nigeria, je kwanini hukwenda?

Chada Boy: Mimi ndiyo nilikuwa msanii pekee wa Tanzania kuchaguliwa kutumbuiza kwenye tamasha la Eko huko Nigeria lakini katika kipindi kile ndiyo tukawa na misiba ya Ruge Mutahaba na Ephraim Kibonde, sikuona umuhimu wa kwenda huko wakati Tanzania nzima inaomboleza.

Juma3tata: Unadhani kwanini ulipata dili hilo wakati Tanzania ina wasanii wengi?

Chada Boy: Kwasababu wimbo wangu Waue umekuwa ukichezwa sana huko Ghana na Nigeria ndiyo maana waandaaji wa hilo tamasha wakaaamua kunipa nafasi nitumbuize.

Juma3tata: Mbali na muziki unafanya shughuli gani nyingine?

Chada Boy: Mimi ni kinyozi maarufu sana hapa Sinza, Dar es Salaam huwa nawanyoa nywele mastaa mbalimbali na watu wa kawaida.

Juma3tata: Mastaa gani umewahi kuwanyoa?

Chada Boy: Wapo wengi sana zaidi ni Diamond Platnumz toka kipindi hicho akiwa na Q Boy ambaye ndiyo alikuwa anasimamia mwonekano wake pamoja na wasanii wengine wengi.

Juma3tata: Unaweza vipi kufanya kazi yako ya kunyoa na muziki kwa ufasaha?

Chada Boy: Kunyoa siwezi kuacha kwa sababu ni fani iliyonitoa mbali sana hata niwe staa mkubwa nitaendelea, kikubwa ni kupanga muda wa kunyoa na muda wa kufanya kazi za muziki ambazo mara nyingi ni usiku.

Juma3tata: Uhusiano wako na mastaa wa Bongo Fleva upo vipi?

Chada Boy: Upo vizuri sana, hakuna msanii ambaye hanifahamu iwe kwenye muziki au filamu maana nimekuwa nikiandaa maonyesho mbalimbali hapa Dar es Salaam.

Juma3tata: Unapitia changamoto zipi katika kuandaa maonyesho yako?

Chada Boy: Changamoto zipo nyingi sana hasa wasanii kunizingua, mfano niliwahi kuandaa shoo nikawaalika Gigy Money na Amber Lulu kwa sababu ni marafiki zangu tukakubaliana watakuja bure kunisapoti.

Waliposikia shoo itakuwa kubwa, Amber Lulu akaniambia bila 500,000 haji na Gigy Money naye bila 400,000 haji kwenye shoo na muda wa onyesho ulikuwa umekaribia ikabidi nitumie akili nyingi kwa kumleta Jike Shupa ambaye alifanya kitu kizuri sana.

Juma3tata: Mwezi uliopita uliingia kwenye ugomvi wa Nuh Mziwanda sababu ikitajwa kuchepuka na mpenzi wake, ukweli ni upi?

Chada Boy: Hapana, mimi sijaoa kwa hiyo nina wasichana wengi ila sijawahi kutoka na msichana wa mtu.

Juma3tata: Umewaandalia nini mashabiki zako?

Chada Boy: Kikubwa bado nahitaji sapoti yao, hivi karibuni nimeachia video ya wimbo wangu mpya Msambwanda ambayo ipo YouTube.

Juma3tata: Asante kwa muda wako.

Chada Boy: Shukrani pia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,415FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles