23.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 22, 2023

Contact us: [email protected]

CCM yasisitiza wagombea sahihi 2024/25

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam kimezitaka jumuiya zake kukisaidia chama kupata wagombea sahihi wanaokubalika na wananchi kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Viongozi wa Jumuiya na Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Ilala wakiwa kwenye mafunzo ya kiitikadi kuwaandaa kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Akizungumza Agosti 26, 2023 wakati wa mafunzo ya kiitikadi kwa viongozi wa jumuiya na Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Ilala, Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Banangwa, amesema wanawajengea uwezo waweze kutambua mahitaji ya chama kuelekea 2024/25.

“Tunahitaji kuwa na wagombea sahihi, wagombea safi, wanaokubalika na wanaowachagua. Hatutapendekeza mtu kwa sababu ni ndugu yetu, au kwa sababu ni mwanamke, kijana, mzee, hapana.

“Mtu mla rushwa, mzinifu tena hadharani, mchonganishi, chama chetu hakina upungufu wa watu na hatukuchagui kwa sababu umesoma sana, tunamchagua ambaye watu wa mtaa wake wanasema anawafaa na ikiwa hivyo kazi ya CCM itakuwa nyepesi…nendeni mkatusaidie kupata wagombea sahihi,” amesema Banangwa.

Aidha amesema madiwani wa chama hicho watapimwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuhakikisha chama kinashinda katika mitaa yao.

“Madiwani sababu za ninyi kuendelea 2025 ni uchaguzi wa mwaka kesho (2024), lazima uhakikishe una wenyeviti wa Serikali za Mitaa ili uwe na uhakika wa kuendelea kuwa diwani, lakini nendeni mkahimize watu bora wa kugombea Serikali za Mitaa msifikiri wanakuja kuwa madiwani,” amesema.

Akiwasilisha mada kuhusu majukumu na wajibu wa viongozi wa chama na jumuiya zake, Mushi kutoka Dawati la Mafunzo CCM Makao Makuu, amesema viongozi wa chama hicho wanatakiwa wawe mfano kwenye jamii.

“Hatutegemei kiongozi wa CCM anyoshewe kidole, anatakiwa awe dira, taa, muongoza njia, awe msaada wenye kutoa majibu sahihi kwenye jamii,” amesema Mushi.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Sidde, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo kuelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mita 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025.

“Mafunzo kama haya yatafikishwa ngazi ya matawi, mashina na kwa wanachama wote kisha tutaanza program maalumu kwenye kata na matawi ili kutimiza ahadi ya mwana – CCM kwa mujibu wa katiba kifungu cha sita,” amesema Sidde.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles