27.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Cannavaro, Oscar si dhambi kutundika daluga

Nadir Haroub ‘Cannavaro’NA ZAINAB IDDY

LICHA ya Wanayanga kuikatia tamaa timu yao katika harakati zake za kutinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika. Binafsi nalipongezi benchi la ufundi chini ya Hans van de Pluijm na wachezaji kwa hatua waliyofika.

Ninaamini vipigo na changamoto kwa ujumla walivyokutana navyo kwenye mashindano ya kimataifa, vimeweza kuwapa funzo ili kufanya vizuri mwakani.

Kazi kubwa wameifanya kuingia hatua ya makundi baada ya kutolewa klabu bingwa, nina imani Pluijm ni mwelewa na analijua vilivyo soka la Afrika hivyo mwakani hatakuwa tayari kuona makosa yaliyojitokeza yakijirudia.

Nikiachana na hayo, kuna kauli inayozungumzwa sana kwamba ‘kujiuzulu ni moja ya njia za kuonyesha uzalendo wa kweli’ na mimi nasema si dhambi kwenu Oscar Joshua na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kutungika daluga.

Wanayanga wanaweza kudhani nina chuki na timu au wachezaji hao, hilo si kweli kwani kitendo hicho ni kwa ajili ya maendeleo ya Yanga na soka la Tanzania kwa ujumla.

Ni wazi kwa sasa wanandinga hawa wazawa hawastahili kuendelea kutegemewa kuipa mafanikio Yanga, nasema hivyo kwa sababu, licha ya umri wa Cannavaro kumtupa mkono lakini uwezo wake uwanjani unazidi kupotea siku hadi siku.

Tunajua kuwa moja ya wachezaji wa timu hiyo wanaostahili sifa kwa kuitumikia kipindi kirefu na mafanikio mkubwa ni Cannavaro, lakini huyu wa sasa si yule aliyekuwa akizisumbua safu za ushambuliaji kwa wapinzani.

Kwa mechi kadhaa zilizopita, Cannavaro ameonekana kuwa uchochoro mzuri wa wapinzani, hili si kosa lake na hastahili kulaumiwa kikubwa ni kuelewa  kwa sasa uwezo wa kukaba, kukimbia na hata kupiga mipira ya vichwa haupo tena.

Hali hiyo ipo pia kwa Oscar, kiasi cha mara kwa mara wachambuzi wa soka, mashabiki na Wanayanga kujiuliza ni vipi kocha Hans anaendelea kumwamini.

Sitaki kuamini kuwa timu kubwa yenye fedha za kumsajili mchezaji mwenye uwezo inashindwa kupata beki bora, kuliko hao ukimtoa Haji Mwinyi ambaye naye kwa sasa anaonekana jipu ndani ya Yanga, lakini pia sitaki kuamini iwapo Vicent Bossou akipata jeraha la kumweka nje kwa miezi sita beki ya Yanga itaendelea kuwa mbovu kwa kuwatumia watu waliokwishapoteza uwezo uwanjani.

Oscar, Cannavaro wanazifahamu kasumba za timu za Bongo na mashabiki wake, ni heri wakajiondoa  mapema kuliko kusubiri kupigiwa kelele za aondolewe.

Haitapendeza Cannavaro na Oscar walioitumikia timu ya taifa na Yanga kwa heshima kubwa kutangazwa kuachwa na sababu ikiwa kushuka kwa viwango vyao, hii ni aibu, kiroho safi, si dhambi kutundika daluga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles