30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wajua dawa ya mawifi wakorofi?  

WIFINA JOSEPH SHALUWA

MAISHA ya ndoa ni matamu sana ikiwa mume na mke wataishi kwa amani na upendo. Lakini wakati mwingine ndugu wa mume, hasa mawifi huweza kusabisha timbwili katika ndoa na kufanya iwe chungu.

Mawifi (siyo wote) mara nyingi huwa na gubu, hujikuta wakiwa kwenye chuki na mke wa kaka yao kwa sababu za hapa na pale, lakini kubwa zaidi hujiona wana haki zaidi kuliko mwanamke huyo kwa sababu  mumewe ni ndugu yao wa damu.

Hizo ni changamoto za kawaida kwenye maisha ya ndoa. Wanawake wengi hujikuta katika wakati mgumu wanapokuwa wakiishi na mawifi wakorofi ndani ya nyumba.

Hata hivyo zipo njia za kutumia ili kukabiliana nao, maana ukweli ni kwamba wanabaki kuwa ndugu wa damu wa mume wako mpenzi. Lazima busara itumike ili kulinda ndoa yako lakini pia undugu wa mumeo na dada zake.

Je, umekumbana na mawifi wakorofi ambao wanakupa maneno yenye kero wa sababu mbalimbali? Labda hujabahatika mtoto na mawifi zako wanakutolea maneno ya shombo? Fuatana nami.

KUWA NA BUSARA
Lazima uwe na busara na moyo wa uvumilivu ili uweze kukabiliana na mawifi wakorofi. Mwingine anaweza akawa analala kutwa nzima bila kusaidia kazi za nyumbani halafu mume anapokuja jioni anakuwa wa kwanza kumwambia maneno ya ajabu.

Hata kama amemwambia kaka yake kuwa labda hushindi nyumbani, baada ya yeye kuondoka asubuhi na maneno mengine mengi kutokana na chuki zake binafsi, unapaswa kutumia busara za hali ya juu.

Kumbuka hao ni mtu na ndugu yake hivyo ni vigumu sana kuwachonganisha, kama ukitumia maneno makali na kujibizana na wifi yako au mumeo.

Kujibizana naye mbele ya mumeo, inaweza kuwa chanzo cha mumeo kuamini aliyoambiwa na dada yake kuwa na ukweli. Msikilize na utulie usiwe na makuu, lakini kama akimuuliza mbele yake unatakiwa kujibu kuwa anayosema siyo ya kweli.

Lakini inawezekana wifi yako akawa amepandikiza maneno hayo kwa chuki zake binafsi au anakuonea wivu jinsi mumeo anavyokununulia nguo kila kukicha wakati yeye kama dada yake hajawahi kumnunulia nguo za gharama kila wakati kama anavyofanya kwako.

Maneno yote hayo na hasira zote atakazokuwa nazo mumeo unatakiwa kumalizia chumbani! Mwache mumeo hasira zake zitulie, baada ya kuoga na kula chakula cha jioni, ataingia chumbani kwa ajili ya kupumzika, usimsumbue, mwache alale mpaka usingizi umpitie.

Kama ataanzisha mazungumzo kwa kukukaripia, usijibizane naye zaidi ya kumuomba msamaha, kama atalala kimya ni sahihi zaidi. Ikifika muda wa saa nane na kuendelea unatakiwa kumuamsha na kuzungumza naye kwa lugha tamu.

Mweleze kuwa maneno ya wifi yako siyo ya kweli lakini kwa lugha nzuri na ya ushawishi ili akuelewe. Kama kuna mazingira yoyote ambayo wifi yako alikuwa ameyatengeneza yanayosababisha kutokuelewana kwenu unapaswa kuweka bayana.

Kwa kutumia lugha nzuri ni wazi kuwa mumeo atakuelewa na kukusamehe ambapo naamini kuwa usiku huo utakuwa wenye kila aina ya furaha na bashasha zilizojaa  cheche za mapenzi.
MWANZO ULIKUWAJE?
Jinsi unavyoanza ndivyo unavyomaliza, kama ukivurunda kitu kuanzia mwanzo, tarajia kuharibu mpaka mwisho. Kinachotokea mwishoni ni kupunguza madhara ya tatizo ambalo tayari limeshatokea na lina madhara makubwa.

Inawezekana tangu ulipokwenda kijijini kwao (ukweni) ulishaona baadhi ya tabia zake mbaya ambazo kwa namna moja ama nyingine zilikukwaza.

Kwanza mumeo atakapokupa taarifa ya ujio wa wifi yako, usioneshe kukasirika, kwa sababu kama ukionesha umekasirika, anaweza akahisi jambo fulani baya kwako.

Pengine atahisi humpendi dada yake hivyo hata siku akikukosea na kumwambia ataamini ni fitina au chuki zako binafsi. Siku wifi yako anapokuja nyumbani, kuwa wa kwanza kumkumbusha mumeo kwenda kumpokea kituoni, weka maandalizi motomoto na onyesha furaha ya ujio wake.

Ukimfanyia hayo, hata kama alikuwa na lake moyoni, atajisikia vibaya kukufanyia kwa kuhofia mema uliyomfanyia. Hata hivyo, kama ana ukorofi wa asili haiwezi kuwa dawa, anaweza akatafuta visa vitakavyokuudhi baadaye.

MALIZENI WENYEWE
Ikiwa wifi yako amekukosea jaribu kuzungumza naye. Inawezekana ghafla alianza kuwa na maneno ya hapa na pale au wivu usioeleweka, pengine alimwambia mumeo, kuwa una tabia mbaya au vyovyote katika kukuharibia ndoa yako. Usionyeshe chuki, zungumza naye taratibu.

Mweleze jinsi unavyompenda na kuuthamini uhusiano wenu. Ikiwa utatumia lugha nzuri naamini atakuelewa lakini kama siyo muelewa ataendelea na chokochoko zitakazokukera.
MSHIRIKISHE MUMEO
Kama yote hapo juu hayakufua dafu, unapaswa kukaa chini na mumeo na kumweleza juu ya jambo hili. Kukaa kwako kimya na kumvumilia kutakuwa hakuna maana, kwa sababu ni rahisi ndoa yako kuvunjika.

Usimfiche chochote, hata kama aliwahi kukutolea maneno machafu kwa mumeo, usijali, zungumza taratibu bila jazba huku ukitumia hoja kuliko maneno matupu!

Nyumba ni kwa ajili yako na mumeo. Kuolewa hakumaanishi kwamba umeolewa na ukoo mzima na kila mmoja anaweza kukudhihaki na kukutukana.

Lazima utambue haki yako na kama mumeo ana mapenzi ya dhati kwako, lazima atakupa kipaumbele na kufanya maamuzi sahihi kwa heshima na sababu ya kuilinda ndoa yenu ambayo ni muhimu sana.

Kumbuka ukitumia kauli chafu au kukaripia, utamfanya ahisi kuwa una chuki na ndugu yake na unataka kuwagombanisha. Usiruhusu fikra hizo akilini mwake.

Kama ulianza vizuri, atashawishika kukuamini maana atajaribu kufikiria jinsi ulivyokuwa ukimkirimu ndugu yake tangu awali kisha atalinganisha na madai yake.

Kumbuka mumeo atakuwa anamfahamu vizuri zaidi dada yake, kama ana matatizo hayo atakuwa anayafahamu kabla, hivyo utatuzi wake kuwa mzuri usio na migogoro!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles