25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

CANNAVARO NI KWELI UMESHINDWA KUMWANDAA MRITHI WAKO YANGA?

Na ZAINAB IDDY


FEBRUARI 25, ilimalizika vibaya kwa mashabiki wa soka hususani wale wapenzi wa Yanga, baada kushuhudia timu yao ikipokea kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa watani zao, Simba.

Yanga walijikuta wakipokea kipigo hicho kitakatifu kutoka kwa Simba, ikiwa ni mara ya pili mfululizo tangu kuanza kwa mwaka huu baada ya awali kunyanyaswa pia kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, lililofanyika Zanzibar kwa kufungwa kwa mikwaju ya penalti 4-2 katika mechi ya nusu fainali.

Ikiwa ni mwezi mmoja tu umepita, mashabiki wa Yanga wamejikuta katika maumivu hayo tena kibaya zaidi wapinzani wao waliweza kurudisha bao na kuwaongeza lingine wakiwa pungufu baada ya beki wao, Janvier Bokungu, kutolewa kwa kadi nyekundu na mwamuzi Mathrew Akrama.

Mara baada ya mchezo huo, lawama nyingi zilionekana kuwaendea baadhi ya wanandinga wa Yanga, Haruna Niyonzima, Haji Mwinyi na Deogratius Munishi ‘Dida’, ambao ni wazi walicheza wakiwa chini ya kiwango, hivyo walistahili kubebeshwa zigo hilo la misumari.

Wakati mashabiki na viongozi wa timu hiyo wakionekana ni vigumu kwao kusahau kipigo cha Simba, Kiroho safi inakwenda mbali zaidi kwa kuangalia nafasi ya Nadir Haroub ‘Cannavoro’ ndani ya Yanga na yale yaliyotokea mara baada ya mchezo.

Inakumbukwa katika mchezo huo, Kelvin Yondani na Dida walionekana kutupiana lawama na hata kufikia hatua ya kushikana, lakini pia Niyonzima na wengine wakiwarushia maneno yasiyofaa mashabiki wa timu hiyo.

Hii si mara ya kwanza kwao kufanya hivyo, kwani kumbukumbu zinaonyesha katika mechi yao dhidi ya Mbeya City waliyofungwa 2-1 na ile ya sare ya bila kufungana mbele ya Azam FC, ambayo iliweza kusababisha baadhi ya wachezaji kutaka kupigwa na mashabiki kutokana na kuwajibu maneno ya ovyo.

Jambo hili ndilo lililonikumbusha nafasi ya Cannavaro ndani ya Yanga, kwani moja ya wachezaji wanaosifika kwa kuwa na busara ndani na nje ya timu ni Mzanzibari huyo.

Lakini tangu beji ya unahodha ikabidhiwe kwa wasaidizi wake, Vicent Bossou na Niyonzima, hali ya nidhamu imekuwa mbovu kwani kila mchezaji ana uwezo wa kuzungumza chochote, mahali popote na mtu yeyote pasipo kuangalia nafasi ya timu yake.

Kamwe kipofu hawezi kumwongoza kipofu mwenzake, ndivyo ilivyo kwa Bossou na Niyonzima wao wenyewe hawana nidhamu watawezaje kuwaongoza wengine?

Lakini suala la kujiuliza hivi ni kweli Cannavaro ameshindwa kumwandaa mrithi wake kama ilivyokuwa Nsajigwa kuja kwake au ndio kusema naye kwa sasa yupo ilimradi kuongeza idadi ya namba ya wachezaji.

Nafasi ya kucheza hana, nini jukumu lake hivi sasa ndani ya Yanga,  je, ni kuvaa jezi na kuvua, kufanya mazoezi na kukaa benchi kama tayari amekubali hana namba ndani ya Yanga na ameamua kuwaachia wadogo zake, iweje ashindwe kumwandaa atakayebeba mikoba yake kuendelea kuipa hadhi beji ya unahodha kama alivyokabidhiwa yeye na Nsajigwa?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles