29.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

CAG aanika ununuzi magari ya Serikali ulivyoongezwa

Mwandishi wetu – dar es salaam

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2017/18, imebainisha

kuwa Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA) haukuendesha ushindani madhubuti katika kufanya manunuzi ya magari ya Serikali.

Inasema bei iliyotolewa na Kampuni ya Toyota Tanzania ilikuwa juu kwa asilimia 15 hadi 49 ikilinganishwa na bei za magari za Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UN) kwa aina ya magari na viwango vya ubora vinavyofanana.

“Ilibainika kuwa Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini ukinunua magari ya viwango vya ubora vinavyofanana kutoka kwa mawakala wengine tofauti na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa, hupoteza takribani Sh milioni 10 hadi 50 kwa kila gari moja lililonunuliwa,” inasema ripoti hiyo.

inasema ukaguzi ulibaini magari yaliyonunuliwa hayakufika kwa wakati wala kwa idadi iliyotakiwa. Ucheleweshaji wa magari ulikuwa kwa hadi siku 130.

MALIPO HEWA NHIF

Kuhusu Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ripoti imebainisha kuwa ulitoa mkopo wa Sh bilioni 24.6 kwa Wizara ya Mambo ya Ndani Agosti 2010 kwa ajili ya ununuzi wa magari na ilitakiwa kuanza kuurejesha baada ya kipindi cha mwaka mmoja yaani Agosti 2011, kwa kipindi cha miaka minane.

“Hadi kipindi cha ukaguzi huu, mkopo huo ulikuwa bado haujarejeshwa.

“Mwaka 2012, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya pia ulitoa kiasi cha Sh bilioni 114.1 kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa bila ya kuwa na makubaliano yoyote ya kimaandishi, hali iliyosababisha kutolipwa kiasi chochote hadi kipindi cha ukaguzi huu,” alisema CAG Profesa Mussa Assad katika ripoti yake.

Alisema japokuwa makusanyo ya mwaka yanaendelea kuwa makubwa zaidi ya malipo ya huduma za bima ya afya, kwa sasa malipo ya huduma za afya yanakua kwa uwiano mkubwa mwaka hadi mwaka zaidi ya uwiano wa kukua kwa mapato.

 “Kutokana na hali hii, makisio ya madai ya huduma za bima ya afya pekee ifikapo mwaka wa fedha utakaoishia Juni 2024 yatakuwa ni asilimia 99.2 ya jumla ya makusanyo yote. Uwiano huu unakisiwa kuongezeka zaidi hadi kufikia asilimia 104.8 katika mwaka unaofuata,” alisema.

Ripoti hiyo inasema NHIF inaweza kuyumba kutokana na aina ya matumizi ya huduma zake, ambapo kundi la KIKOA, matumizi yalikuwa asilimia 710, kundi la viongozi wa dini, matumizi yalikuwa asilimia 401; kundi la Toto Afya Kadi, matumizi yalikuwa asilimia 298; kundi la madaktari wa mafunzo kwa vitendo, matumizi yalikuwa asilimia 174; kundi la wanafunzi, matumizi yalikuwa asilimia 171; na kundi la wachangiaji binafsi, matumizi yalikuwa asilimia 160.

Inasema hali hiyo isipodhibitiwa, itadhohofisha hali ya kifedha na utendaji wa mfuko.

Inaongeza kuwa hii inamaanisha kwamba madai ya huduma za bima ya afya yanaendelea kuongezeka, na itafikia kipindi ambapo makusanyo na mapato kutoka katika uwekezaji hayataweza kukidhi madai na hivyo itaulazimu mfuko kuchukua hatua za dharura kama kuuza mali zake.

UKIUKAJI WA SHERIA YA MANUNUZI

Ripoti inasema pia Sh bilioni 4.61 zilitumika kununua bidhaa, huduma, ushauri wa kitaalamu, na kazi za ujenzi ndani ya wizara, idara, na sekretarieti za mikoa pasipo kutumia taratibu za kushindanisha wazabuni kinyume na kanuni za 163 na 164 za kanuni za manunuzi ya umma za mwaka 2013.

Inasema taasisi saba zilifanya manunuzi yenye thamani ya Sh bilioni 5.37 bila kupata vibali vya bodi za zabuni kinyume na kifungu cha 35 (3) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2011, na Kanuni 55 ya Kanuni za Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2013.

CAG alizitaja taasisi hizo kuwa ni Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa, Sekretarieti ya Mkoa wa Geita, Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga, Wizara ya Katiba na Sheria, Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi Tanzania na Ofisi ya Rais – Idara ya Kumbukumbu na Utunzaji wa Taarifa.

 “Taasisi tano zilifanya manunuzi ya bidhaa, huduma, na kazi za kiasi cha Sh bilioni 1.17 bila kuwapo kwa makubaliano ya kimkataba na wazabuni. Hii ni kinyume na kanuni namba 10 (4) ya Kanuni za Manunuzi ya Umma za Mwaka 2013,” alisema CAG.

UDHAIFU USIMAMIZI WA MATUMIZI

Ripoti ya CAG inasema katika mapitio ya taarifa za matumizi ya fedha za umma, alibaini pia dosari katika udhibiti wa ndani, ikiwemo matumizi ya Sh bilioni 4.66 yaliyofanywa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwenda kampuni binafsi za huduma za kisheria bila kufuata makubaliano ya mikataba.

Inasema taasisi 20 za Serikali kuu pia ziliwalipa watoa huduma mbalimbali kiasi cha Sh bilioni 1.43 pasipo kudai stakabadhi za kielektroniki.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, taasisi hizo ni Sekretarieti ya Mkoa wa Njombe, Sekretarieti ya Mkoa wa Katavi, Idara ya Uhamiaji, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Waziri Mkuu-Ofisi Binafsi, Idara ya Huduma za Magereza, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano – Sekta ya Mawasiliano, Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga, Mahakama ya Tanzania na Sekretarieti ya Mkoa wa Tanga.

Nyingine ni Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi, Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi – Hospitali ya Rufaa Sokoine, Sekretarieti ya Mkoa wa Pwani, Sekretarieti ya Mkoa wa Kilimanjaro, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Tume ya Maendeleo ya Usharika Tanzania, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Kilimo.

CAG alisema malipo yalifanyika kimakosa katika vifungu visivyostahili ya kiasi cha Sh bilioni 885.99 kinyume na kanuni ya 42(2) ya Kanuni za Fedha za Umma za Mwaka 2001.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,905FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles