NA, HUSSEIN JUMA, DODOMA
HOTUBA yake ya Aprili 13, 1986, Munsieville, wakati mumewe Nelson Mandela akiwa gerezani na yeye mwenyewe akiwa kizuizini, inawakumbusha mengi wananchi wa Afrika Kusini.
Winnie Mandela alisema, ‘with our boxes of matches and our necklaces, we shall liberate this country’, kwamba “kwa viberiti vyetu na matairi yetu (ya kuwachomea makaburu), tutaikomboa Afrika Kusini,”
Winnie Mandela hakuwa mwanamama wa mchezo mchezo na aliamini usemi ambao vijana wa kileo huutumia, usemi wa ‘jino kwa jino’. Hakuwa tayari kungojea kuona wananchi wa Afrika Kusini wakinyanyasika, hasa kipindi cha utawala wa kibaguzi wa makaburu (Apartheid rule); na wala Winnie Mandela hakuwa tayari kukaa meza moja na yeyote aliyemhisi kuwa njia moja na kaburu.
Ni swali la kujiuliza, kwa nini Winnie aliwachukia makaburu kupita kiasi na kufikia kiasi kwamba yeye kuua kaburu ilikuwa kama kutafuna jojo? Pengine ni maisha aliyoishi kwenye utawala wa kidhalimu wa makaburu. Pengine Maisha magumu aliyoishi chini ya utawala wa makaburu. Winnie amekua na hasira na chuki dhidi ya makaburu.
Ukweli ni kwamba, ukisema kuwa Winnie aliamini ‘jino kwa jino’, utaona waziwazi hasa miaka miwili baada ya hotuba yake ile Munsieville. Tukio moja ambalo lilliwahi kuelezewa na mlinzi wake binafsi, Jerry Musivuzi ni kwamba, Disemba 29, 1988, Winnie Mandela alimpa amri Richardson, kocha wa iliyokuwa timu ya mpira ya Mandela, The Mandela United Football Club (inasadikika kuwa, klabu hii ilitumika kama ulinzi binafsi wa Winnie Mandela, wakati Nelson Mandela akitumikia kifungo. Na inadaiwa kuwa, klabu hii ilijihusisha na matukio kadha wa kadha dhidi ya makaburu) kuwateka vijana wanne, akiwamo kijana wa miaka 14 James Seipei, mtoto wa aliyekuwa Paroko, Rev Paul Verryn na kuhakikisha wanawatesa hadi kupata ukweli wa kile alichokihisi kuwa, nyumbani mwa paroko, walikuwako wasichana wa kiafrika waliokuwa wakitumikishwa kwa ngono.
Siku ya sita ya mwezi Januari, 1989, mwili wa Kijana Seipei ulipatikana ukiwa na jeraha lililotokezea kooni ikiwa ni dalili kwamba, hapana shaka kijana yule alipata mateso makali ikiwa ni pamoja na kuchomwa kisu kilichotokezea kooni. Na kuna vyanzo vinaeleza kuwa, kuteswa hadi kuuawa kwa kijana Seipei kulimpa ukweli Winnie Mandela juu ya kile alichokihisi awali, ingawa hakuna taarifa rasmi zinazoweza kuthibitisha juu ya hili.
Jina kamili alilopewa na wazazi wake Nomzamo Winfred Zanyiwe Madikizela, mwenye asili ya Xhosa, aliyezaliwa nje kidogo ya Jimbo la Eastern Cape, aliyezaliwa Septemba 26, 1936. Kwa maana hiyo, Madikizela amezaliwa miaka michungu ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia na kuna tukio moja la sherehe za ukomo wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia; sherehe zilizopanda mbengu ya chuki dhidi ya makaburu moyoni mwake. Kwa lugha yao, neon ‘Nomzamo’ lilimaanisha ‘Binti anayejaribu’, na kwa maana hiyo liliendana kabisa na haiba ya Madikizela, kwani hakuwa mwanamama wa kukata tamaa toka akiwa mtoto na hata akiwa mkubwa.
Hata baada ya kifo cha mama yake akiwa na miaka tisa, Madikizela hakuwa binti wa kukata tamaa. Familia yake ilisambaa na nduguze wote wakachukuliwa sehemu mbali mbali kwa ajili ya malezi, lakini yeye alibaki pale na hata kumaliza masomo yake ya pili na baadaye kupata shahada ya Mahusiano ya kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Witwatersrand
Ukisema Maisha magumu kwa wananchi wa Afrika Kusini, Madikizela hakuwa ameyasoma kwenye kitabu; aliyaishi. Baba yake Columbus na Mama yake Getrude walikuwa walimu wa shule ya Bizana na kwa wakati huo wakiwa chini ya utawala wa kidhalimu wa makaburu.
Siku moja mwaka wa 1945, baada ya taarifa kusambaa kuwa, Vita Kuu ya Pili ya Dunia imefika ukomo, makaburu walifanya sherehe kwa taarifa zile. Madikizela alimuomba baba yake waende pamoja kwenye sherehe ile (Baba yake alikuwa Mkuu wa Shule Bizana, hivyo ilikuwa rahisi kwake kupewa mwaliko kwenye sherehe za kikaburu) na kweli baba yake hakuwa na hiyana kufanya hivyo. Kwa mujibu wa vyanzo vingi vya kisa hiki, inadaiwa kwamba, walipofika eneo la sherehe, ukumbini, Mzungu mmoja aliwafuata kabla hawajakaa na kuwaambia, ‘these celebrations were for whites only’, yaani, “Sherehe zile ziliwahusu Wazungu tu,” Madikizela na baba yake walitolewa nje na kubaki hapo kwa dakika kadhaa wakishuhudia sherehe ile ikiendelea.
Kisa hiki kilimkaa sana Winnie, kwani amekuwa akikirudia aghalabu kwenye hotuba zake dhidi ya utawala wa kidhalimu wa makaburu (Apartheid rule), na pindi akikisema kisa hiki, alikuwa akionesha hisia kali za kuwachukia makaburu kwa kila namna na hapana shaka hata tukio la kumtesa hadi kumuua kijana wa Paroko la mwaka 1988 lilikuwa na ‘Resentments’ za udhalimu huo.
Siku chache baadaye, Winnie alishuhudia tukio moja ambalo hakika lilimsisimua na kumjaza chuki zaidi dhidi ya makaburu. Lilikuwa hivi. Bizana, sehemu ambayo alipozaliwa, kulikuwa na Waafrika wengi sana weusi, lakini karibu maduka yote yalikuwa yakimilikiwa na makaburu. Kwa mbali Winnie alimuona baba mmoja Mwafrika akikwangua kwangua mkate na kumlisha mke wake aliyekuwa akinyonyesha mwanae. Mara ghafla, akatokea mtoto wa kikaburu, hadi pale walipokuwa wamekaa na kisha kuwatolea maneno ya kashfa na baadaye kuwapiga na kuwaharibia mkate ule, kisha kuwafukuza eneo lile.
Jamaa yule Mwafrika hakuweza kabisa kufanya lolote zaidi ya kuondoka kwa aibu. Winnie alijiuliza, kwa nini wanaume wengi Waafrika wanaonewa na wala hawafanyi chochote? Lakini baadaye akadhani, pengine jamaa yule angemrudishia mtoto yule, basi hali ingekuwa mbaya zaidi. Sasa, tukio lile liliendeleza kawaida ya watoto wa kiafrika, kama Winnie, kuona baba zao wakifanyiwa udhalimu, wao kutokufanya lolote, hivyo akili yake ikazidi kujaa chuki isiyo na kifani. Masomo ya Winnie yamegharimiwa na dada yake, Nancy, ambaye aliacha shule kwa kukosa fedha na kisha kuanza kufanya kazi ndogondogo ili aweze kumlipia mdogo wake ada.
Madikizela kama Mke wa Mandela na hata baadaye
Vyanzo vingi vinaeleza kuwa, mahusiano ya Winnie na mwanaharakati, mwanamasumbwi na mwanasheria nguli na hata baadaye Rais na Baba wa Taifa la Afrika Kusini, Nelson Mandela yalichipuka mwaka 1957. Ingawa vyanzo hivi vinaonesha kuwa, mahusiano haya yalianza huku Winnie akiwa kwenye ndoa mfu na Evelyn Mase, lakini havielezi ni wapi hasa walipokutana na kuanzisha mahusiano na nini hasa kilikuwa chanzo cha wao kupendana, licha ya ukweli kwamba, Winnie si tu alikuwa na sura ya upole, bali pia alikuwa mrembo wa sura na mwenye tabasamu la bashasha lisilo na ukomo.
Utakubaliana na mimi kuwa, Winnie alikuwa mpole, mwenye haiba ya ukarimu na pia mcheshi wa mara zote. Nimemuona mara ya mwisho Winnie wiki kama tatu tu alipohudhuria tafrija ya kuhitimu masomo yake kiongozi mwandamizi na mbunge wa bunge la Jamhuri ya Afrika Kusini kwa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF), Mbuyiseni Ndlozi. Sherehe ile ilikuwa ya aina yake hasa baada ya kuingia Winnie akiwa ameshikwa mkono na Mwenyekiti wa EFF, Julius Sello Malema. Watu kwenye ukumbi walikuwa wakiangua vicheko visivyo na ukomo wakati wa salamu za Winnie Mandela, kwani aliongea akionesha kuwa mpenzi wa masihara ya hapa na pale. Nakumbuka aliwaambia pale ukumbini kuwa, “Leo hii hata Mandela angalikuwa hai, basi angalikuwa keshakwisha kuhamia EFF,” VIcheko vilitawala kwa kweli.
Kama nilivyosema, kila mmoja huandika lake juu ya lini hasa walianza mahusiano na Mandela. Kuna wanaosema kuwa, Madikizela alikutana na Mandela kwenye kituo cha mabasi Soweto mwaka huo wa 1957 na siku moja baadaye wakapanga miadi kukutana hotelini; sehemu ambayo ajenda yao ya mahusiano ilihitimishwa. Wapo pia wanaosema, Winnie alikutana na Mandela kabla ya hapo akiwa kwenye kazi zake za sanaa. Lakini yote haya, moja muhimu ni kwamba, wawili hawa walioana mwaka wa 1958, siku ya 14 ya Juni, hapo Bizana. Arusi yao ilitajwa na Gazeti la nchini humo, gazeti la Drum Magazine na The Golden City Post, kuwa ni sherehe iliyokuwa ya aina yake. Madikizela na Mandela walijaaliwa watoto wawili; Zenani na Zindziwa, mwaka 1958 na 1960.
Madikizela na Mandela walitalikiana mwaka 1966. Chanzo cha talaka inasadikika kuwa, Madikizela hakuwa mwaminifu kipindi mumewe alipokuwa akitumikia kifungo, lakini pamoja na kutalikiana, inadaiwa kuwa walikuwa wakikutana aghalabu hata baada ya hapo.
Madikizela Mandela, Simba jike la Simba Nelson Mandela
Ingawa si muhimu sana, lakini yapo madai yasiyo rasmi kuwa, Madikizela aliwahi kufanyiwa mahojiano kwenye kituo kimoja cha luninga na Nadiru Naipaul mwaka 2010 juu ya mumewe. Inasadikika kuwa, Madikizela alimshambulia sana aliyekuwa mumewe kwa kusema kuwa (Mandela) aliwaangusha sana watu weusi wa Afrika Kusini, akaenda mbali zaidi kiasi cha kumshambulia hata Askofu Desmond Tutu akimwita ‘Cretin’, yaani mpumbavu. Hoja yake kubwa ya kumshambulia Mandela ilikuwa ni kuikubali Tuzo ya Amani ya FW De Klerk. Aidha, Machi 14, 2010, kauli ilitolewa (hapatajwi ilipotoka) kwa niaba ya Madikizela kuwa, mahojiano yale yalikuwa ni uongo.
Licha ya madai yote haya, Madikizela anabaki kama nembo halisi ya ukuaji wa Nelson Mandela kwenye uwanja wa harakati na hata baadaye kuwa Baba wa Taifa si tu kwa sababu “kila ukimuona mwanaume aliyeendelea, jua yupo mama imara nyuma yake,” Lakini pia Winnie alikuwa mama imara katika uimara wake. Labda tuseme kwamba na kama Peter Hain, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Afrika alivyosema, Winnie anaweza kuonekana mbaya kwa maisha yake baada ya siasa, lakini ukweli utabaki pale pale kwamba, nuru yake ndani ya Taifa la Afrika Kusini haiwezi kuzimwa kiurahisi.
Oktoba 1958, akiwa kwenye misa, Winnie Mandela aliongoza mgomo wa wanawake dhidi ya ubaguzi wa rangi, kufuatia sheria iliyoitwa ‘Pass Law’ ambayo iliwataka Waafrika Kusini kutembea na Kadi; sheria ambayo ilirahisisha sana kudhibitii shughuli na mizunguko ya Waafrika Kusini. Tukio hili lilikuwa tunda la tukio lililokwisha kutokea Mjini Pretoria Agosti 1956 na lile la Johannesburg lililoongozwa na Rais wa Baraza la Wanawake la ANC, Lilian Ngoyi na Albertina Sisulu na wengine kadha wa kadha. Siku hiyo, Winnie alisafiri na Albertina kutoka Stesheni ya Phefeni hadi Jiji la Orlando; sehemu ambayo maandamano yalipokuwa yanaanzia. Kwenye maandamano yale, wanawake zaidi ya 1000 walitiwa nguvuni.
Madikizela Mandela hakuwa mtu mwenye hofu kusema kwamba, kwa kuwa mumewe alifungwa, basi hata yeye asijihusishwe kabisa na harakati. Kwake ilikuwa ni tofauti kabisa. Maisha ya harakati kwake yalikuwa kwenye damu. Mara nyingi, ingawa ni kwa misukosuko kibao, alikuwa akimtembelea mumewe gerezani katika Kisiwa cha Robben akiwa na bintize wawili. Kila alipofika gerezani kumuona mumewe, Madikizela alikuwa akimkumbusha kuwa, hakupaswa kukata tamaa na harakati, kwani Taifa lilikuwa likimtegemea. Hakuchoka kumkumbusha tukio la Juni 16, 1976 kule Soweto; siku ambayo watoto kadhaa wa Afrika Kusini pamoja na aliyekuwa mwalimu wao, mwanaharakati mwingine, Steve Bantu Biko, waliuawa kinyama, tena mchana kweupe kwa shambulio la kutisha, kisa tu kupinga lugha ya kikaburu kutumika kama lugha ya kufundishia. Alimkumbusha pia matukio kadha wa kadha ya kibaguzi ambayo ama kweli yalimfanya Mandela kuwa imara, licha ya kuwa alikuwa akitumikia kifungo.
Madikizela na ANC na siasa Afrika Kusini
Uchaguzi wa ANC, NEC wa Disemba 21, 2007, Winnie Mandela alikuwa na ushawishi mkubwa sana. Ushawishi huu ulitokana na nini hasa?
Kwanza, kama nilivyotangulia kusema awali, moja ya vitu vilivyomvutia Nelson Mandela kwa Madikizela ni ukarimu wake. ANC inathibitisha hili, kwani mara nyingi ilikuwa ikiutambua mchango wake ndani ya chama kwa kuwa ndiye mwanamama aliyekuwa na uwezo wa kujishusha na kuwa karibu na watu maskini, hivyo maskini wengi na hata matajiri, walimpenda sana Madikizela.
Ingawa alikuwa anaamini kwenye ule usemi wa ‘jino kwa jino’, Madikizela alipinga na kulaani vikali sana masaibu yaliyokuwa yakiwapata makwirikwiri (Immigrants) nchini humo kati ya mwezi Mei na Juni ya mwaka 2008. Winnie alijishusha na kuwaomba msamaha Makwirikwiri na aliipatia hifadhii yake binafsi familia ya kwirikwiri mmoja mwenye asili ya Kikongo na kuionya Serikali kuwa, Afrika Kusini ingeelekea kwenye machafuko kwa vitendo vya kihalifu vya Afrika Kusini dhidi ya Makwirikwiri.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2009, Madikizela alishika nafasi ya tano baada ya Jacob Zuma, Kgalema Montlanthe, Mbaleka Mbete (Spika wa Bunge wa sasa, akiwa kama Makamu wa Rais kwa mwaka huo) na Trevor Manuel.
Winnie Mandela amefariki katika Hospitali ya Milpark, jijini Johannesburg, siku ya Aprili 2, 2018 kwa maradhi ya muda mrefu kama ambavyo msemaji wa familia alivyosemea kuwa, amekuwa akisumbuliwa na kKisukari na hivi karibuni alifululiza kwenda hospitali kwa ajili ya matibabu.
Buriani Winnie Madikizela Mandela, Simba jike la Afrika Kusini! Mama wa Afrika! Sura halisi iliyomshtua kaburu na utawala wake wa kibaguzi! Mama uliyeleta ukombozi halisi wa Afrika Kusini mumeo akiwa gerezani.
Roho yako ilazwe mahali pema peponi na hakika kila nafsi itaonja mauti!
Makala hii imeandikwa na Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Kitivo cha Elimu kama sehemu ya kumbukumbu ya maisha ya marehemu.
Simu: +255 759 947 397
Barua Pepe: [email protected]