32.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

AFRIKA IMEMPOTEZA MAMA WINNIE MANDELA

Na, JULIUS MTATIRO



MAMA Winnie Mandela, Mke wa zamani wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini Marehemu Nelson Mandela, amefariki dunia.

Winnie ambaye majina yake rasmi ni Nomzamo Winifred Madikizela Mandela ambaye alikuwa mmoja wa wanawake walioongoza mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, amefariki dunia akiwa na miaka 81.

Mama Winnie amefariki akiwa katika matibabu kwenye Hospitali ya Netcare Milpark ya Johannesburg  Jumatatu  ya Aprili, 2018 saa za alfajiri.

Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, Winnie amekuwa “ON and OFF” hospitalini hadi alipokutwa na umauti akiwa amezungukwa na familia yake.

Winnie alizaliwa mwaka 1936 eneo la Bizana lililoko Estern Cape na alihamia Johannesburg akiwa kijana kwa ajili ya kusomea masuala ya kijamii ambapo alikutana na Nelson Mandela mwaka 1957 na wakafunga ndoa mwaka 1958 na kupata watoto wawili.

Kwa sababu ya ukatili wa Serikali ya makaburu, ndoa ya Winnie na Mandela ilipatwa na huzuni baada ya Mandela kufungwa kifungo cha maisha mwaka 1963 akituhumiwa kutenda makosa ya uhaini. (Mandela aliachiwa huru mwaka 1990 baada ya kukaa gerezani kwa miaka 27).

Wakati Mandela yuko gerezani, Winnie hakusita kuendeleza mapambano dhidi ya makaburu kwa hiyo walimkamata na kumuweka kwenye kizuizi cha nyumbani. Mara nyingine mwaka 1969, Winnie aliwekwa kizuizini kwa miezi 18 gerezani.

Kuna wakati mwanzoni mwa miaka ya 1990 Winnie alikutwa na hatia ya kuhusika kwenye mauaji ya mwanaharakati Stompie Seipei (ambaye inasadikiwa aliuawa na walinzi wa Winnie), Winnie akahukumiwa kifungo cha miaka sita gerezani baadaye kifungo kikapunguzwa na kuwa faini na miaka miwili ambavyo vyote viliondoshwa kwa rufaa.

Ndoa ya Winnie na Mandela ilianza kudorora sana mara tu Mandela alipotoka gerezani baada ya Winnie kutuhumiwa kuwa alikuwa na mahusiano na wanaume wengine vijana.

Uthibitisho wa kuwa Winnie alikuwa “anam-cheat” Mandela ni pale ambapo moja ya barua ambazo Winnie alimuandikia mpenzi wake iliishia mikononi mwa magazeti na ikaripotiwa MUBASHARA bila chenga na kuleta aibu kubwa kwa Mandela na familia yao.

Katika barua hiyo Winnie alikuwa ameandika, “..Hujatulia, unahangaika na visichana vingine huku mimi ukinipa visingizio tele…hali mbaya ya mahusiano yangu na “Tata” (Mandela) na kutozungumza kwetu (mimi na Mandela) kwa miezi mitano kunaonekana hakukugusi. Naendelea kukwambia mahusiano yangu na Mandela yanafifia na wewe haujali kwa sababu kila usiku unaridhishwa na wanawake wengine…”

Katika kitabu cha Mwanasheria nguli George Bizo kiitwacho “Odyssey to Freedom”, Bizo amewahi kufichua kuwa Mandela alikuwa anakwepa kuhudhuria mashauriano ya kisheria ambayo Bizo alikuwa akiyafanya na Winnie wakati Winnie akishtakiwa kwenye kesi ya mauaji ya Seipei.

Sababu ya Mandela kutohudhuria mashauriano hayo ni uwepo wa hasimu wake (hasimu wa Mandela) ambaye alikuwa anachepuka na Winnie wakati Mandela akiwa gerezani na hadi alipotoka gerezani, ambaye (mchepuko), alikuwa anashiriki kwenye mashauriano hayo kama mwanasheria. Mandela akaona hawezi kukaa meza moja na mwanaume anayemshughulikia mke wake.

Baada ya uchaguzi wa mwanzo wa kidemokrasia wa Afrika  Kusini mwaka 1994, Winnie alichaguliwa kuwa mbunge na akateuliwa kuwa Naibu Waziri wa Michezo na Utamaduni. Lakini baadaye Mandela alimfukuza kazi baada ya Winnie kufanya safari ya kiserikali kwenda Ghana bila ruhusa ya Ofisi ya Rais.

Mandela na Winnie waliachana rasmi mwaka 1996, miaka 37 baada ya ndoa yao.

Winnie anabakia kuwa mwanamama mfano halisi wa umuhimu wa wanawake kwenye safari ya ukombozi barani Afrika. Hadi anafariki amepokea tuzo nyingi sana kutoka mataifa mbalimbali, zikitambua mchango wake katika harakati za Uhuru wa Afrika Kusini.

Mungu ailaze roho ya Mama yetu Nomzamo Winifred Madikizela-Mandela mahali pema peponi. Amina

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles