23.8 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

BULAYA AUNGANISHWA KESI YA KINA MBOWE

NA KULWA MZEE -DAR ES SALAAM


MBUNGE wa  Bunda, Ester Bulaya (CHADEMA),  ameunganishwa kwenye kesi inayowakabili viongozi wanane wa chama hicho akiwamo  Mwenyekiti,   Freeman Mbowe, na kusomewa upya mashtaka 12.

Bulaya alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,  Wilbard Mashauri  jana.

Wakili wa Serikali  Mkuu,  Faraja Nchimbi,  aliomba kufanya mabadiliko  ya hati ya mashtaka kwa kumuongeza Bulaya, ombi ambalo lilikubaliwa na mahakama na kuwasomea mashtaka upya.

Mbali na Mbowe,  washtakiwa wengine ni  Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho,   Zanzibar Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika.

Wengine ni  Mbunge wa Tarime mjini, Ester Matiko na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vicenti  Mashinji, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Tarime vijijini, John Heche.

Wakili Nchimbi aliwasomewa washtakiwa  mashtaka 12.  Alidai katika shtaka la kula njama kuwa wanadaiwa kati ya Februari Mosi na 16,  mwaka huu,  wakiwa Kinondoni Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama na wengine ambao hawapo mahakamani, kwa kutenda kosa la jinai na kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

Bulaya anakabiliwa na shtaka la kushawishi kutenda kosa la jinai ambako anadaiwa Februari 16, mwaka huu,  katika viwanja vya Buibui Kinondoni Dar es Salaam alishawishi wakazi wa Kinondoni kutenda kosa la jinai kwa kufanya maandamano yenye vurugu.

Nchimbi alidai washtakiwa wote Februari 16, mwaka huu, wakiwa katika barabara ya Kawawa, Kinondoni Mkwajuni, Dar es Salaam, kwa pamoja wakiwa wamekusanyika kutekeleza lengo la pamoja kinyume cha sheria, waliendelea na mkusanyiko katika namna iliyowafanya watu waliokuwa kwenye eneo hilo waogope watakwenda kwenye uvunjifu wa amani.

Inadaiwa washtakiwa wote katika tarehe hiyo wakiwa kwenye barabara hiyo kwa pamoja katika ujumla wao wakiwa wamekusanyika wao sita na wenzao 12 ambao hawapo mahakamani wakiwa katika maandamano au mkusanyiko wenye vurugu na kutozingatia amri ya kuachaa maandamano iliyotolewa na askari, waligoma kutawanyika na kuendelea na mkusanyiko huo wa vurugu uliosababisha kifo cha Akwilina Akwiline na majeraha kwa askari wawili kutokana na mkusanyiko wa vurumai uliosababishwa na wao.

Katika shtaka ambalo linamkabili Heche peke yake, inadaiwa Februari 16 mwaka huu katika Viwanja vya Buibui Kinondoni katika mkutano wa hadhara, alitoa maneno ya chuki dhidi ya Serikali.

Inadaiwa alisema, ‘kesho patachimbika, upumbavu ambao unafanywa kwenye nchi hii.. Wizi unaofanywa na Serikali ya awamu ya tano,  watu wamapotea… Watu wanauawa, wanaokotwa katika mitaro lazima ukome’, maneno ambayo yanaleta chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali.

Washtakiwa  walikana mashitaka na  upande wa Jamhuri  ulidai upelelezi umekamilika na kuomba  kuwasomea washtakiwa hao maelezo ya awali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles