
ABUJA, Nigeria
RAIS wa Nigeria, Muhammadu Buhari, amesema taifa hilo lenye watu wengi zaidi barani Afrika limegeuka na kuwa masikini ghafla.
Shirika la BBC Swahili limekariri Buhari akitoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja baada ya Afrika Kusini kutwaa tena nafasi ya kuwa taifa lenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika.
Akizungumza jana mjini Abuja, Buhari alisema: “Umekuwa mwaka mgumu sana kwa Nigeria. Kabla yetu kuingia madarakani, mafuta yaliuzwa dola za Kimarekani 100 kwa pipa lakini bei hiyo ilishuka hadi dola 37 na sasa ni kati ya dola 40 au dola 45 kwa pipa.
“Ghafla tumekuwa taifa masikini, lakini kujitolea kwetu kuhakikisha uwazi na uwajibikaji kunazuia wananchi kuhisi kwamba kuna upungufu mkubwa katika uchumi,” Alisema Rais Buhari.
Nigeria ilikuwa inashikilia nafasi hiyo kwa miaka miwili mfululizo kutokana na tathmini za wachumi, lakini Afrika Kusini imefanikiwa kuipita baada ya kutumiwa kwa viwango vya sasa vya ubadilishanaji wa fedha dhidi ya dola ya Marekani.
Sarafu ya rand ya Afrika Kusini imeimarika pakubwa ilhali naira ya Nigeria imeshuka kwa kasi ambapo thamani ya uchumi wa Afrika Kusini ni dola za Kimarekani bilioni 301 angali uchumi wa Nigeria ukisalia katika kiwango cha dola za Marekani bilioni 296.