MOSCOW, Urusi
KATIKA hali isiyotarajiwa na wengi, Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amemfukuza kazi mkuu wa majeshi ya nchi hiyo, Sergei Ivanov.
Rais Putin amechukua uamuzi huo jana ikiwa ni siku moja baada ya kufanya kikao cha ndani na wakuu wake wa masuala ya usalama nchini humo.
Kwa mujibu wa BBC, Rais Putin hakueleza sababu zilizomsukuma kuchukua uamuzi huo wa kumtimua mtendaji wake huyo wa muda mrefu.
Baada ya kuondolewa katika cheo hicho cha juu kabisa katika masuala ya usalama wa nchi hiyo, Ivanov (63) anatarajiwa kupewa majukumu mapya ya usimamizi wa masuala ya mazingira na uchukuzi.
Tayari Rais Putin amemteua Anton Vaino (44) kumrithi Ivanov. Kabla ya mabadiliko hayo, Vaino alikuwa naibu katika kitengo hicho.
Juzi Rais Putin alikutana na baraza lake la usalama, ikiwa ni siku moja baada ya kuishutumu Ukraine kwa kuchochea mzozo kwenye eneo linalogombaniwa la Crimea, ambalo Urusi ililitwaa mwaka 2014.
Rais Putin alikutana na maofisa waandamizi wa kijeshi pamoja na maofisa wa kijasusi kwa ajili ya kutathmini upya hatua za kuchukua katika kupambana na ugaidi kwenye eneo la mpaka, bahari na eneo la anga la Crimea.
Baada ya kikao hicho aliahidi kuchukua hatua madhubuti dhidi ya Ukraine, ambayo ameishutumu kwa kupanga mashambulizi ya kigaidi kwenye rasi ya Crimea, tuhuma ambazo zimekanushwa na Ukraine, ikiziita ni za uongo ambazo zinaonekana kama njama ya Urusi kutaka kueneza uhasama zaidi.
“Nadhani ni dhahiri kwamba maofisa wa Ukraine hawatafuti njia za kuyatatua matatizo haya kwa mazungumzo, bali kupitia vitendo vya kigaidi. Suala hili ni la kutisha sana,” alisema Putin.
Hayo yanajiri wakati Wizara ya Ulinzi ya Urusi ikiwa imetangaza kuwa kikosi cha jeshi la majini ambacho kimeweka kambi katika Bahari Nyeusi, Crimea, kitaanza kufanya mazoezi ya kivita kwenye eneo hilo katika kujibu mashambulizi ya kwenye maji yatakayofanywa na wahujumu.
Wakati hayo yanajiri, Rais wa Ukraine, Petro Poroshenko, ameamuru kwamba vitengo vyote vya kijeshi karibu na Crimea na Mashariki mwa Ukraine kuwekwa katika hali ya tahadhari, baada ya idara ya usalama ya Urusi kusema imefaulu kuyazima mashambulizi ya kigaidi ya jeshi la Ukraine katika Bahari Nyeusi wiki hii, shutuma ambazo zimekanushwa na Serikali ya Ukraine.
Rais Poroshenko amesema anatafuta njia ya kufanya mazungumzo ya dharura na Rais Putin pamoja na viongozi wa Ufaransa, Ujerumani, Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden na Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk.
Wakati huo huo, Marekani imezitolea wito Ukraine na Urusi kujiepusha na malumbano kati yao na kuhimiza mazungumzo baina ya pande hizo mbili yaanze tena. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Elizabeth Trudeau, amesema nchi hiyo ina wasiwasi mkubwa na imezitaka nchi hizo kupunguza mvutano.