RIO DE JANEIRO, BRAZIL
TIMU ya taifa ya soka ya Brazil, imefanikiwa kuingia hatua ya nusu fainali katika michuano ya Olimpiki baada ya kuichapa Colombia mabao 2-0.
Brazil ambao ni wenyeji wa michuano hiyo, walikuwa na wakati mgumu katika michezo miwili ya mwanzo ambapo walitoa suluhu dhidi ya Afrika Kusini na Iraq na kuwafanya mashabiki wa timu hiyo kuizomea.
Hata hivyo, waliweza kuutumia vizuri mchezo uliofuata dhidi ya Denmark na kushinda mabao 4-0 na kuwafanya waingie hatua ya robo fainali kabla ya juzi kuichapa Colombia mabao 2-0 na kuingia nusu fainali katika michezo hiyo ya Olimpiki.
Mabao ya nahodha wa timu hiyo, Neymar na Luan Vieira, yalipeleka furaha kwa mashabiki wao ambao walikuwa wakiisema vibaya timu hiyo ya taifa.
Hata hivyo, wenyeji hao wanatarajia kucheza mchezo wa nusu fainali dhidi ya wapinzani wao Honduras keshokutwa.