24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Walipewa nafasi Olimpiki, wamekuwa wa kwanza kuondolewa

Serena_williams_31_3436673b

NA BADI MCHOMOLO,

MICHUANO ya kimataifa ya Olimpiki inaendelea kutimua vumbi jijini Rio de Janeiro nchini Brazil, huku michuano hiyo ikitarajia kufikia tamati mwishoni mwa wiki hii Agosti 21, ambapo itakuwa siku ya Jumapili.

Hadi sasa Marekani inaongoza kwa kukusanya medali nyingi kutokana na wawakilishi wake kufanya vizuri dhidi ya mataifa mengine, hata hivyo inadaiwa kwamba nchini hiyo inafanya vizuri kutokana na idadi kubwa ya washiriki ambao wana uwezo mkubwa.

Kuna mataifa mengine hadi sasa yameshindwa kufanya vizuri na kukosa kabisa tuzo. Hii inatokana na washiriki wake kuwa wachache, hivyo kuwafanya washindane kwenye michezo michache.

Hata hivyo, mbali na mataifa kuonesha ubora wao katika michuano hiyo, kuna baadhi ya wanamichezo walipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kutokana na ubora wao lakini wamekuwa wa kwanza kuyaaga. SPOTIKIKI leo hii imekuchambulia wanamichezo ambao walipewa nafasi lakini wamekuwa wa kwanza kuaga.

Novak Djokovic

Huyo ni bingwa wa michuano ya mchezo wa tenisi kutoka nchini Serbia, anashika nafasi ya kwanza kwa ubora katika mchezo huo duniani kwa upande wa wanaume.

Nyota huyo alipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika michuano hiyo, lakini alishangaza wengi baada ya kuyaaga mashindano hayo ambayo yanafanyika mara moja kwa miaka minne.

Djokovic alikuwa alijikuta akibubujika machozi kwenye raundi ya kwanza kwenye Olimpiki baada ya kushindwa kuonesha ubora wake dhidi ya Juan Martin Del Potro, raia wa nchini Argentina ambaye anashika nafasi ya 141 kwa ubora katika mchezo huo duniani.

Djokovic alipewa nafasi ya kufanya vizuri kutokana kushindwa kufanya hivyo kwenye michuano ya Wimbledon. Hata hivyo baada ya kushindwa kwenye Wimbledon mwezi mmoja uliopita alishindwa kushiriki michuano ya Roger Cup kwa ajili ya kujiandaa na Olimpiki, lakini hata hivyo alifungasha virago mapema kwa kufungwa setti 7-6 (7-4) 7-6 (7-2).

Serena Williams

Huyu ni bingwa mtetezi wa tenisi kwa upande wa wanawake kwenye michuano ya Olimpiki, alifanya vizuri mwaka 2012 jijini London, lakini mwaka huu ameshindwa kutetea ubingwa wake na kujikuta akitolewa mapema kwenye michuano hiyo dhidi ya Elina Sitoniva kutoka nchini Ukraine.

Serena mbali na kuwa bingwa wa mchezo huo mwaka 2012, lakini mwaka huu alionesha uwezo wake kwenye michuano ya Wimbledon na kutwaa ubingwa, lakini kwenye Olimpiki ametolewa mapema.

Nyota huyo alitolewa kwa seti 6-4-6-3 dhidi ya bingwa huyo ambaye anashika nafasi ya 20 kwa ubora wa mchezo huo duniani.

Hata hivyo, mbali na kutolewa kwa mchezaji mmoja mmoja, lakini Serena hakufanya vizuri na dada yake Venus Williams kwenye michuano hiyo huku wakiwa kama timu, ambapo napo walitolewa mapema dhidi ya timu kutoka Jamhuri ya Czech.

Andy Murray
Andy Murray

Andy Murray

Alifanya vizuri kwenye michuano ya Wimbledon mwaka huu na kuchukua taji la michuano hiyo. Kutokana na kile ambacho alikifanya kwenye michuano hiyo kila mmoja alimpa nafasi ya kufanya hivyo kwenye Olimpiki, hasa kutokana na kushika nafasi ya pili kwa ubora duniani.

Hali ilikuwa tofauti na ushindani mkubwa aliokutana nao kwenye michuano hiyo ilimfanya ayaage mapema na kuwaacha wachezaji ambao majina yao sio makubwa kwenye masikio ya watu wakiendelea na michuano hiyo.

Nyota huyo aliingia kama timu na kaka yake Jamie Murray, huku wakiwakilisha England, lakini umoja wao haukuwa na nguvu yoyote na kujikuta wakitolewa mapema katika raundi ya kwanza dhidi ya wapinzani wao kutoka nchini Brazil, Thomaz Bellucci na Andre Sa.

Michuano ya Olimpiki iliwataka washinde kila mchezo ili waweze kusonga mbele kwenye hatua inayofuata, lakini ukipoteza mchezo inakuwa basi unayaaga mashindano na ndicho kilichotokea kwa nyota huyo na kaka yake ambapo walishindwa kutamba mbele ya bingwa wa mchezo huo ambaye anashika nafasi ya 55 kwa ubora duniani, Bellucci na Andre Sa, ambaye anashika nafasi ya 60 kwa ubora duniani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles