24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Bosi Clasic Mall, wenzake kortini kwa kuisabishia hasara serikali

NA KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imemfikisha mahakamani Meneja wa Kampuni ya Clasic Mall, Vardan Mkhitaryan na mwenzake kwa mashtaka saba ikiwemo kufanya udanganyifu  katika mawasiliano ya kimataifa na kusababisha hasara ya Sh milioni 44.5.

Washtakiwa hao  Mkhitaryan (47) ambaye ni Property Manager na  Rosemary Mwemezi (32) ambaye ni mlinzi  walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustino Mmbando.

Akisoma mashtaka Wakili wa Serikali, Jackline Nyantori alidai shtaka la kwanza linawakabili washtakiwa wote ambapo wanadai kula njama kutenda kosa.

Inadaiwa katika tarehe tofauti Dar es Salaam, kati ya Oktoba mosi mwaka 2019 na Mei 28 mwaka huu walitenda kosa la kufanya udanganyifu katika mawasiliano.

Shtaka la pili linamkabili mshtakiwa Mkhitaryan, anadaiwa kati ya Oktoba mosi na 30 mwaka jana jijini Dar es Salaam, kinyume cha sheria aliingiza vifaa vya Mawasiliano vya kielektroniki vya Airtel vyenye namba G9W9K14A18000539 yenye IMEI namba 3574800040402060 na kuunganisha katika kadi za simu za Airtel bila kuwa na leseni ya TCRA.

Nyantori alidai shtaka la tatu linamkabili huyo mshtakiwa wa kwanza ambapo anadai katika kipindi hicho maeneo ya Mbezi Beach alisimika vifaa hivyo na kuviunganisha kwenye kadi za simu za Airtel bila kuwa na leseni.

Mshtakiwa huyo anashtakiwa katika shtaka la nne kwa kundesha Mawasiliano bila leseni na katika shtaka la tano washtakiwa wote wanadaiwa kati ya Oktoba 10 mwaka 2019 na Mei 28 mwaka huu, kwa lengo la kukwepa kulipa malipo halali alipokea na aliruhusu simu za kimataifa kwa ulaghai.

Shtaka la sita linamkabili mshtakiwa wa kwanza ambapo anadaiwa kutumia vifaa hivyo kufanya Mawasiliano bila ridhaa ya TCRA .

Nyantori alidai shtaka la saba kwa washtakiwa wote wanadaiwa kati ya Oktoba 10 mwaka 2019 na Mei 28 mwaka huu, huku wakijua waliisababishia Mamlaka na Serikali hasara ya Sh 44552,175.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, mshtakiwa karudishwa rumande na kesi iliahirishwa hadi Juni 18 mwaka huu kwa kutajwa.

Mshtakiwa katika kesi hiyo anawakilishwa na Wakili Steven Bwana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles