SMZ yafanikisha sheria kulinda wazee

0
535

Na MWANDISHI WETU – ZANZIBAR

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imefanikisha sheria ya kuwalinda wazee.

Sheria hiyo inatoa fursa ya kuboresha hali ya wazee visiwani humo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwanachama wa Jumuiya ya Wazee na Wastaafu Zanzibar (JUWAZA), Ghanima Othman alisema sheria hiyo inafanya utoaji wa pensheni jamii visiwani humo kuwa haki ya msingi kwa wazee.

“Hii ni habari nzuri kwetu wazee wa Zanzibar ina maana sasa tuna uhakika wa kupata pensheni jamii, huduma bure za afya pamoja na mambo mengine mengi. Maisha ya wazee Zanzibar sasa yanakwenda kubadilika kwa sababu ya sheria hii,”alisema Othman.

Alisema wanaishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa hatua madhubuti inazochukua katika kulinda na kuhakikisha ustawi wa wazee unafikiwa Zanzibar.

“Ni miaka minne tu tangu kuanza kutoa pensheni jamii miongoni mwa wazee Zanzibar na tayari imepatikana sheria ambayo pamoja na mambo mengine ina hakikishia wazee kupata pensheni jamii,” alisema

Naye, Mkurugenzi wa Shirika la Help Age International, Smart Daniel alisema Desemba mwaka jana serikali ya Zanzibar iliandaa kongamano na kutoa ripoti ya utafiti wa manufaa ya utoaji pensheni visiwani humo.

Alisema ripoti hiyo ilionesha kuwa hata kwa pensheni inayotolewa, maisha ya wazee yameweza kuboreshwa.

“Kwa sheria hii ni dhahiri kuwa wazee wenye umri wa miaka 70 na kuendelea wana uhakika wakupata pensheni nawataweza kudai haki hiyo iwapo mzee atashindwa kupatiwa pensheni,”  alisema Daniel.

Alisema Sheria hiyo inawapa wazee haki ya kuweza kushiriki katika ngazi za maamuzi ya masuala yanayowahusu, kulinda wazee  dhidi ya ubaguzi na unyanyaswaji, haki ya kupata taarifa sahihi zinazowahusu, na wajibu wa wanafamilia kuwatunza na kuwapatia mahitaji muhimu wazee.

Alisema hadi mwaka jana zaidi ya wazee 27,000 wamekuwa wakipokea pensheni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here