28.2 C
Dar es Salaam
Monday, July 4, 2022

Bodi taasisi 100 za dini, siasa hatarini kufutwa

Na ASHA BANI -DAR ES SALAAM

WAKALA wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) umezitaka bodi za wadhamini wa taasisi zaidi ya 100 ambazo hazijafanya marejesho ya wadhamini hadi kufikia Juni, mwaka huu kufanya hivyo mara moja kabla ya

hatua kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kuzifuta.

Miongoni mwa taasisi hizo ni vyama vya siasa, taasisi za kidini na mashirika mengine.

Kaimu Kabidhi Mkuu wa RITA, Emmy Hudson alivitaja baadhi ya vyama vya siasa ambavyo havijafanya marejesho ya wadhamini kuwa ni pamoja na Chama cha Democratic (DP), United Democratic Party (UDP) Chama cha Sauti ya Umma (SAU) na Tanzania Labour Party (TLP).

Alizitaja baadhi ya taasisi za dini ni pamoja na Kanisa Kanisa la Katoliki Mtakatifu Benedict la Peramiho, Kanisa la Katoliki Dayosisi ya Mtwara, Masjid Pazi, Masjid Nur na Msikiti wa Mbagala Kizinga zpte za Dar es Salaam.

 “RITA inaendelea na uhakiki wa kina wa bodi za taasisi zote zilizosajiliwa chini ya Sheria ya Usajili wa Wadhamini  Sura ya 318, lengo likiwa kufahamu hali ya kila taasisi kama zinatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na katiba za taasisi husika,’’ alisema Emmy.

Alisema wakati uhakiki ukiendelea, bodi za taasisi hizo zinatakiwa kuwasiliana na wakala ili kuhakiki taarifa zao.

Pia alisema kwa upande wao tayari wameanza kuzitembelea ofisi za taasisi hizo.

“Muunganisho wa wadhamini ni utaratibu unaohusisha usajili wa wadhamini ambao huwezesha wadhamini waliounganishwa (trustees incorporation) kuwa na utu wa kisheria, kuweza kushtaki au kushtakiwa kwa majina yao, kumiliki na kuuza mali na kuingia mikataba kwa niaba ya taasisi hizo.

“Mfumo huu wa muunganisho wa wadhamini unaongozwa na Sheria ya Usajili wa Wadhamini, Sura ya 318 Toleo la 2002. (The Trustees’ Incorporation Act, CAP 318 R.E.2002),” alisema Emmy.

Alisema wakala huo ni taasisi ya Serikali yenye dhamana ya kusajili na kusimamia utendaji kazi wa bodi za wadhamini wa taasisi ambazo zina dhamana kubwa ya kusimamia mali za taasisi husika kwa uadilifu na weledi.

“Ijulikane kwamba wadhamini wa taasisi wanawajibika kisheria kama mdhamini mmoja mmoja au kwa pamoja endapo uzembe au ubadhirifu utajitokeza katika utendaji wake wa kazi.

“Tunatoa rai kwa bodi za wadhamini kuzingatia sheria ya usajili wa wadhamini, ikiwemo kutoa taarifa mara mabadiliko yanapotokea na kuleta marejesho ya kila mwaka,” alisema Emmy.

Alisema kwa mujibu wa sheria, bodi ambazo hazitekelezi majukumu yake kikamilifu zinatakiwa kufutwa katika daftari la msimamizi mkuu wa wadhamini na zitapaswa kurejesha mara moja hati za usajili (Certificate of Incorporation)  kwa Kabidhi Wasii Mkuu kulingana na kifungu cha 23(4) cha Sheria ya Usajili wa Wadhamini.

Emmy alisema mali za taasisi, asasi hizo zinaweza kuwekwa chini ya usimamizi wa mdhamini wa umma, endapo kutakuwa na ombwe la wadhamini hadi hapo utaratibu mwingine utakapotolewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
195,637FollowersFollow
545,000SubscribersSubscribe

Latest Articles