25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Hospitali ya Rufaa Kumbukumbu ya Nyerere itunzwe

HISTORIA imeandikwa. Ndilo neno ambalo unaweza kusema baada ya Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere mjini Musoma kuanza kutoa huduma mbalimbali kwa wagonjwa ikiwa ni miaka karibu 46 imepita tangu kuanza kujengwa.

Tunasema historia imeandikwa kwa sababu ujenzi wa hospitali hiyo ulikuwa ndoto kukamilika tangu mwaka 1976, wakati Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julisu Nyerere alipouasisi.

Wazo la Mwalimu Nyerere limetimia juzi, baada ya hospitali kuanza kutoa huduma zake mbalimbali kwa wagonjwa. Hii ni taarifa nzuri ikizingatiwa kuwa kutokana na ukubwa wa hospitali hiyo, itahudumia karibu mikoa yote ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani ya Kenya.

Tunasema hivi kwa sababu wagonjwa wengi walikuwa wakilazimika kusafiri umbali wa kilometa 270 kwenda Bugando, Mwanza ili kupata matibabu ya uhakika, sasa adha hii imepungua kwa kiasi kikubwa.

Lakini pia, wananchi wengi walilazimika kusafiri hadi Dar es Salaam kupata tiba za magonjwa kama satarani na mengine mengi.

Kukamilika kwa ujenzi wa hospitali hii ni heshima kwa uamuzi uliochukuliwa na Rais Dk. John Magufuli wa kuhakikisha ndoto ya Mwalimu Nyerere inatimia. Tunalisema hili kwa sababu hapo katikati wamepita viongozi wakuu wa nchi watatu, lakini ujenzi ukabaki historia tu.

Tunaupongeza uongozi wa mkoa, chini ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Carolina Mthapula kwa usimamizi na ufuatiliaji makini ambao umekuwa ukifanywa na ofisi yake tangu Rais Magufuli alipoamua kujenga hospitali hiyo.

Usimamizi wa aina hii ndiyo unatakiwa kwenye miradi mikubwa, mambo ya blaablaa hayapaswi kupewa nafasi. Kile kinachoagizwa na mkuu wa nchi kinapaswa kusimamiwa na kuonekana mbele ya wananchi.

Mradi huu umetumia zaidi ya Sh bilioni 15 hadi  kukamilisha.

Uongozi wa mkoa unapaswa kupongezwa kwa kusimama kidete kusimamia wakandarasi  na washauri elekezi ambao wakati fulani walikuwa wakisota.

Ni wazi miaka yote hii wananchi wa mkoa huu walikuwa wamekata tamaa kuhusu kukamilika kwa hospitali hii, lakini sasa wanafurahi matunda mazuri ya Serikali ambayo iliamua kuuvalia njuga.

 Moja ya matunda ambayo yanategemewa kuwapo ndani ya hospitali hii, ni vitengo vya mama na mtoto  na hospitali ya rufaa ya mkoa, kutakuwapo  kitengo cha matibabu  bingwa ya mifupa na viungo na kwamba hospitali hiyo inatarajiwa kuwa na hadhi ya hospitali ya kanda.

Lakini pia huduma za matibabu ya figo zinatarajiwa kuanza muda wowote ndani ya wiki hii baada ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  kupeleka vifaa kwa ajili ya kusafisha na kutibu figo vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 300.

Sisi MTANZANIA tunasema uongozi wa mkoa sasa una haki ya kuhakikisha hospitali inatunzwa kwa gharama zote. Kuhakikisha kunakuwapo na wataalamu wa fani zote na vifaa.

Tunasisitiza hili kwa sababu wananchi wataokoa gharama kubwa ya fedha kwenda mikoa mingine kutafuta matatibu. Kama wameweza kuvumilia miaka 46, sasa ni wakati wao wa kupata tiba za uhakika.

Tunaamini mganga mkuu wa mkoa na timu yake wamejipanga vema  kutoa huduma na kulinda rasilimali zote ambazo zinawekezwa hapo kwa mamilioni ya fedha.

Tunamalizia kwa kuwaasa wananchi wa Mkoa wa Mara, mikoa ya jirani na nchi jirani kutumia hospitali hii kikamilifu kupata matatibu, badala ya kusafiri kwenda mbali kama ilivyokuwa zamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles