23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Benki zatakiwa kutoa huduma za bima

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

TAASISI za fedha nchini zikiwamo benki, zimetakiwa kugeukia na kuangalia namna bora ya kutoa huduma za bima zote, ikiwamo za afya kama ilivyofanya Benki ya NMB.

Hatua hiyo imetokana na NMB kuzindua rasmi huduma ya bima ya Bancassurance itakayotolewa katika matawi yote 224 ya benki hiyo nchini.

Akizungumza juzi Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo, Kamishna wa Bima wa Mamlaka ya Bima nchini (Tira), Dk. Mussa Juma alisema Serikali kupitia taasisi yake inachukua juhudi mbalimbali kukuza sekta ndogo ya bima nchini ili mchango wake katika pato la taifa ufikie asilimia tatu ifikapo mwaka 2023.

Dk. Juma alisema hivi sasa sekta ndogo ya bima zinazosimamiwa na Tira, huchangia asilimia 0.7 ya pato la taifa.

“Malengo yetu ni kuhakikisha kuwa asilimia 60 ya Watanzania watu wazima wawe wanapata huduma za bima ifikapo mwaka 2024. 

“Tunalenga pia kuhakikisha kuwa asilimia 60 ya Watanzania wote wawe wameweza kuelewa umuhimu wa bima ifikapo mwaka 2024,” alisema Dk. Juma.

Alisema kuwa ili kufikia azma hiyo, kampuni za bima, madalali wa bima, mawakala wa bima na benki zinazotoa huduma za bima zitalazimika kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa Watanzania ili wapate kuelewa umuhimu wa kuziwekea bima mali zao.

Dk. Juma alisema wadau wa bima watalazimika kutumia teknolojia mpya ili kuwafikia watu wengi zaidi, wakiwemo wafanyabiashara ndogo ndogo na baba na mama lishe.

Awali akizungumza katika uzinduzi huo, Meneja Mwandamizi wa Bima wa NMB, Martin Massawe, alisema uwepo wa matawi ya benki yake katika wilaya zote nchini kutasaidia kukuza sekta ndogo ya bima na kuinua mchango wake katika pato la taifa.

“Tulipata leseni ya kutoa huduma za bima mara baada ya kupitishwa kwa kanuni za Bancassurance mwaka jana. Kutokana na kupatikana kwa matawi ya NMB katika wilaya zote nchini, tunaamini kupatikana kwa huduma za bima katika matawi yetu kutasaidia kukuza sekta ndogo ya bima,” alisema Massawe.

Naye Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi, Biashara Ndogo na za Kati wa NMB, Filbert Mponzi alisema benki hiyo imeshatoa elimu ya bima kwa wafanyakazi wake wapatao 200 ambao wamethibitishwa kumudu utoaji wa huduma za bima kwa wateja.

“Tunaamini ujio wa Benki ya NMB katika kutoa huduma za bima ni ‘game changer’ (itabadili mwenendo wa sekta) na kuipeleka katika viwango vya juu,” alisema Mponzi.

Alisema NMB itatumia uwepo wa klabu za kibiashara katika maeneo mbalimbali nchini ili kueneza ujumbe wa umuhimu wa bima.

Huduma za bima zitakazopatikana katika matawi ya NMB ni pamoja na zile za kampuni za Sanlam Life, UAP, Shirika la Bima la Taifa (NIC), Jubilee, Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC) na Reliance.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles