23.9 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Bashe: Wakulima kunufaika bei ya nafaka

TUNU NASSOR – DAR ES SALAAM

NAIBU Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema wakulima wameanza kunufaika na kupanda kwa bei za nafaka baada kuruhusiwa kufanya biashara ya mazao.

Bashe alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa swali na mwandishi kuhusu kauli ya Waziri wa wizara hiyo Japhet Hasunga ya kuruhusu kuuzwa nafaka nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa wizara hiyo na wafanyabiashara wa nafaka ndani na nje ya nchi, Bashe alisema mpaka sasa mahindi mkoni Rukwa yamefikia Sh 600 kwa kilo moja.

Alisema hapo awali majindi katika mkoa huo yaliuzwa kati ya Sh 150 na 200 kwa kilo jambo lililowapa hasara wakulima.

“Kwa sasa nitamshangaa mkulima atakayeuza mahindi yake chini ya Shilingi 600 kwa kuwa bei inaendelea kupaa,” alisema Bashe.

Aliongeza kuwa anawashauri wakulima kuendelea kuyatunza mazao hayo hadi Desemba mwaka huu kwa kuwa anaamini kuwa bei itaongezeka na kufikia 1,000.

“Hatuwezi kuzuia wananchi kuuza mazao yao nje ya nchi kwa kuwa wizara tunaamini kuwa kilimo ni biashara,” alisema Bashe.

Bashe alisema mkulima hulima yeye na familia yake lakini anapovuna hakuna sababu ya mazao yake kuwa mali ya umma.

“Mkulima anapopata hasara hakuna sekta nyingine inayojitokeza kumsaidia kuondosha hasara aliyoipata,” alisema Bashe.

Alisema wizara hiyo imeanzisha kanzidata ambayo itasaidia kufanya kujua idadi ya wakulima, ukubwa wa maeneo wanayofanyia shughuli za kilimo na kiwango cha mazao wanayopata.

Awali Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, alisema wizara hiyo inaipitia upya sera ya kilimo ya mwaka 2015 ili kuiboresha na kwenda na wakati na  kukidhi mahitaji ya wadau.

“Sera hii imekuwa ikitumika bila kuwa na sheria hivyo tunatarajia kuwasilisha mswada wa sheria ya kilimo itakayotuongoza namna bora ya kusimamia kilimo,” alisema Hasunga.

Alisema athari kubwa anayoiona katika sekta hiyo ni ardhi iliyotengwa kwa ajili ya kilimo kubadilishwa matumizi na kuwa ya makazi hivyo itawekwa katika sheria kuwa ardi ya kilimo isitendelezwe kwa makazi.

Akizungumzia hali ya chakula nchini Hasubga alisema nchi inajitoshereza kwa chakula kwa asilimia 119.

“Mikoa inayoongoza kwa wingi wa chakula ni Ruvuma ina asilimia 227 ya chakula na kufuatiwa na Rukwa asilimia 220 na Songwe asilimia 200 huku Dar es Salaam ikiwa ya mwisho kwa asilimia tatu,” alisema Hasunga.

Aliongeza kuwa Tanzania ina hekta milioni 44 ambapo hekta milioni 29 zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji lakini hekta 475 pekee ndio zinafanya kilimo cha umwagiliaji.

“Hii ni fursa kwa sekta binafsi kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji  na kuongeza tija ya kilimo hapa nchini,” alisema Hasunga.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi nyumba na  Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula aliwaagiza watumishi wa mipango miji wanapopanga matumizi ya ardhi wakumbuke kutenga maeneo ya kilimo.

“Tunahitaji kilimo kiendelee kwa ajili ya malighafi za viwanda pamoja na kuuza chakula katika soko tulilopata la Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika(SADC),” alisema Mabula.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles