28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

Baraza la Ujenzi la Taifa laridhishwa na kasi ya ujenzi mradi wa Nyerere

Na Mwandishi Wetu, Pwani

Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), imeridhishwa na kasi ya ujenzi wa Mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere huku ikimpongeza, Rais Dk. John Magufuli kwa kuvalia njuga mradi huo na kuhakikisha unatekelezeka kipindi hiki ambacho nchi inajitayarisha kwa ajili ya maendeleo ya viwanda.

Aidha, imesema ni hatua nzuri katika wakati huu ambapo Tanzania inajenga Reli ya Kisasa (SGR) maeneo ambayo umeme utahitajika sana.

Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NCC, Prof. Mayunga Nkunya alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye ziara wa wajumbe wa bodi na Menejimenti ya NCC iliyotembelea mradi, mkoani Pwani.

Amesema wazo la ujenzi wa mradi huo lilikuwepo siku nyingi, isipokuwa watu walikuwa wanaogopa watawezaje, lakini Rais Dk. Magufuli ameweza.

“Kwa kweli tunamshukuru sana Rais Dk. Magufuli, ili wazo amelivalia njuga na mradi huu unatekelezeka sasa. Waliomtangulia walikuwa wanafikiria huu mradi hautekelezeki kwa sababu ya gharama na mengineyo, lakini unatekelezeka na ni muhimu kwa taifa letu,” amesema Prof. Nkunya.

Aidha, ameongeza kuwa; “Kwa hiyo tunamshukuru sana rais kwa kufanya uamuzi mgumu wa kuweza kujenga mradi huu wakati huu ambapo tunajitayarisha kwa ajili ya maendeleo ya viwanda na tunajenga reli ya SGR ambapo umeme utahitajika sana, kwa hiyo kuwa na mradi kama huu ni kitu bora sana kwa maendeleo ya taifa,” amesema Prof. Mkunya.

Amefafanua kuwa wamejionea utaalam wa hali ya juu wa ujenzi wa mradi huo mkubwa na ambao una miradi midogo midogo 10.

“Kizuri zaidi ambacho kimetufurahisha ni wafanyakazi wengi ambao ni wataalam ni Watanzania na wale waliokuwa wakitupa maelezo kila tulipokuwa tunauliza maswali wanatujibu kwa ufasaha na ni Watanzania,” aamesema Prof. Nkunya.

Amesema pamoja na mradi huo kutusaidia kuzalisha umeme wa kutosha, lakini pia umesaidia kujenga uwezo wa Watanzania wa kuwawezesha kutekeleza miradi mingine kwa miaka mingine ijayo, kwa sababu wataalam wamepatikana kupitia mradi huo.

Aidha, amepongeza mkandarasi mkubwa katika mradi huo na washirika wake kwa kuweza kusaidia kuwajengea uwezo Watanzania kupitia ujenzi wa bwawa hilo.

Kuhusu lengo la ziara yao, Prof. Nkunya amesema wao kama NCC walienda kuona mradi upo namna gani kwa sababu huo ni mradi wa kipekee, hivyo ilikuwa fursa kwao kujifunza ili miradi mingine ikitokea namna hiyo, wao kama wasimamizi wa sekta ya ujenzi wajue itatekelezwa namna gani.

“Lakini pia mradi huu ni mgeni, una vitu vipya na sisi kama Baraza la Ujenzi kati ya vitu ambavyo tunafanya ni kuweka viwango ambavyo vitaweza kutusaidia katika miradi kama hii baadaye,” amesema Prof. Nkunya.

Amesema utaalam unaotumika kwenye mradi huo wao kama NCC utawasaidia sana.

Kuhusu kitu walichojifunza katika ziara yao hiyo, Prof. Nkunya amesema; “Tumejifunza kuwa kwenye mradi mkubwa kama huu unahitaji wataalam mbalimbali, hapa kuna kampuni mbili za Misri, lakini kuna wakandarasi wasaidizi kutoka China, swahili wenzetu na wengine, kwa hiyo tumejifunza mradi mkubwa kama huu hauwezi kutekelezwa na kampuni moja.

“Tumejionea kazi ambazo zinavyokwenda, zinakwenda kwa uhakika na kweli mwaka kesho tutapata umeme,” amesema Prof. Nkunya.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa NCC, Dk. Matiko Mturi, akifafanua kuhusiana na ziara yao, amesema mradi huo ni wa kihistoria, moja kwa sababu ya kuchukua maamuzi magumu kutekeleza miradi ambayo ilikuwa inafikiliwa wakati tunaanza kupata Uhuru ambayo nia yake ilikuwa ni kujenga maendeleo ya nchi.

“Kwa hiyo maamuzi yaliyofanywa ni mawazo ambayo yalikuwepo tangu tunapata Uhuru, pili ukiambiwa tu hauwezi kuelewa ukubwa wa mradi huu na hauwezi kujua nini kinaendelea, kwa hiyo Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Menejimeti tuliamua kuja kwanza kuona ukubwa wa kazi hiyo, nini kinahusika lakini pia kuangalia maendeleo yaliyofikiwa.

“Tusisitize kwamba tumeona juhudi kubwa ya kuwawezesha Watanzania kutekeleza miradi yao wenyewe, sasa hivi na huko mbele. Na kikubwa tumeona taswira ya miradi inayotegemewa katika sekta ya ujenzi. Tulizoea miradi midogo midogo, lakini kwa miaka ya hivi karibuni tumeanza kuona miradi mikubwa ambayo kwa kiasi kikubwa sana inahitaji umakini sana katika kuitekeleza,” amesema Dk. Mturi.

Aidha, ametolea mfano mradi huo wa Nyerere, mradi wa SGR na mingine mingine yote inayoonesha mabadiliko ya aina ya miradi inayokuja.

Ametaja jambo lingine ambalo walienda kuona kwenye mradi huo kuwa ni namna ya ushiriki wa watu wa kawaida, kwani mradi huo unawezesha watu wengine wa kawaida.

“Kwa hiyo kwa kiasi kikubwa sisi tulichokiona ni nanna maamuzi mazito yanayofanywa na Serikali yanavyoweza kubadilisha taswira na mategemeo ya Watanzania na muhimu zaidi ni namna ya Watanzania wenyewe wanavyohusika kwa kiasi kikubwa cha weledi katika utekelezaji wa mradi huo,”amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles