23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Bandari Mtwara na fursa kiuchumi Kusini, nchi jirani

ASHA BANI, aliyekuwa MTWARA

BANDARI ya Mtwara ni mojawapo kati ya bandari kuu tatu za mwambao wa bahari zilizopo nchini, zinazosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa
Bandari Tanzania (TPA).

Uwezo wa bandari hiyo kwa sasa ni kuhudumia kwa usalama meli zenye
urefu wa mita 222 na kina cha maji kisichozidi  mita 9.5 katika gati
yenye urefu wa mita 385.

Akiizungumzia bandari hiyo, Meneja wa wake, Mhandisi Juma Kijavara,
wakati akitoa taarifa ya utendaji wa kazi, anasema huwa inatumika katika kufanikisha biashara kwa bidhaa zitokanazo nchini kwenda nchi za nje ikiwamo Msumbiji, Comoro, India na Vietnam.

Anasema imekuwa ikihudumia zaidi shehena ya korosho
ambayo ni zao kuu la biashara kwa mikoa ya Kusini.

“Bandari hii inahudumia pia shehena za saruji, bidhaa za vyakula, mitambo kwa ajili ya miradi mbalimbali pamoja na shehena ya majimaji
ikiwamo kemikali na mafuta. Sambamba na huduma hizi pia imekuwa
msimamizi wa bandari za Lindi na Kilwa,’’ anasema Kijavara.

Anasema katika kipindi cha mwaka 2017/2018 na 2018 /2019 shehena  iliyohudumiwa ni tani 106,170 ambazo ni pungufu kwa asilimia 71 ya 363,287 tani zilizohudumiwa kwa mwaka 2017/2018.

“Kupungua kwa shehena iliyohudumiwa kulitokana na kutosafirisha
shehena ya korosho pamoja na makaa ya mawe kama ilivyokuwa katika
matarajio ya bandari.

Meneja wa Bandari ya Mtwara, Mhandisi Juma Kijavara.

Mhandisi Kijavara anasema kuwa katika kipindi cha mwaka 2018/2019
idadi ya meli zilizohudumiwa katika bandari hiyo zilikuwa 141
ikilinganishwa na meli 66 zilizohudumiwa mwaka wa fedha 2017 na 2018
ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 113 na kwamba hiyo imetokana na kuongezeka kwa meli za mwambao.

Anabainisha kuwa kuna miradi mbalimbali ya maendeleo inayofanyika
katika bandari hiyo ikiwamo mpango wa ununuzi wa vifaa vya
utekelezaji, ujenzi wa miundombinu ya bandari kwa kuzingatia mpango
mkuu na mpango mkakati wa mamlaka.

Pia aligusia miradi ya maendeleo ikiwamo mpango wa ununuzi wa vifaa vya utekelezaji, ujenzi wa miundombinu ya bandari
kwa kuzingatia mpango mkuu na mpango mkakati wa mamlaka.

Anasema serikali ina mpango wa kupanua Bandari ya Mtwara kwa
kujenga gati nne mpya na kuifanya kuwa ya kisasa kwa ajili ya
kuhudumia shehena ya gesi, mafuta na mazao ya kilimo ukanda wa
maendeleo wa Mtwara unaojumuisha mikoa iliyopo kusini na nchi jirani
za Malawi, Zambia na Msumbiji.


“Awamu ya kwanza ya utekelezaji inahusisha ujenzi wa gati la urefu wa
mita 300 la kuhudumia shehena mchanganyiko, ambapo mkataba kati ya TPA na mkandarasi ambaye ni muunganiko wa kampuni M/s China Rwailway Construction Engeneering Group (CRCEG) na M/S China Railway Major Bridge Engeneering Group (CRMBEG) za nchini China.

“Mradi huu ulisainiwa Machi 4 mwaka 2017; ujenzi wa gati hili
unatarajiwa kukamilika Machi 2020 na hadi sasa kazi ya usanifu
imekamilika na kazi ya ujenzi inaendelea na imefikia asilimia
55,’’ anaeleza Mhandisi Kijavara.

Anasema mradi huu ukikamilika utaiwezesha Bandari ya Mtwara kuhudumia shehena nyingi zaidi takribani tani milioni moja.

Anataja mradi mwingine kuwa ni wa mita ya kupima mafuta unaotekelezwa chini ya ofisi ya Rais, unaofanywa na mkandarasi M/s Endress+Hauser ya nchini Uswizi akishirikiana na kampuni ya kizalendo ya BQ Constractors Ltd, kwa ujenzi wa ‘flow meters’ za Mtwara, Dar es Salaam na Tanga kwa
thamani ya Euro milioni 17.

Anasema kwa upande wa Bandari ya Mtwara, mradi utahusisha ujenzi wa
‘skid’ mbili pamoja na ‘control room’ kwa ajili kupima mafuta ya
diseli na petroli.

Anasema mradi ukikamilika utakuwa umeiwezesha bandari kutekeleza
maelekezo ya serikali na itakuwa na uwezo wa kupima mafuta halisi
yanayopitia bandari hiyo.

Akizungumzia bandari ndogo ya Kilwa, Lindi, Rushungi na Kisiwa/Mgao,
anasema kumefanyika upembuzi yakinifu  na uandaaji wa michoro ya awali kwa ajili ya uendelezwaji wake.

Anasema mamlaka inakusudia kufanya uwekezaji mkubwa wa upanuzi wa
bandari za Lindi, Kilwa na Kisiwa/Mgao, mradi ulioanza August 2019
na muda wa mradi ni miezi 18 hivyo, unategemewa kukamilika Februari
2021 kwa thamani ya Sh milioni 732.392.

“Mradi huu ukikamilika utaifanya mamlaka kuwa tayari kuhudumia mizigo ambayo inatokana na utekelezaji wa mipango ya serikali wa kujenga kiwanda cha mbolea Kilwa pamoja na usafirishaji wa mizigo mbalimbali ya uvuvi wa kibiashara, kilimo na viwandani,’’

Anaeleza kuwa kwa kipindi kirefu bandari hiyo imekuwa ikitegemea shehena ya zao la korosho hivyo kufanya kuwa ya msimu, kutokana na changamoto hiyo bandari imefanya  juhudi ya kupata shehena.

“Mamlaka ya bandari imempa punguzo la bei ya usafirishaji Kampuni ya
Dangote, kwa ajili ya kusafirisha shehena ya saruji na makubaliano ni
kusafirisha shehena tani 120,000 kwa mwezi.

“Pia mamlaka imeingia makubaliano na Kampuni ya Market Insight kwa
ajili ya kusafirisha makaa ya mawe kutoka Mkoa wa Ruvuma kupitia
Bandari ya Mtwara kwenda masoko ya nje na matarajio ni kusafirisha
tani 70,000 za shehena ya makaa ya mawe kwa mwezi pindi
usafirishaji huo utakapoanza,’’ anasema Mhandisi Kijavara.

Pia alizungumzia suala la mafanikio ya kiulinzi na usalama katika
bandari hiyo, ambapo anabainisha kuwa wameingia katika mfumo wa ulinzi wa meli na bandari kimataifa (ISPS CODE COMPLIANCE) mwaka  2013.

Anasema mara baada ya kuingia katika mfumo huo bandari ilianza kufuata kanuni za kiulinzi zinazotambuliwa kimataifa hivyo, kuwezesha ulinzi kuimarika na kupata mafanikio yaliyopo sasa.

“Kutokana na mafanikio hayo, Bandari ya Mtwara ni miongoni mwa
zilizofanya vizuri kiulinzi pamoja na kuwa eneo lenye changamoto ya
kiusalama mpakani mwa nchi ya Msumbiji,’’ anasema Mhandisi Kijavara.

Kuhusu urasimishaji wa bandari bubu, Ofisa Manunuzi na Ugavi wa Bandari ya Mtwara, Abdilah Salim, anasema bandari hiyo imefanikiwa kuzitembelea na kuzitambua bandari 59 zilizopo katika pwani ya Mkoa wa Lindi na bandari 11 zilizopo katika Mkoa wa Mtwara.

Anasema tayari mapendekezo yamewasilishwa makao makuu kwa ajili ya
hatua za kuzirasimisha bandari bubu za Mbuyuni, Kilwa Kivinje, Mchinga
II, Songosongo na Rushungi, Mikindani, Kisiwa, Msimbati, Kilambo na
Litembe Pwani.

Salim anasema kurasimishwa kwa bandari hizo kutasaidia kuweka uwiano
sawa kati ya wafanyabiashara wanaotumia bandari kuu ambao wanalipa
kodi na wale walio katika bandari bubu ambao hawalipi kodi inavyotakiwa na kuiingizia nchi hasara kwa kukosa mapato.

Anasema kuna hasara mbalimbali zinazotokana na kutumia bandari bubu
ikiwa ni pamoja na kuwa njia za maambukizi ya maradhi kutoka eneo la nchi jirani na kuingia nchini, pia kuwa sehemu ya kupitisha dawa za
kulevya na hata bidhaa feki, jambo ambalo linaendelea kutafutiwa ufumbuzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles