24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

BAHATI YAO

ZAINAB IDD – DAR ES SALAAM

TIMU ya Simba na Yanga zimefungana mabao 2-2, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara,  uliochezwa jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba ilikuwa ya kwanza kujipatia mabao yake kupitia kwa Meddie Kagere aliyefunga kwa mkwaju wa penalti dakika ya 42 kabla ya Deo Kanda kufunga bao la pili  dakika ya 46.

Yanga ilisawazisha kupitia kwa Mapinduzi Balama dakika ya 50 na Mohammed Issa ‘Banka’ dakika ya 53.

Sare hiyo inaifanya Simba kuendelea kukalia usukani wa ligi hiyo, ikifikisha pointi 35, baada ya kucheza michezo 14, ikishinda 10, sare tatu na kupoteza mmoja.

Yanga baada ya sare hiyo imefikisha pointi 25 na kupanda juu ya msimamo wa ligi hiyo, ikitoka nafasi ya tano hadi ya nafasi nne.

Mchezo wa jana uliwarejesha wapenzi na mashabiki wa timu hizo kile kilichotokea Oktoba 20, 2013, Uwanja wa Taifa.

Siku hiyo, mchezo kati ya timu hizo ulimalizika kwa sare  ya mabao 3-3.

Yanga hadi kipindi cha kwanza kinamalizika ilikuwa mbele kwa mabao matatu lakini Simba ilitoka nyuma na kusawazisha.

Mchezo ulianza kwa kasi huku Simba ikimiliki zaidi mpira na kusukuma mashambulizi kuelekea lango la Yanga.

Dakika ya 15, Mlinda mlango wa Yanga, Farouk Shikalo alifanya kazi ya ziada kupangua mchomo wa Mzamiru Yassin na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.a

Dakika ya 30, Papy Tshishimbi alipoteza nafasi ya kuindikia Yanga bao, baada ya kupokea pasi safi ya Ditram Nchimbi, lakini shuti lake lilitua mikononi mwa mlinda mlango wa Simba, Aishi Manula.

Dakika ya 42, Kagere aliindikia Simba bao la kwanza kwa mkwaju wa penalti.

Mwamuzi Jonisia Rukyaa aliizawadi Simba penalti hiyo, baada ya beki wa Yanga, Kelvin Yondan kumwangusha Kagere wakati anaenda kuleta madhara langoni mwake.

Hata hivyo, wachezaji wa Yanga walionekana kutoridhika na uamuzi wa Jonisia kuwapa Simba penalti hiyo.

Sakata hilo lilisababisha beki wa kulia wa Yanga, Juma Abdul kulimwa kadi ya njano.

Dakika ya 44, Tshishimbi alipoteza nafasi nyingine ya kuisawazishia Yanga bao,  baada ya kupokea pande maridadi la Banka  lakini mkwaju  wake ulipanguliwa na Manula na kuzaa kona ambayo haikuwa na faida.

Dakika 45 zilikamilika kwa Simba kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao moja.

Kwa ujumba, Simba ilitawala eneo la kiungo hatua iliyoinyima Yanga fursa ya kupanga mashabulizi yenye tija.

Uimara wa Shikalo pia ulikuwa kikwazo kwa Simba kujipatia mabao zaidi, baada ya kupangua mikwaju kadhaa ya hatari.

Kipindi cha pili, Simba iliuanza mchezo kwa kasi, dakika 46, Kanda alifunga bao la pili akiimalizia pasi nzuri ya Kagere, aliyewahadaa walinzi wa Yanga na kumpa nafasi ya mfungaji kufunga kirahisi.

Dakika ya 49, Kocha wa Simba, Sven Vanderbroec alifanya mabadiliko, alimtoa Kanda na nafasi yake kuchukuliwa na Hassan Dilunga.

Dakika ya 50,  Balama aliindikia Yanga bao la kwanza kwa shuti kali akiwa nje 18.

Bao hilo liliipa nguvu Yanga ya kumimina mashambulizikwenye lango la Simba, ambapo dakika ya 53, Banka aliindikia bao la pili kwa kichwa akimalizi krosi iliyochongwa na Adeyum Saleh.

 Dakika ya 59, Kocha wa Yanga, Charles Mkwasa alifanya mabadiliko alimtoa Abdulaziz Makame na nafasi yake kujazwa na Yikpe Gislein, huku Adeyum akimpisha Andrew Vicenti ‘Dante’.

Dakika ya 74, Jonesia alimlima kadi ya njano beki wa Yanga, Ally Mtoni ‘Sonso.

Dakika 89, John Bocco nusura aifungie Simba bao la tatu, baada ya mpira wake wa  kichwa aliunganisha krosi ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kugonga mwamba wa Yanga kabla ya Yondan kuuondoshwa kwenye eneo la hatari.

Dakika 90 za mtanange huo zilikamilika kwa timu hizo kutoka uwanjani zikiwa nguvu sawa baada ya kufungana mabao 2-2.

Simba:Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Tairone Santos, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Deo Kanda, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere, Clatous Chama na Francis Kahata.

Yanga: Farouk Shikalo, Juma Abdul, Adeyum Saleh, Ally Mtoni, Kelvin Yondani, Abdulaziz Makame, Mapinduzi Balama, Mohammed Issa ‘Banka’, Ditram Nchimbi, Papy Tshishimbi na Haruna Niyonzima.    

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles