26.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 3, 2022

ATHALI ZA KUZIDI KWA TINDIKALI ASILIA MWILI

Tindikali asilia inapozidi mwilini, huweza kusababisha tatizo la kuumwa viungo vya mwili.

 

NA JACKSON NYABUSANI - 0652 082 765     |     

MWILI wa binadamu kwa asili yake umeumbwa kwa namna ambayo viungo vyote vinaweza kufanya kazi kwa ufasaha kutegemeana na taarifa ambazo zinasafirishwa kutoka kwenye ubongo na kupelekwa kiungo husika.

Ili mwili uweze kufanya kazi vizuri na kusitokee tatizo lolote, haina budi kila kemikali ya asilia iliyopo mwilini iwe katika kiwango ambacho ni stahiki.

Miongoni mwa kemikali asilia ambayo inapatikana katika mwili wa binadamu ni hii inayojulikana kwa jina la kitaalamu Uric Acid.

Uric Acid ni kemikali asilia inayopatikana katika mwili wa binadamu. Kemikali hii hupatikana baada ya kuvunjwa vunjwa kwa vyakula ambavyo ndani yake kuna kundi la kemikali aina ya Purine ambayo baada ya kuvunjwa ndipo huzalisha Uric Acid.

Katika mwili wa binadamu, kiwango ambacho ni cha kawaida mtu kuwa nacho ni 2.4-6.0 mg/dL kwa mwanamke, na 3.4-7.0 mg/dL kwa mwanamme. Kiwango cha uric acid mwilini hupimwa kwa kutumia njia ya damu.

Kiwango hiki endapo kitazidi mwilini kitasababisha matatizo mwilini na hasa katika maeneo ya mwili ambayo ni maungio ya mifupa/jointi.

Katika maungio ya mifupa au jointi, mtu atapatwa na maumivu makali, kuvimba na kubadilika kwa umbile la maungio ya mifupa na kuwa kama kumepinda. Hali hii kitaalamu huitwa gout.

Pia kuzidi kwa kiwango cha uric acid mwilini kinaweza kuwa ni dalili ya magojwa kama ya ini, figo na saratani. Mwilini kemikali hii ya asilia hutolewa kupitia njia ya mkojo kama urea, tofauti na wanyama wengine au ndege ambao wao kemikali hii hutolewa kupitia kinyesi na wakati mwingine imekuwa na mwonekano kama chokaa iliyochanganyika na kinyesi, mfano kinyesi cha kuku.

Upatikanaji wa uric acid mwilini ni kupitia ulaji wa vyakula ikiwamo maharagwe yaliyokaushwa, maini, figo na baadhi ya vyakula vya baharini au seafood (sardines pamoja na tuna).

Pia uric acid mwilini hupatikana baada ya matokeo ya seli hai za mwili kuvunjika (seli kufa na kutengeneza purine ambazo nazo huvunjika na kutengeneza uric acid).

Kwa kuwa kiwango kikubwa cha uric acid kinasababisha matatizo ya kiafya, ni vyema kufahamu ni namna gani ambavyo mtu anaweza kuenenda ili kuhakikisha kiwango cha uric acid mwilini kinakuwa si cha kuweza kusababisha matatizo ya kiafya.

Miongoni mwa njia za kutumia katika kurekebisha kiwango cha uric acid mwilini, ni kuepuka vyakula vyenye kiasi kikubwa cha ‘Purine’ inayosababisha kupatikana kwa uric acid. Vyakula hivyo vya kuepuka ni pamoja na maini, figo pamoja na baadhi ya vyakula vya baharini kama vilivyotajwa hapo juu. Pia ni vyema kutumia vyakula vyenye kiasi kikubwa cha virutubisho pamoja na vitamin ambavyo kiafya vinasaidia kuondoa sumu mwilini.

Virutubisho na vitamini ambazo husaidia kurekebisha kiwango cha uric acid mwilini ni pamoja na vitamin B6, Vitamin C, madini ya magnesium.

Haya hupatikana katika matunda kama vile ndizi mbivu, machungwa, matikiti maji, maembe na mananasi. Pia juisi ya limao katika mwili husaidia katika kutengeneza chumvi aina ya calcium carbonate ambayo husaidia kuyeyusha (neutralize) tindikali asilia mwilini.

Aidha, sambamba na ulaji wa vyakula hivyo kwa mtu ambaye ana tatizo la kiwango kikubwa cha tindikali asilia mwilini (Baada ya vipimo vya kitaalamu), inashauriwa kutumia dawa zinazopunguza kuzalisha kwa uric acid mwilini. Lakini pia kusaidia kuondoa maudhi na maumivu makali ya viungio.

Miongoni mwa dawa hizo ni Allopurinol. Ili miili yetu iweze kuendelea kufanya kazi vizuri, inashauriwa kufanya uchunguzi wa kitaalamu ili kubaini upungufu mapema na kuepukana nao kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,573FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles