30.9 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Amwachisha mwanawe shule kisa uonevu

Akiwa 'darasani'

Aamua kumfundisha dunia ya biashara ofisini

JOSEPH HIZA,

VITENDO vya uonevu dhidi ya watoto na au vijana wanaoonekana machoni kuwa wanyonge au wenye kasoro fulani za kimwili au kiakili vikifanywa na wale wakubwa au wenye silka za kibabe imekuwa sehemu ya maisha katika mataifa mengi duniani hasa ya Ulaya.

Katika mataifa hayo watoto au vijana hasa katika mitaa yenye vurugu hulazimika kujiunga na magenge ya vijana yenye viongozi wake ili kujilinda dhidi ya uonevu wa magenge mengine korofi.

Magenge haya baadhi huenda mbali kutengeneza kanuni za kufuata unapojiunga sambamba na kiapo cha utii, ambacho  kiongozi humsomea mwanachama mpya neno kwa neno huku akifuatisha.

Mfano wa aina ya viapo ni kama hiki; “Mimi fulani bin fulani wa Sinza Kijiweni mjini Dar es Salaam, ninaapa kuzitii sheria na kanuni za genge la Sinza Kijiweni.”

Lakini pia vitendo hivyo vya kionevu dhidi ya wanyonge vimeshamiri mno kiasi cha kutisha katika shule za nchi hizo, hali unayoweza kufananisha japo ipo kwa kiwango kidogo katika baadhi ya shule hasa za sekondari Tanzania.

Nchini Tanzania kwa mfano wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza mara nyingi hujikuta wakikumbana na kila aina ya uonevu kutoka kwa kaka na dada zao hasa wale wa kidato cha pili ambao ni kama vile wanalipiza kisasi kwa walichofanyiwa huko nyuma.

Ukiachana na utangulizi huo, tukirudi katika makusudio yetu ya makala haya, wakati mtoto anapokabiliwa na kila aina ya uonevu tena usiostahimilika shuleni. Kuamua hatua ya kuchukua kwa mzazi ni jambo gumu mno.

Iwe kwa mtoto wako anashindwa kuendana na kazi za darasani au anakumbana na vitendo vibaya vya uonevu kutoka kwa wenzake kiasi cha kumnyima raha na kumfanya ashindwe kusoma au aichukie shule, kuna suluhu chache rahisi za kuchukua.

Lakini haikuwa hivyo kwa baba Lee Cooke wa nchini Uingereza, ambaye badala yake aliamua kumuondoa kabisa mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka tisa kutoka shuleni.

Mwanawe huyo kwa karibu miaka miwili amekuwa akionewa na wanafunzi wenzake kwa namna mbalimbali ikiwamo kudhihakiwa maendeleo yake duni darasani, kupigwa na kila aina ya vituko.

Mbaya zaidi kwa mujibu wa baba yake huyo, walimu na uongozi wa shule kwa ujumla wake haukuwa ukichukua hatua, kwa maana ya kufumbia macho maonevu na madhambi.

Lee Cooke
Lee Cooke

Baba yake huyo, meneja wa kampuni ya mali zisizohamishika huko Wolverhampton, West Midlands, alichagua kumwondoa shuleni na kuchukua jukumu la kumfundisha mwenyewe mtoto wake.

Ni pale mwanawe huyo alipokiri kuwa amekuwa akiandamwa na uonevu na wanafunzi wenzake darasani na hivyo Cooke ameamua kumfundisha mbinu za dunia ya biashara katika umri wa mapema.

Baba huyo mwenye kujivunia kwa hatua aliyochukua aliweka picha ya mwanawe wakati wa siku yake ya kwanza ya shule mpya ofisini ambayo ilisambaa mitandanoni kwa kasi.

Kuanza maisha kama mwanafunzi wa biashara, kijana huyo mdogo alionekana nadhifu katika shati na tai wakati akipokea simu akiwa mezani kwake chini ya uangalizi wa baba yake.

“Leo ni siku ya kwanza ya mwanangu mwenye umri wa miaka tisa kwa maisha mapya,” Cooke aliandika chini ya  picha hiyo.

“Baada ya kukabiliwa na uonevu kwa miaka karibu miwili shuleni, huko Wednesfield, Wolverhampton, nilimuondoa kutokana na kukosa ulinzi, msaada na ufisadi uliokithiri kwa uongozi wa shule, ambao ulificha maovu ndani ya kapeti dhidi ya matendo mabaya.”

Wakati yeye akitarajia kusoma mada zote muhimu kuhusu biashara, siku ya kwanza masomo ya msingi yakiwamo Hisabati, Sayansi ya Teknolojia na masuala ya simu yalifundishwa.

Kwa Cooke, habari nzuri ni kwamba mwanawe ameanza kufurahia kusoma tofauti na awali alipoipoteza shauku hiyo ya kusoma.

“Leo tumesoma Hisabati, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na masuala ya mawsiliano ya simu,” anasema.

Baba huyo aliyegeuka mwalimu anasema kwamba kwa kumwondoa mwanawe katika mazingira mabaya ya shule kunamfanya  apate uwanja mpana wa kujifunza, kukua na kujiendeleza na ametoa mwito kwa wazazi wengine kutokubali uonevu, dhuluma na ukandamizaji dhidi ya watoto wao shuleni.

“Ninatumaini ataonesha uonevu na dhuluma hizo na kuwaumbua wale walimu waliozifumbia macho kwa sababu maendeleo duni darasani hakumaanishi kuwa unastahili kuandamwa na wanafunzi kandamizi na kupuuzwa na walimu hao waliopaswa kukulinda!” Cooke anasema na kuongeza:

“Kamwe usikubali uonevu na simama imara kujilinda mwenyewe leo.”

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa mtandao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles