Aliyekuwa boss MSD mbaroni kwa tuhuma za utakatishaji, kusababisha hasara ya Sh bilioni 3

0
337

Kulwa Mzee, Dar es salaam

ALIYEKUWA Mtendaji Mkuu wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu, mwenzake wamepanda kizimbani wakikabiliwa na mashtaka matano ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka na kutakatisha zaidi ya Sh bilioni 1.6.

Washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate.

Wakili wa Serikali  Faraja  Nguka,  aliwataja washtakiwa kuwa Bwanakunu na  Mkurugenzi wa Logistiki MSD, Byekwaso Tabura.

Wakili Nguka akisoma mashtaka alidai kati ya Julai 1, 2016 na Juni 30, 2019 maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma kwa pamoja walitumia madaraka vibaya na kujihusisha na genge la uhalifu kwa ajili ya kujipatia faida.

Katika shtaka la pili inadaiwa kati ya Julai 1, 2016 na Juni 20, 2019 washtakiwa wote kwa pamoja waliisababishia MSD hasara ya  Sh 3,816,727,112.75.

Wakili Nguka alidai shtaka la tatu linamkabili Bwanakunu ambaye anatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka ambapo inadaiwa kati ya Julai 1, 2916 na Juni 30, 2019 katika maeneo ya Keko Wilaya ya Temeke kwa makusudi alitumia nafasi yake kulipa Sh 3,816,727,112.75 kwa wafanyakazi wa MSD kama nyongeza ya mishahara na posho bila ruhusa ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais na hivyo kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya kiasi hicho cha fedha.

Katika shtaka la nne washtakiwa wote wanadaiwa kati ya Julai 1, 2016 na Juni 30, 2019 katika maeneo tofauti ya Jamhuri ya Muungano Tanzania kwa pamoja waliruhusu uhifadhi mbaya wa vifaa tiba uliosababisha vifaa hivyo kuharibika hivyo kuisababishia MSD hasara ya Sh 85,199,879.65

Shtaka la tano ni la utakatishaji fedha ambalo linalowakabili washtakiwa wote,  inadaiwa kati ya Julai 1, 2016 na Juni 30, 2019 katika maeneo ya Keko Wilaya ya Temeke Mkoa wa Dar wa Salaam wote kwa pamoja walijipatia Sh  1,603,991,095.37 wakijua fedha hizo ni zao la uhalifu ambao ni kuongoza genge la uhalifu.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ambayo hayana dhamana kisheria hivyo walirudi rumande hadi Juni 18 mwaka huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here