24.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 17, 2021

Polisi Arusha waanza kujipanga kwa uchaguzi

Janeth Mushi -Arusha

JESHI la polisi mkoani Arusha limeanza kujipanga kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, huku Kamanda wa Polisi, Jonathan Shanna, akisema wanataka ufanyike kwa amani bila kutumia hata bomu moja la machozi.

Shanna aliyasema hayo jana jijini hapa wakati akizungumza kwenye kikao kazi kilichoshirikisha maofisa, wakuu wa polisi na waratibu wa jeshi hilo kuanzia ngazi ya kata.

“Uchaguzi mkuu wa mwaka huu jeshi la polisi tuna wajibu wa kuhakikisha unafanyika kwa  amani na utulivu, uchaguzi ufanyike bila kutumia bomu hata moja na ndo maelekezo tumepewa na IGP, katika wilaya zote uchaguzi ufanyike kwa amani na utulivu.

“Lakini hata hivyo naomba hili niseme kwa msisitizo, iwapo wananchi, wagombea au wapigakura katika mkoa wetu watatuita au watatuchokoza, hatutasita kuwachukulia hatua za kisheria ila wakitii sheria bila shuruti watafurahia uchaguzi, lengo letu ni kuhakikisha kila mmoja anatii sheria bila shuruti.”

Kuhusu kikao kazi hicho alisema askari hao wana wajibu wa kutoa elimu ya ulinzi shirikishi kwa wananchi waliopo katika kata zao ili hali ya usalama idumu.

“Leo tumewaita hapa ili kuwakumbusha majukumu ya kazi ambapo kutakuwa na mada ikiwa ni pamoja na ugunduzi na upelelezi wa makosa ya uchaguzi, ushirikishwaji wa jamii katika kufanikisha uchaguzi, elimu juu ya haki za raia katika uchaguzi na utayari wa jeshi la polisi katika kipindi chote kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Katika hatua nyingine, Shanna, alieleza kushangazwa na baadhi ya taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zikidai Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, ameanza kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

“Naomba nikuchomekee kidogo, nimeona kwenye mitandao wakikutuhumu kwamba unafanya kampeni, lakini mimi najiuliza kampeni zipi hizi unazozifanya mkoa mzima?

“Nilikuwa naongea na ma OCD wangu kwa kweli wanakupongeza kila kukicha kila siku uko wilaya moja kati ya wilaya zetu sita za mkoa wa Arusha na huko unasiistiza amani na utulivu, unasisitiza maendeleo, unahakikisha miradi iliyokwama inakwamuliwa.

“Mimi na ma OCD  tunasema huu ni uongozi unaoweka alama, tunaomba usikatishwe tama, tunaomba usirudi nyuma, dhamira yako ni njema unaupenda mkoa wako na nadhani kati ya mikoa inayomeremeta Arusha ni mmojawapo,”alisema.

Gambo anatajwa kuwa miongoni mwa wanaotaka kuwania katika Jimbo la Arusha Mjini kwa tiketi ya CCM, ambalo kwa sasa linaongozwa na Godbless Lema (Chadema).

Wengine wanaotajwa kuwania nafasi hiyo kwa tiketi ya CCM ni pamoja na mfanyabiashara  Philemon Mollel (Monaban), aliyekuwa Meya wa Jiji la Arusha Calist Lazaro, Edmund Ngemela, Mosses Mwizarubu, ingawa hadi sasa hakuna aliyethibitisha kwamba atawania nafasi hiyo.

Gambo

Kwa upande wake Gambo aliwapongeza askari hao kwa kuimarisha usalama katika Mkoa wa Arusha na namna walivyojiopanga kusimamia uchaguzi kwa amani na utulivu.

“Maelekezo yaliyotolewa na IGP na wewe umewaita askari wako hadi wa ngazi ya kata ili asitokee hata mmoja ambaye atasema hakusikia, nawapongeza kwa kuimarisha usalama ndani ya mkoa wa Arusha.

“Tukitoka nje ya Mkoa wa Arusha wanasema Arusha wanayoijua wao ilikuwa ni ya maandamano, vurugu, ilikuwa Arusha ambayo kila mtu akipata mawe yake Mirerani akipata visenti kidogo anaenda baa analewa anampiga mtu risasi, lakini tumeona matukio hayo yamekuwa historia.

“Japokuwa tunakwenda kwenye uchaguzi, zile kazi nyingine siyo kwamba zinakwenda likizo, lazima watu wafahamu kwamba tutafanya kazi ya uchaguzi na majukumu mengine ikiwemo kupambana na ujambazi yataendelea, wasione sasa hivi tunafanya semina maalum kwa ajili ya kujipanga kusimamia uchaguzi wakadhani  majukumu mengine yatasimama,”alisema.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

12,054FansLike
2,941FollowersFollow
18,400SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Latest Articles